Dira ya Dunia na Salim Kikeke
Katika hatua ya kihistoria, shirika la utangazaji la
kimataifa la BBC linazindua kipindi kipya cha televisheni kwa watazamaji
nchini Tanzania na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Hii ndiyo mara ya kwanza kwa shirika lolote la kimataifa kuanzisha matangazo ya televisheni katika lugha ya Kiswahili.Kipindi chenyewe kinajulikana kwa jina Dira ya Dunia kutokana na umaarufu wa kipindi cha redio kutoka Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Mhariri Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh anasema "hatua hii ni dhihirisho kwamba BBC inaitikia mabadiliko katika jinsi watu wanavyopokea habari kupitia safu mbalimbali. Dira ya Dunia katika televisheni kitatoa jukwa mwafaka la kuonyesha sura mpya inayoibuka barani Afrika. Ni bara ambalo linashuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kama ilivyo desturi ya BBC, tuzingatia maadili ya kuwa huru, kutangaza kwa njia halisi na isiyopendelea upande wowote."
Kwa takriban miaka 60 Idhaa ya Kiswahili ya BBC imejenga sifa na taadhima kupitia matangazo yake ya redio kama vile, Dira ya Dunia, Amka na BBC na Michezo. Idhaa ya Kiswahili ya BBC inajivunia kuwa na wasikilizaji takriban milioni 20.
Kipindi cha televisheni kitafungua ukrasa mpya katika uhusiano kati ya BBC na watazamaji wake.
Dira ya Dunia kitakuwa hewani kila siku, Jumatatu hadi Ijumaa, kupitia vituo washirika. Nchini Tanzania kitaonyeshwa kupitia Star TV. Nchini Kenya kitakuwa kwenye kituo cha QTV huku mipango zaidi ikifanywa kukisambaza katika kanda nzima ya Afrika mashariki na kati.
Mtangazaji kinara ni Salim Kikeke. "Naona fahari kubwa kushiriki katika hatua hii kubwa na ya kihistoria ya kuanzisha matangazo ya televisheni. Tumekuwa tukifanya kila tuwezalo kuhakikisha kila kitu kipo shwari kabla ya kuzindua kipindi hiki ambacho tunatumai kitawavutia wengi."
Kwa jumla wasikilizaji wengi wa matangazo ya BBC kupitia kwenye redio wapo barani Afrika. Zaidi ya watu milioni 80 wanasikiliza BBC kupitia lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kihausa, Kisomali, Kinyarwanda/Kirundi, Kiarabu na Kifaransa.
Utazamaji wa televisheni unaongezeka kwa kasi hasa katika sehemu za mijini. Kutokana na teknolojia mpya aina ya digital, idadi ya stesheni za TV itaongezeka hali ambayo itazua ushandani mkubwa katika kuwavutia watazamaji.
Mhariri wa kitengo cha Afrika, Solomon Mugera alisema "mkakati wa BBC ni kuhakikisha matangazo yetu yanapatikana kwenye redio, televisheni, tovuti, facebook na simu ya mkononi."
Kiasi kikubwa cha idadi ya watu katika nchi nyingi za Afrika wapo chini ya umri wa miaka 25. Wengi wao wana elimu ya hali ya juu, wanaishi mijini, wana tamaa ya kujiendeleza na kwa kutumia vyombo kama vile mtandao, simu ya mkononi na majukwa ya kijamii kama vile Facebook, wanaweza kujenga uhusiano wa kimataifa.
Chanzo:BBC Swahili
Post a Comment