
ASHANGAA SMZ KUZIDIWA NGUVU, UAMSHO YAKUBALI KUSHIRIKI MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Ibrahim Yamola
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ‘kudhibiti wahuni wanaotaka kuvuruga amani visiwani humo’.
Kauli hiyo ya Pengo ni ya  kwanza tangu kuibuka kwa vurugu visiwani Zanzibar mapema mwezi huu, na  kusababisha uharibifu wa mali, huku makanisa yakilengwa zaidi na kikundi  kinachojiita cha Jumuiya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI).
Pengo  alitoa kauli hiyo wakati wa ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la  Msalabani Bagamoyo, mkoani Pwani, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu  wa Shirika la Roho Mtakatifu, utakaofanyika kwa siku 30 kuanzia jana.
Kardinali  Pengo alisema, ‘wahuni hawawezi kuizidi Serikali makini’.“Makanisa yetu  yamecomwa moto na watu wahuni. Kama Serikali ipo na haiwezi kuchukua  hatua dhidi ya wahuni, usalama uko wapi?” alihoji Kardinali Pengo.
“Wahuni  wanaweza kutuunguzia makanisa saba kwa mpigo, lakini mbele ya hapo kuna  makanisa kadhaa ambayo yalikwishaunguzwa na kubomolewa na hao wahuni,”  alisema.Pengo aliendelea kuhoji, “Kama sasa wahuni wameishinda nguvu  Serikali ya watu kwa hiyo tutawaliwe na wahuni na wafanye lile  wanalolitaka, tunajiuliza tunakwenda wapi?
Mara baada ya vurugu  za Zanzibar, jopo la maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali, walifanya  mazungumzo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), huku wakiituhumu  kushindwa kudhibiti vitendo vya uchomaji moto makanisa na kuihadharisha  kuchukua hatua za haraka.
Jana, Pengo alilitaka shirika hilo  kumsaidia Askofu Augustine Shayo wa Jimbo Katoliki Zanzibar, kuunganisha  nguvu zao katika harakati za kuimarisha amani.
Pengo alisema  mbali ya vurugu hizo, hivi sasa utumwa bado unandelea kukithiri nchini,  hususan kwa viongozi wa Serikali kuwakandamiza wananchi wa hali ya  chini.
Alisema wapo baadhi ya viongozi wanaotaka utumwa uendelee kuwapo kutokana na matendo yao dhidi ya wananchi.
“Tanzania  ni huru sawa, lakini mimi sitaki kusadiki kuwa ni huru kwa kila mmoja  na kila Mtanzania, wapo watu ambao wangependa wao waneemeke hata kwa  madhara ya wengi bila huruma hadi siku ya leo,” alisema na kuongeza:
“Tangu  Shule ya St. Marian inaanzishwa, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa  wakitaka watoto wao wakasome pale na watoto wa maskini wasipate nafasi.”
Alitoboa  siri kuwa ‘kuna barua za maombi zisizo za msingi ambazo amekuwa  akipelekewa Askofu Shayo na kuzikataa, na wakati mwingine amekuwa  akitishiwa maisha, kwani wapo wanaotaka kuwasomesha watoto katika shule  nzuri ili waendele kujineemesha. Sasa huu sio utumwa?’
Kardinali  Pengo alililitaka Shirika la Roho Mtakatifu kutumia mkutano huo  kuendelea kuhimiza amani hapa nchini na kutupia jicho Zanzibar, ambako  amani inavurugika kwa matendo ya watu aliowaita wahuni.
Mkutano wa Shirika
Kwa  mujibu wa Makamu Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, Padre John Kuff  kutoka Ghana, mkutano huo unafanyika Afrika kwa mara ya kwanza, tangu  kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1868.
Tanzania ni mwenyeji wa  mkutano huo wa 20 ambao umekuwa ukifanyika kila baada  ya miaka sita, na  mkutano wa mwisho ulifanyika Ureno mwaka 2004.
Baadhi ya nchi zitakazoshiriki mkutano huo ni Canada, Nageria, Ureno, Ufaransa, Ghana, Uingereza, Irand na mwenyeji Tanzania.”
Akizungumzia  shirika hilo, Pengo alisema wakati linaanza kazi nchini walikuta amani  imevurugika, lakini walifanya kazi kubwa amani ikarejea, hivyo alilitaka  kusimamia ukweli hata kama watu wengine watawabeza.
Kipozi aahidi amani
Akitoa  salamu za Serikali kanisani hapo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed  Kipozi alisema washiriki wa mkutano huo wawe na amani kwani ulinzi  utaimarishwa wakati wote.
“Kwa siku zote 30 za mkutano huu ulinzi na usalama utaimarishwa ili kuhakikisha mnafikia malengo yenu,” alisema Kipozi.
Mwananchi
Post a Comment