Mwenyekiti Mwenza
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amesema ili kuweza
kuanzisha chama kimoja cha upinzani chenye nguvu, inahitajika viongozi
wa upinzani kujenga msingi wa uaminifu miongoni mwao.
Pamoja na kwamba hakutaka kutamka wazi kuwa uaminifu huo kwa sasa
haupo, Mwenyekiti huyo pia wa Chama cha NCCR-Mageuzi, amesisitiza kuwa
bado lengo la kuanzisha chama hicho kimoja cha Ukawa lipo palepale na
linaendelea kufanyiwa kazi.
Mbatia alikuwa akihojiwa katika kipindi kinachorushwa kila Jumapili
na Televisheni ya Azam. Alisema katika kuanzisha chama hicho, suala la
uaminifu miongoni mwa viongozi ni muhimu ili kufikia malengo halisi ya
uanzishwaji wa chama hicho.
Alipohojiwa kwamba, kwa sasa Ukawa hakuna uaminifu ndio maana bado
uanzishwaji wa chama hicho unasuasua, mbunge huyo wa Vunjo, aligoma
kueleza kwa uwazi zaidi kusisitiza kuwa uaminifu ni lazima katika suala
nyeti kama hilo.
Alisema kwa sasa azma hiyo ya kuwa na chama kimoja imeanza kuonekana
zaidi kwa vitendo kuliko maneno kwani kupitia umoja huo walisimamisha
mgombea mmoja wa urais hali iliyowapatia mafanikio.
“Ni kweli kwenye umoja wetu kuna migongano ya hapa na pale lakini hiyo ni kawaida lazima tuwe na fikra tofauti, lakini tungefikiria kwenye chanya zaidi ila bado kuna haja ya kujengeana uaminifu kwanza,” alisema.
Aidha, alisema uanzishwaji wa Ukawa ni wazo la NCCR-Mageuzi kwa kuwa
tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1991 kilikuwa na lengo la
kuunganisha nguvu ya upinzani.
“Kwa maana hiyo Ukawa ni mtoto wa NCCR-Mageuzi ambayo ni mama wa upinzani. Kususia vikao vya Bunge Akizungumzia kitendo cha wabunge wa upinzani kuendelea kususia vikao vya Bunge pindi inapotokea kutoelewana ndani ya chombo hicho, Mbatia alisema hiyo ndio njia pekee ya kupatiwa haki wanayoidai badala ya kukaa kimya.”
Hata hivyo, alipobanwa na kuhojiwa kwa nini wasitumie fursa
waliyonayo na kubaki ndani ya Bunge na kuwasilisha maoni yao, alisema
hiyo ni njia mojawapo ya kuonesha hasira waliyonayo juu ya mfumo uliopo
unaoliendesha bunge hilo.
“Hakuna mtu aliyesomea kuwa mbunge au Rais, mabunge yote yaliyopita yaliyoongozwa na Samuel Sitta na Anne Makinda, yote yalikuwa na malalamiko, lakini Bunge hili la 11 malalamiko yamezidi. Ndio maana na sisi tunaamua kutoka ikiwa ni njia ya kuonesha hasira hasa pale tusiposikilizwa,” alisema.
Kuhusu hoja kwamba kwa sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie
madarakani, Ukawa imeanza kudhoofu, Mbatia alikanusha hoja hiyo na
kusisitiza kuwa kwa sasa umoja huo ndio umeonesha mshikamano hasa
kutokana na matukio ya bungeni.
Ukawa na nguvu za Chadema Pamoja na hayo, Mbatia alisema kitendo cha
Ukawa kuinufaisha zaidi Chadema kwa kuwapatia wabunge wengi ni jambo
lililotegemewa kwani hata mwaka 1995 NCCRMageuzi nayo iliposimamisha
mgombea urais aliyekuwa na nguvu kipindi hicho, ilijipatia umaarufu na
mafanikio ya kisiasa.
Maridhiano bungeni Aidha, mbunge huyo alipongeza jitihada za Spika wa
Bunge, Job Ndugai za kurejesha maridhiano yaliyovunjika katika mkutano
uliopita baina ya wabunge wa upinzani na chama tawala na kusisitiza kuwa
hatua za spika huyo ni jambo zuri la kuungwa mkono.
Alisema kinachotakiwa ndani ya chombo hicho ni kuhakikisha taratibu
zilizowekwa zikiwemo kanuni za Bunge zinafuatwa huku akiendelea kumtupia
lawama Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa ndiye tatizo la mvurugano
ndani ya chombo hicho.
“Hata hivyo, Tanzania hii ni yetu sote, keshokutwa tunakutana na viongozi wa dini zote kuzungumza suala la amani ya nchi yetu. Naamini juhudi hizi zikiendelea tutafikia mahala pazuri,” alisema.
Post a Comment