HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA KWA MWAKA
WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza kwa umahiri mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013. Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Job Ndugai (Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wanaokusaidia kuongoza Bunge hili kwa kazi nzuri wanayoifanya.
3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nne. Chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee kudumisha hali hiyo ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa bei yoyote.
4. Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais mwezi Mei 2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye nafasi mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali. Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.
5. Mheshimiwa Spika, kwa njia ya kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Wizara yangu kwa kuwa ndiyo inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima kwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
6. Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao za kina ambazo zimetoa ufafanuzi na miongozo kwa masuala mbalimbali muhimu ya Taifa letu kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa ujumla wake, naomba kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri walizozifanya. Hotuba zao zote zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na jamii yanayohusu nchi yetu na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au nyingine.
7. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi mzima wa Wizara kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati kwa ushauri wao mzuri ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara walizozifanya kwenye nchi mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya kujionea wenyewe na kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali zinazotukabili kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri Serikali.
8. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John M. Haule, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika kuiongoza Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya Taifa letu.
9. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na hasa wana-Mtama wote. Napenda pia nimshukuru mke wangu Mrs. Membe na watoto wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha kwangu.
10. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane na Viongozi wote, Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea Zanzibar. Kwa wale wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza, namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu waweze kupona haraka.
Post a Comment