MWANASIASA na mwanaharakati maarufu nchini, Tundu Lissu (49), ana
uwezekano mkubwa wa kushinda nafasi ya urais wa Chama cha Mawakili wa
Tanganyika (TLS) uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii,
Uchaguzi wa TLS ambao mwaka huu umetawaliwa na hali ya mvutano kati ya
chama hicho na serikali ya Rais Dk. John Magufuli, umepangwa kufanyika
mjini Arusha Jumamosi hii ya Machi 18.
Uchunguzi uliofanywa na Raia Mwema wa kuzungumza na baadhi ya mawakili,
majaji wastaafu na wanasheria maarufu nchini umebaini kwamba Lissu; kwa
sasa, ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kwa sababu kubwa
tatu.
Sababu hizo tatu zinazodaiwa kumbeba Lissu kwenye uchaguzi huo wa aina
yake ni – dhamira ya wanachama wa TLS kuwa na chama kinachotimiza
majukumu yake ipasavyo, idadi kubwa ya wapiga kura kuwa vijana ambao
wanampenda Lissu na pia kutaka kuionyesha serikali kuwa chama hicho ni
huru.
“ Sababu ya kwanza ni kwamba ingawa TLS ni mojawapo ya taasisi kongwe
nchini, ikiwa imeanzishwa mwaka 1954, haijulikani sana miongoni mwa
Watanzania.
“ Ni kama vile imelala. Lakini, kama umebaini, tangu ijulikane kwamba
Lissu atawania nafasi hiyo, vyombo vya habari vinaandika na watu
wanazidi kuifahamu. Tumepata picha kwamba kumbe taasisi yetu inamhitaji
mtu wa aina yake,” alieleza mmoja wa wanasheria aliyezungumza na gazeti
hili kwa masharti ya kutotajwa jina.
Mahojiano ya gazeti hili na mawakili kadhaa yameonyesha pia kwamba
ingawa TLS ina wanachama takribani 5,000, zaidi ya nusu ni wanasheria
vijana ambao wengi wao wanaelezwa kumuunga mkono Lissu, ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa chama hicho.
Wanasheria hao vijana wanaelezwa kuwa na mwelekeo wa kutaka mabadiliko
makubwa ya uendeshaji wa taasisi hiyo na wanamwona Lissu kama mtu pekee
anayewakilisha taswira hiyo ipasavyo.
Kubwa zaidi linalodaiwa kumsaidia Lissu ni hatua ya serikali kuonekana
haimtaki Lissu, kiasi cha mmoja wa mawaziri wa Magufuli, Dk. Harrison
Mwakyembe, kutishia kukifuta chama hicho endapo kitaendeshwa katika
misingi ya kisiasa.
Dk. Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba na pia
mwanasheria kitaaluma na mwanachama wa TLS alitoa tishio hilo wakati
akizungumza na ujumbe wa mawakili uliomtembelea ofisini kwake mjini
Dodoma mapema mwezi huu.
“ Mimi nisingeweza kumchagua Lissu kuwa Rais wa TLS. Sidhani kama ni mtu
sahihi kwa chama chetu. Lakini serikali ni kama imemsaidia apate nafasi
hiyo na nadhani sasa atapata.
“ Serikali imemfuatafuata sana na sasa wanasheria wanasema enough is
enough. Imetosha. Mwakyembe alisema wataifungia TLS. Naona watamchagua
Lissu ili waone kama ana ubavu wa kukifunga chama hicho,” alieleza mmoja
wa majaji waliozungumza na gazeti hili pasipo kutaka kutajwa majina
yao.
Maelezo ya Mwakyembe kwa ujumbe wa TLS uliotembelea Dodoma ukiongozwa na
Rais anayemaliza muda wake, John Seka, yalifanana na yale ya Rais
Magufuli aliyoyazungumza Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa Siku ya Sheria, Magufuli alionya kwamba kuna watu
wanataka kuingiza siasa kwenye uchaguzi wa TLS na kwamba serikali yake
haitashirikiana na TLS inayosukumwa na upinzani.
“ Nitapata shida sana kuteua Jaji kutoka Tanganyika Law Society kama
mtakuwa mnafanya mambo yenu kwa kutumiwa. Niwaambie kwamba kama mtafanya
kazi zenu bila kujali maslahi ya taifa, mtashindwa,” alionya.
Mmoja wa mawakili maarufu nchini, Alex Mgongolwa, aliliambia gazeti hili
juzi Jumatatu kwamba hadhani kwamba Lissu ni mgombea wa kudharauliwa
katika kinyang’anyiro hicho.
“ Nadhani demography ( suala la umri) kwa sasa linampa faida mgombea
anayeungwa mkono na vijana. Kwa hali ilivyo sasa, Lissu anaungwa mkono
na mawakili wengi vijana ambao ndiyo wanaunda sehemu kubwa ya wapiga
kura. Nadhani Lissu ana nafasi,” alisema Mgongolwa.
Kwa upande wake, wakili mwingine ambaye amewahi pia kuwa mwandishi wa
habari, Aloyce Komba, alisema wapo mawakili wenye wasiwasi na Lissu
lakini kuna mazingira yaliyopo sasa yanampa nafasi.
“ Siwezi kusema kwamba mimi nitampigia kura yangu Lissu lakini nasema
kuna mazingira ambayo yanampa faida. Watu wanataka kuona TLS iliyo
ngangari na wanadhani Lissu anaweza kuifanya hivyo.
“ Kuna suala la umri wa wapiga kura ambalo ni la muhimu. Kwenye chaguzi
zote za karibuni, mgombea aliyeungwa mkono na mawakili vijana ndiye
hatimaye alishinda. Kwa sasa, inaonekana upepo wa vijana uko kwa Lissu
na hivyo huwezi kumdharau,” alisema wakili Komba.
Mwakyembe
Akizungumza na ujumbe huo wa TLS, Mwakyembe alisema serikali haitakuwa
tayari kuvumilia wakati chama hicho kikianza kutimiza mambo
yaliyosababisha kuanzishwa kwake na kujiingiza katika siasa.
“Kama wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS
ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya
kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa sheria yenu iko
chini yetu.
“Mkiharibu kwa lolote wizara ndiyo yenye wajibu wa kuwatolea maelezo
katika hilo mnalotaka kulifanya sasa kuna mgongano wa maslahi, je, ninyi
kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?
“Serikali haina shida na wanachama wa TLS kuwa wanachama wa vyama vya
siasa ila tatizo linakuja pale mnapotaka kuchagua viongozi ambao tayari
wanazo kofia mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa,” alisema na
kuongeza:
“Hao ndio watakaobeba sura na mtazamo au mwelekeo wenu, hapo hatuwezi
kukubali kwa kuwa watatenganishaje uongozi wao katika chama husika na
uongozi wao ndani ya TLS, huo sasa ndio mgongano wa maslahi.
“Ndio maana mwanasheria yeyote akiingia katika utumishi wa umma uwakili
wa kujitegemea anauweka pembeni ili kuepuka mgongano wa maslahi,”
alisema Mbunge huyo wa Kyela.
Maelezo ya Tundu Lissu
“Mimi nina misimamo thabiti ya kutetea utawala wa sheria, utawala wa
kikatiba na utawala bora. Ni mpinzani wa CCM kwa sababu hiyo. Kazi yangu
bungeni imejengeka katika misingi hiyo. Kama nikichaguliwa Rais wa TLS
huo ndio utakuwa msimamo wangu.
“Kwa bahati nzuri, misingi ninayoisimamia ndio pia ni malengo ya
kisheria ya TLS kwa mujibu wa Sheria iliyoianzisha, yaani Sheria ya
Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Sura ya 307.
“Kwa miaka mingi, TLS imeacha kusimamia misingi hii kwa hofu ya kuwaudhi
watawala. Kumekuwa na dhana kwamba tukiwa wapole basi mambo yetu
yataenda vizuri. Mambo ya nchi yetu hayajaenda vizuri kwa sababu ya
ukimya wa TLS.
“Na wala mambo ya mawakili walio wengi hayajaenda vizuri pamoja na
kuwako ukimya huu. Nikiwa Rais wa TLS ukimya huu utaisha. Wanaotaka
kuendesha nchi yetu kama mali yao binafsi, bila kujali sheria na Katiba
yetu; wanaotaka kutawala bila vizingiti vya sheria na Katiba, hao ndio
wanaoogopa kugombea kwangu. Je, ubunge wangu na uanasheria mkuu wangu wa
Chadema utakuwaje???
“Kazi ya Rais wa TLS si full-time job (si ya kukaa ofisini kila siku),
ni kazi ya muda tu. Sidhani kama Rais wa TLS ana ofisi ya kudumu pale
Makao Makuu. Hata kazi ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema si full-time job.
Sina ofisi Makao Makuu ya Chadema. Kazi ya ubunge ni full-time lakini
ina flexibility kubwa sana.
“Nje ya vikao vya Bunge na Kamati, mimi ndiye ninayepanga ratiba yangu.
Kwa sababu hiyo, pamoja na majukumu mengi niliyo nayo, ninaamini
nitapata muda wa kutekeleza majukumu ya Rais wa TLS. Wanaopiga kelele,
akina Mwakyembe na Magufuli, wanaogopa si Chadema bali wanaogopa TLS
yenye nguvu na inayojitambua.
“Hofu yao sio hofu ya Chadema, ni hofu kwamba wanasheria wakiamka katika
umoja wao wana nguvu kubwa ajabu kwa sababu ya unique position
waliyonayo kisiasa na kijamii. Kwa hiyo, kwenye uchaguzi huu wa TLS,
choice iliyopo mbele ya wapiga kura si choice ya Chadema au CCM bali ni
choice kati ya TLS inayotambua wajibu wake na TLS inayoogopa wajibu huo.
It's between change or status quo (ni kati ya wanaotaka mabadiliko au
kubaki hapa tulipo), alisema Lissu.
Wiki iliyopita, Kamati ya Uteuzi ya TLS ilitangaza majina ya wanachama
watano wa chama hicho waliopitishwa kuwania urais wa chama hicho na
nafasi nyingine.
Wagombea hao watano waliotangazwa kuwania nafasi hiyo ni Lissu, Francis
Stolla, Victoria Mandari, Godwin Mwapongo na Lawrance Masha.
Stolla amewahi kuwa Rais wa TLS Kwa takribani vipindi viwili huku Masha
akiwa amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana na pia Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi.
Tume ya uteuzi ya TLS inaongozwa na Rais mstaafu wa TLS, Kibuta
Ongwamuhana na wajumbe wengine ni Jaji Augusta Bubeshi, Kalolo Bundala,
Ibrahim Bendera na Akida Modest.
Rais wa TLS ambaye amemaliza muda wake wa mwaka mmoja, Seka aliondolewa
katika nafasi hiyo na kamati hiyo kwa madai ya kupoteza sifa. Ni yeye na
mwenzake Nmbute Akaro ndiyo pekee waliokatwa kwenye majina hayo.
TLS imeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 307 ya Mwaka 1955 iliyorasmishwa
na Bunge baada ya Uhuru kupitia Sheria ya Judicature and Application of
Laws Act (JALA) ya Mwaka 1961.
2 comments
this is great https://empireict.net/
ReplyEmpire ICT Solutions Co. Ltd
ReplyPost a Comment