Waandishi Wetu, Dar na Dodoma
MABADIKO ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012, iliyopitishwa Aprili mwaka huu, imeendelea kuzua mtafaruku sehemu mbalimbali nchini, huku wabunge wakishinikiza kuwa, sheria hiyo inapaswa kurejeshwa bungeni ili ijadiliwe upya.
Jana, wabunge waliunga na wafanyakazi kupinga kipengele cha sheria hiyo kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, au miaka 60 kwa mujibu wa sheria.
Hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe upya ilitolewa na Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.
Hoja ya Jafo ilitokana na kuwapo kwa taarifa kuwa, zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini wameacha kazi huku wengine zaidi ya 4,000 wakiwa tayari wamewasilisha barua za kuacha kazi kutokana na sheria hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitofautiana na wenzake pale aliposema kuwa sheria inayolalamikiwa ilishapitishwa na Bunge, hivyo angependa kujua uhalali wa kujadiliwa tena bungeni.
Jijini Dar es Salaam, mjadala mzito uliendelea huku baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wakisema: “Marekebisho hayo ni kandimizi na yanalenga kuwanyima haki wanachama ambao wanaweza kupata matatizo mbalimbali wakiwa kazini”.
Kwa upande wake Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), jana ilitoa taarifa iliyoweka bayana kuwa, fao la kujitoa kazini limefutwa na kwamba jambo lolote linalohusu mafao ya aina hiyo linapaswa kusubiri kutolewa kwa miongozo husika.
Bungeni Dodoma
Jafo alitoa hoja akitaka Bunge liahirishe mjadala wa hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara jana ili kujadili kwa dharura sheria hiyo aliyosema kuwa imeanza kuzua mtafaruku na sintofahamu miongoni mwa jamii.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, Wafanyakazi wa sekta mbalimbali wamepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga kuwanyima haki ya fedha zao wanazokatwa kwa mujibu wa sheria. Naomba mwongozo wako, Bunge tujadili suala hilo kwa dharura," alisema.
Jafo alitoa hoja hiyo akitumia Kanuni ya 47 (1)(2) na (3) ambayo huruhusu jambo la dharura kujadiliwa.
Hoja ya Jafo iliungwa mkono na Mhagama ambaye alisema kuwa hilo ni jambo kujadiliwa lakini kwa wakati huo lilikuwa limekosa kitu kimoja ambacho ni mdai halisi ya wafanyakazi ambayo yanalalamikiwa.
“Hoja yako imeungwa mkono na ni kitu muhimu kujadiliwa, lakini imekosa kitu kimoja. Naomba unisaidie, ni mambo gani hasa ambayo wafanyakazi wanayohitaji yajadiliwe,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Tunatakiwa tuwasaidie wafanyakazi nchini, kwani hali imekuwa tete kwa wafanyakazi kuhusu suala hili na ili tuwatete ipasavyo ni vizuri tukajua madai halisi kuhusu jambo hilo.”
Alipomaliza kutoa mwongozo huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisimama na kukieleza kiti cha Spika kuwa jambo hilo ambalo Jafo amelizungumzia ni zito na hadi sasa kauli ya Serikali haijatoka hadi hivi sasa.
“Kwa busara yako mwenyekiti, naomba uitishe kamati ya uongozi ili tuweze kujadili jambo hili,” alisema Zitto.
Lissu kwa upande wake alisema kuwa, jambo aliloeleza Jafo ndicho kiini cha kelele zilizopo mtaani hivi sasa, hivyo anaiunga mkono.
Baada ya Lissu kumaliza, alisimama Mhagama na kueleza kuwa tayari alishatoa mwongozo kuhusu jambo hilo kwamba, ni muhimu Jafo akafanya mawasiliano na wafanyakazi ili kujua wanachohitaji kifanyike.
“Nilichokisema hapa nampa muda Jafo afanye ‘consultation’ na wafanyakazi hao ili atengeneze hizo hoja zake vizuri na kulileta suala hilo bungeni,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Ifikapo 7:15 mchana (jana) Kamati ya Uongozi itakaa ila Jafo awasiliane na wafanyakazi ili tuweze kujua matatizo yao...”
Lakini Lugora alitoa mawazo tofauti akisema: “Wanalalamikia kitu ambacho ni sheria iliyopitishwa hapa bungeni. Nataka kujua uhalali wa kujadiliwa suala ambalo tulilipitisha hapa bungeni”.
Mhagama alisimama na kumweleza Lugola kuwa Bunge linatakiwa kujadili maslahi ya wananchi na kwamba, sheria zilizopitishwa na Bunge siyo msahafu ambao hauwezi kubadilishwa.Baadaye jioni, Mhagama alisema Jafo ameelekezwa kwamba akaandae hoja yake kisha aiwasilishe kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda ili iwasilishwe bungeni kwa taratibu za kawaida.
Wanasheria
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Kaki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema wanapinga marekebisho ya Sheria hiyo kwa kuwa yanawanyima haki wanachama wa mifuko hiyo kupata stahili zao wanapozihitaji.
“Mimi kama mwanasheria naona kuwa, marekebisho haya yanalenga kuwakandamiza wanachama wa mifuko hiyo, kwani kila mtu ana mahitaji yake na majukumu yake sasa sio vema kumpangia mtu lini anapaswa kuchukua stahili yake,” alisema Sungusia na kuongeza:
“Tunafahamu kuwa, Serikali inadaiwa fedha nyingi na mifuko hii kutokanana mikopo mbalimbali; kwa mfano ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Machinga Complex pamoja na jengo la Bunge. Sasa wameamua kufanya marekebisho haya ili kufidia fedha zilizotumika na kusababisha ukandamizaji kwa wanachama.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Sengondo Mvungi alisema marekebisho ya sheria hiyo ni kandamizi wa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wanachama wanapaswa kuamka kupinga sharia hiyo.
Alisema wananchi wanachama wanapaswa kupinga sharia hiyo kwani haijawashirikisha na ina lengo la kuwakandamiza.
Dk, Mvungi alifafanua kuwa, sharia hiyo imepitwa na wakati kwani wafanyakazi hawakushirikishwa na kwamba sharia hizo zilitungwa wakati wa chama kimoja.
Kauli ya SSRA
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji Dar es Salaam jana imesema kuwa, maombi yote ya kujitoa katika mifuko ya hifadhi yamesimamishwa hadi baada ya miezi sita.
Taarifa hiyo ilisema usitishaji huo wa kujitoa hautayahusu maombi ya wale ambao wamejitoa kabla ya Julai 20 mwaka huu 2012 na uamuzi huo imebainisha taarifa hiyo kuwa imefuatia mkanganyiko uliojitokeza hivi karibuni na kuleta mgongano baina ya wadau.
Taarifa hiyo imekanusha madai kuwa sitisho la fao la kujitoa linatokana na shinikizo la Serikali, au madai mengine kuwa, mifuko imefilisika.“Mamlaka inawaomba wanachama na wadau wote kuwa na utulivyu wakati wa mchakato ukiendelea kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya wanachama” sehemu ya taarifa hiyo imesema.
Taarifa hiyo imebainisha na kufafanua kuwa marekebisho hayo ambayo yamezua migongano na wadau yamepitia hatua zote za kisheria na ushirikishwaji wa wadau muhimu katika sekta hiyo, ambao ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, chama cha waajiri pamoja na serikali.
“Mchakato umefanyika kwa kuzingatia tofauti ya ajira, mazingira ya kazi na hivi sasa mamlaka inaendelea kuandaa miongozo na kanuni za mafao kwa lengo la kuboresha maslahi ya wanachama na majadiliano yatahuisha wadau wote muhimu” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Via Mwananchi
Loading...
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment