Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Mchanganuo Mzima wa Bajeti ya Serikali 2016/ 2017 Iliyosomwa Jana Bungeni, BOFYA HAPA Kujua nini Kimepanda na Nini Hakijapanda

SERIKALI imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53, ambayo nguvu kubwa imewekwa katika kukusanya mapato kwa kulinda viwanda vya ndani na kubana matumizi ya serikali ili kuelekeza sehemu kubwa ya matumizi katika maeneo ya vipaumbele.

Katika bajeti hiyo, bidhaa za lazima zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru wa barabara na maji ya kunywa, havijaguswa huku bidhaa za starehe kama bia, sigara, soda, juisi na nyingine kama nguo za mitumba, huduma za kupanga nyumba na uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa kodi, huku kiinua mgongo cha wabunge, kufutiwa msamaha wa kodi.

Aidha, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ikiwemo mapato ya taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Mafuta (EWURA), Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine za udhibiti, sasa yatapelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo mahitaji yao ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa ya mapato waliyokusanya.

Aidha, maduka ya kutoa huduma katika majeshi, yamefutiwa kodi rasmi na badala yake, Serikali inajipanga kuongeza posho kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na ofisi zote za Serikali, zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni asiyetumia mashine za kodi za kielektroniki (EFD’s).

Kodi juu
Katika bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi ni pamoja na vinywaji baridi, kutoka Sh 55 kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa forodha katika maji ya matunda (juisi) yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa nchini, ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka 11 kwa lita. Juisi zinazotokana na matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru wake pia umepanda kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 210 kwa lita.

Bia, vilevi, mvinyo
Kwa upande wa bia, serikali imependekeza bia inayotokana na nafaka ya hapa nchini, ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru upande kutoka Sh 409 kwa lita mpaka 430.

Bia zingine, ushuru wake pia umepanda ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729 kwa lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu, ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita mpaka Sh 534.

Kwa upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu zilizolimwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka Sh 192 kwa lita mpaka Sh 202.

Ushuru wa mvinyo unaotengenezwa na zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali, havikuachwa nyuma maana ushuru umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.

Sigara
Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya hapa nchini kwa kiwango angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi Sh 11, 854 kwa kila sigara 1,000.

Kwa upande wa sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa kila sigara 1,000.

Sigara zenye sifa tofauti na hizo, ambazo hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya ndani, ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285 hadi Sh 50,700 kwa kila sigara 1,000.

Katika tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa kuwa sigara, ushuru wake umeongezeka kutoka Sh 24,388 hadi Sh 25,608 kwa kilo huku ushuru wa sigara aina ya Sigar ukibaki kuwa asilimia 30.

Vilainishi, gesi asilia, simu juu
Katika mafuta ya kulainisha mitambo, ushuru umepanda kutoka Sh 665.50 kwa lita hadi Sh 699 kwa lita, huku ushuru wa grisi za kulainisha mitambo, ukipanda kutoka senti 75 kwa kilo, hadi senti 79 kwa kilo.

Gesi asilia pia ushuru umepanda kutoka senti 43 kwa futi za ujazo mpaka senti 45 kwa futi za ujazo.

Kuhusu viwango vya ushuru wa kuhamisha fedha kwa kutumia simu, serikali imependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10, kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu, katika kutuma na kupokea fedha, badala ya ushuru huo kutozwa tu katika kutoa fedha.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, kwa utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya wa kuhamisha sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.

Ulaji wa wabunge, hisa
Kwa upande wa kiinua mgongo cha wabunge wakati wa kustaafu, sasa kitatozwa kodi kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa.

Aidha, mapato yote yatokanayo na hisa katika kampuni mbalimbali sasa yatatozwa kodi, baada ya kufutwa kwa msamaha kwa waliokuwa wakimiliki hisa chini ya asilimia 25.

Kodi ya mishahara
Katika kodi inayokatwa katika mishahara (P.A.Y.E), imepunguzwa kutoka asilimia 11 mpaka tisa kwa wafanyakazi wanaopata mshahara wa kuanzia Sh 170,000 lakini hauzidi 360,000. Kwa wanaopata zaidi ya 360,000 lakini haizidi 540,000, watakatwa Sh 17,100 pamoja na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.

Kabla ya hapo walikuwa wakikatwa Sh 20,900 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.

Wanaopata zaidi ya Sh 540,000 lakini haizidi Sh 720,000, watakatwa Sh 53,100 pamoja na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi 540,000.

Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 56,900 na hiyo asilimia 25 ya kiasi kilichozidi 540,000. Kwa wanaopata zaidi ya Sh 720,000 wao watakatwa Sh 98,100 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh 720,000.

Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 101,900 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kilichozidi Sh 720,000.

Kodi za nyumba
Serikali pia imependekeza malipo ya kupanga nyumba, nayo yatozwe kodi ambayo haikuweka kiwango, ila imependekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, apewe mamlaka ya kukadiria kiwango cha chini na cha juu cha mapato yapatikanayo na pango ili yatozwe kodi.

Kodi za nyumba, usajili magari, pikipiki
Mbali na mapato ya kodi za nyumba, Serikali imependekeza kupandisha ushuru wa kusajili magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa kila gari na kutoka Sh 45,000 hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.

Kwa watumiaji wa namba binafsi za magari, ada sasa itapanda kutoka Sh milioni 5 kila baada ya miaka mitatu mpaka Sh milioni 10.

Kodi ya majengo
Aidha, kodi za majengo sasa hazitakusanywa na halmashauri, badala yake TRA ndiyo inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria, kukusanya, kuhifadhi na kuiwakilisha katika halmashauri husika.

Mbali na TRA kupewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, serikali pia imependekeza kupunguza misamaha ya kodi za majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.

Ulindaji wa Viwanda
Saruji aina ya (HS Code 2523.29.00) zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ushuru wake wa forodha umepandishwa kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35 ili kulinda saruji inayozalishwa nchini dhidi ya ushindani wa bei ya saruji kutoka nje ya nchi.

Kwa bidhaa za chuma ikiwemo mabati kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nazo ushuru umetoka asilimia 0 mpaka 10, ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini, huku bidhaa za nondo kutoka nje nazo zikipandishwa kodi kutoka asilimia 10 mpaka 25, kwa nia ya kulinda viwanda vya ndani.

Nyavu za kuvua samaki kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushuru wake umepanda kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 huku vichujia vya vilainishi na petroli kutoka nje ya nchi vikiongezwa ushuru kufikia asilimia 25 kutoka asilimia 10, ili kulinda bidhaa za ndani.

Sukari, ngano, mitumba, mafuta ya kula
Katika sukari, serikali imekusudia kupunguza msamaha wa kodi na hivyo waagizaji wa bidhaa za sukari kutoka nje watalazimika kuanza kulipa ushuru wa asilimia 15 kutoka asilimia 10, huku ikitarajiwa kuongezeka zaidi na kuwa asilimia 20 mwaka 2017/18 na asilimia 25 mwaka 2018.19, ili kulinda viwanda vya ndani.

Kwa upande wa ngano kutoka nje, ushuru umepunguzwa kutoka asilimia 35 mpaka 10, kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha kulingana na mahitaji.

Kwa upande wa nguo na viatu vya mitumba Serikali imepandisha ushuru kutoka dola za Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4 kwa kilo, kwa nia ya kudhibiti nguo hizo lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia uingizaji wake.

Kwa upande wa mafuta ya kula kutoka nje nayo ushuru umepanda kutoka asilimia 0 mpaka 10 kwa mafuta ghafi ya kula, ili kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta na viwanda vya ndani.

Tozo za pamba, kahawa, korosho
Miongoni mwa tozo zilizofutwa kuondoa kero kwa wananchi ni mchango kwa kila kiwanda cha kuchambua pamba wa Sh 450,000 na ada ya vikao vya halmashauri wakati wa kujadili wafanyabiashara wa pamba ya Sh 250,000.

Kwa upande wa kahawa, Serikali imefuta ada ya leseni ya kusindika kahawa ya dola za Marekani 250, huku ushuru wa kusafirisha korosho wa Sh 50 kwa kilo, ukifutwa.

Tozo zingine zilizofutwa katika korosho ni ushuru wa chama kikuu cha ushirika Sh 20 kwa kilo, gharama za mtunza ghala Sh 10 kwa kilo, kikosi kazi cha kufuatilia masuala mbalimbali Sh 10 na makato ya unyaufu.

Pia Serikali imepanga kuendelea kufuta tozo nyingine zinazokatwa na halmashauri, wakala na mashirika katika mazao ya wakulima, baada ya kufanya tathmini za kina.

Maduka kambi za jeshi
Serikali imependekeza kufuta msamaha wa kodi uliokuwa ukitolewa katika maduka na migahawa maalumu kwa ajili ya askari wa majeshi, kutokana na msamaha huo kutumiwa vibaya na kupoteza mapato ya serikali na badala yake, askari watapata posho mpya juu ya posho ambazo wamekuwa wakipewa.

WAZIRI WA MAGUFULI 'AMPIGA' LOWASSA

  Adai serikali haijalenga wafanyabiashara waliosaidia upinzani kwenye kampeni. Asema hataki kuwa waziri ombaomba kwa madai nchi nyingine zinalazimisha kukubali ndoa za jinsia moja ili upate msaada
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
.....................
Ikiwa zimepita siku 40 tangu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kusema baadhi ya wafanyabiashara waliounga mkono upinzani wanasumbuliwa kwenye kodi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amemjibu bila kumtaja jina moja kwa moja.
 
Januari Mosi, mwaka huu, akitoa salamu za mwaka mpya katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli, Lowassa alisema amepokea malalamiko ya kuwapo kwa uonevu na vitisho kwa wadau walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani wakati wa kampeni.
 
Alisema hali hiyo ilitokea ilhali hatua ya wafanyabiashara hao haikukiuka Katiba, hivyo kuzitaka idara zinazohusika kuchukua hatua ili kuepusha  matatizo yasiyo ya lazima.
 
“Imeanza kutokea tabia ya kuwalaumu na 'kuwa-harass' (kuwasumbua) wale waliounga mkono vyama vya upinzani. Wanawa-harass kwenye kodi, nasikia wanawa-harass kwenye miradi na hata mitaani, hili si jambo zuri,” alisema Lowassa.
 
DK. MPANGO AMJIBU  
Jana, Dk. Mpango akizungumza na wafanyabiashara kwa lengo la kufahamiana na kuelezana mikakati ya serikali, alisema operesheni iliyoendeshwa bandarini kwa wafanyabiashara waliokwepa kulipa kodi, haikuwa na lengo la kuwabana wale waliosaidia upinzani wakati wa uchaguzi mkuu.
 
Alisema hatua ya serikali ya kukusanya kodi kwa nguvu kwa wafanyabiashara hao haikuwa na lengo la kuwanyanyasa.
“Dhana iliyopo sasa kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini ya makontena kuwa iliwalenga baadhi ya wafanyabiashara waliousaidia upinzani, si ya kweli,” alisema.
 
Kauli hii ya Dk. Mpango inatafsiriwa  ilikuwa ikimjibu kumjibu Lowassa kwa kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kiongozi huyo pekee  aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndiye alijitokeza hadharani na kulalamikia kunyanyaswa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiunga mkono upinzani wakati wa kampeni.
 
Akizungumza na wafanyabiashara hao jana, Dk. Mpango alisema serikali ya awamu ya tano inatambua mchango wa wafanyabiashara hivyo itashirikiana nao katika kujenga uchumi wa nchi.
 
Alisema dhana kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini iliwalenga wafanyabiashara waliowasaidia wapinzani wakati wa kampeni si ya kweli.
 
“Serikali ya Rais Dk. John Magufuli inatambua umuhimu wa uwekezaji katika uchumi wa nchi. Dhamira yangu ni kufanya kazi na wafanyabaishara wakubwa na wadogo,” alisema Dk. Mpango.
 
Alisema serikali ya Rais Magufuli haitawavumilia wafanyabiashara wachache ambao wanakwepa kodi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa itatumika sheria na hakuna mfanyabishara yeyote atakayeonewa.
 
Alisema kama kutakuwa na mfanyabishara atakayeonewa na mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), atoe taarifa wizarani haraka.
 
Aliongeza kuwa hapendi kuwa waziri ombaomba kwa kuwa amechoka kuwasindikiza wengine na kusema masharti ya kuomba misada ni makubwa na mengine hayatekelezeki, akitolea mfano wa kukubali sheria ya ndoa ya jinsia moja.
 
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwahudumia wanachi kwa kuwapa huduma bora za kijamii pamoja na kuwa na uchumi imara, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kukusanya mapato.
 
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango aliwaambia wafanyabiashara hao katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, serikali itafuta ushuru na tozo ndogo ndogo ambazo zimekuwa kero kwa wafanyabiashara.
 
Kadhalika, alisema bajeti hiyo itajielekeza katika kujenga uchumi imara wenye viwanda, miradi mikubwa itakayoleta matokeo makubwa na ajira nyingi pamoja na maeneo wezeshi kwa ajili ya kujenga viwanda kama vile uwapo wa umeme wa uhakika, bandari na ardhi.
 
Dk. Mpango alisema serikali imeziagiza taasisi zake zinazojihusisha na tozo kuorodhesha na kuleta aina zote za tozo ambazo wanatoza ili kuzifuta.
 
Alisema serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa uwekezaji katika uchumi, hivyo itashirikiana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
 
Waziri huyo alisema katika bajeti ijayo serikali itajielekeza katika viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana nchini kama vile misitu, uvuvi, madini na kilimo.
 
Dk. Mpango alisema kutajengwa viwanda vikubwa vitakavyoweza kuajiri idadi kubwa ya watu kama vile kiwanda cha nguo, viatu na mafuta ya kupikia.
 
Alisema kwa sasa msajili wa hazina ameshaelekezwa na ameanza kufanya uchambuzi kwa viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi inavyotakiwa.
 
Dk. Mpango alisema serikali itawanyang’anya wamiliki wa viwanda hivyo na kuwapatia wabia ambao wanaweza kuviendeleza.
Alisema bajeti ijayo pia itajielekeza katika ujenzi wa reli ya kati ya kisasa ambayo inahitaji Sh. trilioni nane hadi tisa kukamilisha ujenzi wake, na serikali haiwezi kujenga kwa fedha za bajeti.
 
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na Sera kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Felix Mosha, alisema serikali inapaswa kutafuta mfumo ambao utalinda viwanda vya ndani, pamoja na utaratibu wa kuwekeza katika kilimo.
Alisema hakuna taifa litakalokuwa kiuchumi bila ya kuwekeza katika kilimo.
 
Rais wa Chama  cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga, alisema tozo nyingi ambazo wafanyabishara wanatozwa, hazina umuhimu wowote.
 
Alisema bandarini kuna majangili wengi wa ushuru na kodi, huku akipendekeza malipo yote kulipwa kwa shilingi badala ya dola na kuongeza kuwa TRA inapaswa kukusanya tozo ya kuhifadhi mizigo bandarini badala ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
 
CHANZO: NIPASHE

AHADI YA SH.BILIONI 12.3 YA RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI YA MAOMBI YA UENDESHAJI WA MAHAKAMA YATIMIA LEO.

Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango (Katikati) akiwakabidhi Naibu waziri wa katiba na sheria, Amon Mpanju(kulia) na Mtendaji mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga cheki ya shilingi Bilioni 12 na milioni mia tatu ikiwa ni kutimiza ahadi  ya Rais Dkt. John Pombe Josef Magufuli aliyoahidi siku alipokuwa mgeni rasmi siku ya Mahakama hapa nchini ikiwa ni siku tano tuu tangu siku ya kuahidi.
Waziri wa Fedha Mipango, Philip Mpango (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusiana na kutimiza ahadi aliyoiahidi Rais  Dkt. John Pombe Josef Magufuli alipoahidi katika maadhimisho ya siku ya mahakama hapa nchini. Kulia ni Naibu waziri wa katiba na sheria, Amon Mpanju na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile. 
Mtendaji mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga (kushoto)akimshukuru Rais  Dkt. John Pombe Josef Magufuli kwa kutimiza ahadi yake aliyoiahidi siku ya maadhimisho ya siku ya mahakama. kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.

 Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii 
WIZARA ya Fedha na Mipango imetoa sh.bilioni 12.3 kwa ajili shughuli za mahakama ikiwa ni sehemu ya ahadi ya  Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyoiahidi katika kilele cha maadhimisho ya  siku ya mahakama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema fedha hiyo imetolewa kwa kutimiza ahadi ya Rais ya uendeshaji wa shughuli za mahakama.

Mpango amesema kuwa ahadi ya Rais ilikuwa ni ya siku tano ambazo zimetimia kwa kutoa hundi ya sh.bilioni 12.3 ambazo zitakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa.

Amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kutokana na ahadi hiyo imefanya kuweka wazi juu ya fedha hizo kwa waandishi wa habari.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju amesema lengo ni kuongeza kasi kwa mashauri yaliyopo kuondoshwa  pamoja na waliokwepa kodi  yashughulilikiwe.

Ahadi ya Rais ilitolewa baada ya maombi ya Jaji Mkuu, Othman Chande katika maadhimisho ya  kuanza kwa mwaka wa mahakama kudai kuwa wana uhaba fedha za maendeleo  katika kuweza kuendesha shughuli za kimahakama.
Naibu waziri wa katiba na sheria, Amon Mpanju akisaini dafari la wageni mara baada ya kuwasili katika ofisi za wizara ya fedha na mipango jijini Dar es Salaam leo. 
Mtendaji mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga (kushoto) akisaini kitabu cha wageni leo alipowasili katia ofisi za wizara ya fedha na mipango jijini Dar es Salaam leo.
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top