Zikiwa zimebakia siku takriban tatu kufikia siku muhimu ya kuanza kwa zoezi muhimu la sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu, bado malumbano yanaendelea kutanda sehemu mbalimbali juu ya tukio hili, hali ambayo binafsi imekuwa ikinipa mashaka sana juu ya ufanisi wa zoezi lenyewe.
Achia mbali madai yaliyoripotiwa jana toka kwa wenzetu Wahadzabe, ambao walidai hadi wapewe nyama ya kima sijui ngedere, gongo na bangi ndio wakubali kuhesabiwa, wapo waliokuwa wakigomea zoezi hilo kwasababu eti wana madai haya na yale dhidi ya serikali.
Kuanzia mikumbo ya kidini hadi mikumbo isiyojulikana ilikoanzia, vikundi vya watu wenye kuhanikiza watu kususia sensa, vimeendelea kuwa na sauti kwa kadiri ambavyo serikali nayo kwa upande wake imeendelea kutumia nguvu kubwa kuhamasisha umuhimu wa kila mmoja wetu kushiriki zoezi hili.
Hali hii inanikumbusha ujinga ambao tumekuwa tukiufanya wakati wa chaguzi mbalimbali na za ngazi mbalimbali pia. Imekuwa ni rahisi sana kwa Watanzania kutoshiriki katika chaguzi, pale inapotokea wanahitajika na wana fursa ya kufanya hivyo, na mwishowe wanapokuwa hawayaoni mabadiliko, wamekuwa mahiri sana katika kulalamikia viongozi ambao wao walishindwa kuwang'oa madarakani kupitia sanduku la kura. Hali hii mimi binafsi napenda niweke wazi kuwa naichukulia kama kiwango cha juu kabisa cha ujinga wetu (nimejaribu kupunguza makali maana kimsingi huu ni upumbavu)
Ndio, mwananchi ambaye unaona umechoshwa na chama fulani, lakini hutaki kwenda kupiga kura, unadhihirisha nini kama sio ujinga wa hali ya juu? Au unakwenda kupiga kura kisha unakuwa kiongozi wa kufanya fujo, badala ya kulinda kura yako na za mgombea wako kwa njia zilizo sahihi, unatarajia mabadiliko yepi?
Ni watanzania wangapi ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa huduma muhimu huko maeneo ya vijijini, ambako inaelezwa kuwa wamekuwa wakipelekewa mahitaji pungufu kulingana na idadi yao? Bahati mbaya sana ni kuwa, wote ambao wamekuwa wakilalamikia hili wamekuwa wakitoa takwimu zisizokuwa na uhakika juu ya wanaowasemea. Leo hii tunaletewa fursa ya kuhesabiwa ili ijulikane wako wangapi kwa usahihi kusudi hata watapoomba misaada iende kwa uwiano wa wanaoomba, mtu mwingine anasema gomeni kuhesabiwa. Hii akili au matope?
Leo hii unahamasisha watu kugoma kuhesabiwa. Kesho unaanza kuwashawishi waamini kuwa serikali yao haiwajali na ndio maana haiwapelekei misaada au huduma za muhimu zenye kuwahusu, huku ukijua wazi kuwa ni vigumu maana serikali hiyo haijui wanaohitaji ni wangapi. Na bado una ujasiri wa kusimama mbele ya kadamnasi na kujinadi kuwa wewe ni kiongozi, mkombozi au mwenye kuwatakia mema wananchi wenzako na taifa kwa ujumla? Haiwezekani, nchi hii haijawa Mirembe.
Umefikia wakati wa sisi wananchi kujua nguvu zetu na kuacha kutumiwa na watu wachache wenye nia ya kunufaika na kuishi maisha ya pepo wakiwa hapa duniani kupitia migongo yetu. Ukweli ni kwamba, unaposhiriki kupiga kura kwa ustaarabu na ukashiriki kulinda kura yako na zingine za mgombea wako kistaarabu, unatengeneza mazingira ya mabadiliko makubwa na yenye mantiki kuliko kufanya vinginevyo.
Na katika hili la sensa, ukweli utabakia kuwa, ni vigumu sana kuwa tutaweza kuwa na maendeleo katika mazingira ambayo hakuna anayejua kuwa tuko wangapi. Ni lazima kila Mtanzania kuhakikisha anashiriki sensa, ili hata siku akimnyooshea kidole kiongozi wake, anamnyooshea kwa haki na mamlaka yote kwani anaweza kumuuliza "si ulishajua kuwa nipo, kwanini hunihudumii?" tofauti na kususia maana unakuwa unajiondolea nguvu ya kuuliza stahiki zako. Ndio, utamuuliza nani ilhali hakuna anayekujua?
SHIME WATANZANIA WENZANGU, SENSA NI ZOEZI MUHIMU NA AMBALO HALIISHII TU KATIKA KUJUA TUKO WANGAPI, BALI PIA KUONYESHA NGUVU YETU NA NAMNA AMBAVYO TUNAWEZA KUFANYA MAAMUZI NA YAKAWA NA NGUVU GANI.
SHIRIKI SENSA ........ SHIRIKI KUONYESHA NGUVU YAKO NA SHIRIKI KUONYESHA NGUVU YA UMMA.
...................................................
Shukrani nyingi zimuendee Kaka Rama S.Msangi kwa waraka wake huu wa kuhamasisha ushiriki wetu katika zoezi la Sensa.
Chanzo:Rama S.Msangi kutoka katika ukurasa wake wa Facebook.
Post a Comment