Marehemu Waziri Mkuu wa Ethiopia,Mheshimiwa Meles Zenawi
......................................................
Nitaishi kuwa Meles
Mwaka
1975 Mwanafunzi wa mwaka wa Kwanza wa Chuo Kikuu cha Haile Selasie
(sasa Chuo Kikuu cha Addis Ababa) Legese Zenawi, akiwa na umri wa miaka
19 tu, aliacha masomo yake na kujiunga na kikundi cha Ukombozi cha watu
wa Tigray (Tigray Peoples Liberation Front). Legese alikuwa anasomea
shahada ya kwanza ya udaktari. Hakurudi tena Chuoni kusomea Udaktari na
hakuishi tena maisha ya ujana ambayo sisi wengine wote tumeishi na
kuyafurahia. Mwaka 2012 Legese akiwa na umri wa miaka 57 alifariki
dunia. Lakini aliaga dunia akiwa Meles Zenawi na sio Legese Zenawi, jina
alilopewa na wazazi wake huko Adwa kaskazini mwa Ethiopia.
Legese
alibadili jina lake kwa hiari yake kufuatia kuuwawa kwa rafiki yake na
mpiganaji mwenzake Meles mwaka 1975. Aliamua kumuishi mpiganaji mwenzake
kwa kuchukua jina lake na kuacha jina alilopewa na wazazi wake. Meles
alifanikiwa kupigana dhidi ya utawala wa kiimla wa Mengistu Haile Mariam
na kumtoa madarakani na kuingiza uongozi wa kimaendeleo chini ya chama
cha Kitaifa cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front
(EPRDF). Meles Zenawi aliahidi kumpigania rafiki yake Meles kwa faida ya
wananchi wanyonge wa Ethiopia na akatimiza ahadi hiyo kwa mafanikio
makubwa sana.
Mwanzoni Meles alipigana kwa lengo la kutaka uhuru wa eneo la Tigray kutoka Utawala wa Mengistu
na kundi la wanajeshi chini ya Derg. Meles na wenzake waliamini kabisa
kwamba utawala nchini mwao chini ya Mfalme Haile Selasie na hata chini
ya utawala wa Derg uligubikwa na ukabila na ueneo kwa faida ya kabila
kubwa nchini humo, Amhara.Aliamini kwamba makabila madogo kama kabila
lake la Tigray kutoka kaskazini mwa Ethiopia na hata makabila mengine
kama Wasomali walikuwa wanakandamizwa na kunyonywa ndani ya nchi yao.
Aliamini kwamba utajiri wa nchi ulikuwa unatumika kwa faida ya kundi
moja lililohodhimadaraka
ya nchi na kabila lao. Akiwa na umri wa miaka 19 tu na mwanafunzi wa
mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu aliamua kushika silaha na kupambana na
ugandamizaji huu.
Hata
hivyo Meles alibadili kabisa mtazamo wake alipogundua kuwa sio watu wa
Tigray tu waliokuwa wakinyonywa na kugandamizwa na utawala wa Mengistu
bali ilikuwa ni WaEthiopia wote bila kujali makabila yao. Mwaka 1985
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama cha TPLF akiwa na umri wa miaka 29
tu.Alihakikisha anaikomboa Tigray kama mkakati wa kuikomboa Ethiopia
yote. Alishirikiana na wakombozi wa Jimbo jirani la Eritrea ili kutetea
Uhuru wao na kuwapa uhuru wa kuamua kama wanataka kubakia sehemu ya
Ethiopia au kuwa Taifa huru ambapo waliamua kuwa Taifa huru.
Akiwa kijana wa chini ya umri wa miaka 30 aliunganisha makundi
mbalimbali yaliyokuwa na lengo la kuleta ukombozi na kujenga Ethiopia
mpya chini ya mwavuli ya chama cha EPRDF. EPRDF ilikuwa ni umoja wa
makabila yote nchini Ethiopia na walimchagua Meles kuongoza mapamabano
ya ukombozi.
Mwaka
1991 Meles Zenawi aliongoza EPRDF kuingia Addis Ababa na kushika Dola
huku Mengistu akikimbilia nchini Zimbabwe. Meles akiwa na umri wa miaka
36 tu alichaguliwa kuwa Rais wa muda wa Ethiopia na mkutano mkuu wa
kitaifa ambao kwa mara ya kwanza ulikutanisha makabila yote nchini
Ethiopia. Miaka mitatu baadaye kufuatia kura ya maoni Jimbo la Eritrea
likajitenga kutokaEthiopia na kuunda Taifa huru. Meles alitimiza ahadi
yake ya kuruhusu watu wa Eritrea kuamua kama wanataka kuwa Taifa
linalojitegemea au kuwa sehemu ya Shirikisho la Ethiopia. Hata mahusiano
kati ya Ethiopia na Eritrea yalipokuwa mabaya sana kiasi cha kupigana
vita kugombea kijiji cha Badme, Meles hakuchukua fursa hiyo kuirudisha
Eritrea kuwa mkoa ndani ya Ethiopia au hata kupata njia ya kwenda
baharini, bali aliheshimu matakwa ya waEritrea ya kujitawala.
Ukweli
ni kwamba vita kati ya Eritrea na Ethiopia ilikuwa ni vita isiyo na
maana yeyote ile na itabakia kuwa doa katika historia ya uongozi wa
Meles. Kitendo cha Meles kutoheshimu maamuzi ya Umoja wa Mataifa kwamba
Badme ni sehemu ya Eritrea pia ni doa ambalo wafuasi wa Meles
wataendelea kuwa nalo daima dumu na wakosoaji wa Meles wataendelea
kujengea hoja kuonyesha kuwa Kiongozi huyu hakuwa anaheshimu maamuzi ya
Taasisi za kimataifa. Hata hivyo doa hili haliwezi kufuta kabisa
mafanikio makubwa ambayo kamaradi Meles ameyapata katika Ethiopia
iliyokombolewa.
Meles
alipochaguliwa kuwa Kiongozi wa chama cha TPLF mwaka 1985 Ethiopia
ilikuwa kwenye ramani ya dunia kama Taifa lililoshindwa kulisha watu
wake. Dunia nzima kulikuwa na kampeni za kusaidia kuondoa njaa nchini
humo ambayo iliua zaidi ya watu milioni moja. Wakati mauaji ya kimbari
nchini Rwanda yaliua watu milioni moja kwa mapanga na mashoka, njaa
iliua watu kama hao hasa katika maeneo ya Tigray na Wollo kwa sababu ya
uzembe wa Serikali ya Mengistu. Mmoja
wa wajumbe wa Kamati Kuu wa chama cha Mengistu kilichokuwa kinatawala
wakati ule (Workers Party of Ethiopia) bwana Dawit Wolde
alimtahadharisha Mengistu kuhusu hali mbaya ya wananchi na kwamba
Serikali ilipaswa kuchukua hatua na kujibiwa ‘kulikuwa na mabaa ya njaa
miaka yote kabla sisi hatujatawala. Hiyo ni namna uasili (nature)
inafanya kazi yake. Kuingilia uasili ndio maana leo tumefikia watu
milioni 40’( Meredith in The State of Africa). Mengistu alilewa madaraka
kiasi cha kusahau kwamba siku moja kabla ya kumvua madaraka Mfalme
Haile Selasie walimwonyesha filamu (The hidden famine) ya namna yeye
alivyokuwa anastarehe na pombe aghali na kulisha nyama mbwa wake ilhali
wananchi wake walikuwa wanakufa kwa kukosa chakula katika baa la njaa la
mwaka 1984 katika Wilaya ya Wollo. Haile Selasie baada ya kuonyeshwa filamu hiyo alipoteza fahamu kwa mawazo na siku iliyofuata tarehe 12 Septemba 1974 akavuliwa ufalme na vijana watatu wanajeshi akiwemo Mengistu Haile Mariam.
Mengistu huyo huyo akiwa Rais wa Ethiopia akawa anajenga hoja kwamba
njaa ni tukio la asili ili ‘kubalance’ idadi ya watu nchini mwake! Haya
ndio mazingira ambayo Meles alichaguliwa kwayo kuongoza mapambano ya
ukombozi akiwa na umri wa miaka 29 tu.
‘naomba
vitabu vya Uchumi’ ndio ombi pekee Meles alilitoa kwa mwanahabari wa
kigeni aliyekwenda kumfanyia mahojiano mara baada ya kuchukua uongozi wa
Taifa lake. Mwanahabari huyo alimwuliza ni msaada gani anataka kutoka
kwa nchi za magharibi ili awaambie kupitia habari yake anayokwenda
kuandika. Meles alijua kwamba ana ajenda moja kubwa nayo ni kuondoa
njaa. Kuondoa Umasikini nchini mwake. Ajenda hii Meles aliifanyia kazi
kwa nguvu zake zote kipindi chote ambacho yeye alikuwa Rais na Baadaye
Waziri Mkuu wa Ethiopia.
Nakumbuka
tulikuwa tunatania mtu yeyote aliyekondeana kwa kusema ‘ana njaa kama
Ethiopia’ na hiyo ndio ilikuwa picha inayokuja machoni mwa watu wengi
duniani kuhusu Ethiopia. Meles
hakumaliza shida zote za Ethiopia, lakini alipambana nazo.
Alizipunguza. Amelitoa Taifa lake kutoka Taifa la kupigiwa mfano kwa
njaa na umasikini kwenda Taifa la kupigiwa mfano kwa maendeleo. Katika
kipindi cha miaka ishirini ya utawala wake hatujasikia baa kubwa la njaa
kama ilivyozoeleka kila muongo nchini humo. Mwana historia mmoja nchini
humo alionyesha kuwa kila muongo ulikumbwa na njaa kali nchini
Ethiopia, 1958, 1966, 1973 na 1984. Lakini toka Meles achukue uongozi wa
Taifa la Ethiopia hatukusikia njaa miaka ya tisini wala miaka ya 2000.
Ninaamini watakaomrithi Meles watahakikisha kuwa hakuna njaa tena ya
kiwango kile nchini Ethiopia kwa miongo mingine yote ijayo. Mafanikio
haya yanatokana na sera na maamuzi thabiti na ya dhati kutoka kwa
kiongozi ‘Sitaki njaa nchini kwangu’. Pia usimamizi thabiti wa maamuzi
sahihi yaliyotolewa.
Meles
aliamua kupambana na umasikini na kujenga Taifa lenye nguvu za
kiuchumi. Aliamua mapema kabisa kukataa ushauri wa IMF na Benki ya Dunia
wa kuufungua uchumi wa Ethiopia haraka sana (liberalisation). Yeye na
wenzake waliamua kuufungua uchumi kidogo kidogo kulingana na ratiba
waliyojiwekea wao wenyewe. Kutokana na hali hiyo sehemu kubwa ya uchumi
wa Ethiopia umeshikwa na wao wenyewe wananchi wa Ethiopia. Amejenga
miundombinu kuunganisha uchumi wa nchi na hivyo kufungua masoko ya ndani
licha ya yeye mwenyewe Meles kusisitiza sana mauzo ya nje. Kutokana
na maamuzi yake, hivi sasa Ethiopia itaanza kuuza nje Viatu vya ngozi
vilivyotengenezwa nchini humo vyenye thamani ya dola za kimarekani
bilioni nne. Hii ni sawa na mara mbili ya mauzo ya dhahabu yote ya
Tanzania kwenye soko la dunia. Ethiopia haina mafuta wala madini ya
kutosha kama Tanzania, lakini uchumi wake umekuwa ukikua kwa zaidi ya
asilimia kumi kwa miaka saba mfululizo. Ndio maana Meles ameweza
kupunguza umasikini kutoka asilimia 45 ya watu waliokuwa wakiishi kwenye
dimbwi la umasikini mwaka 1991 mpaka asilimia 29 mwaka 2011. Katika
kipindi kama hicho (1991 – 2011) Umasikini Tanzania ulishuka kutoka
asilimia 37 ya watu kuishi kwenye dimbwi la Umasikini mpaka asilimia 35
tu. Tanzania iliamua kufuata sera za kufungua uchumi wa nchi kwa haraka
kama walivyoshauri Taasisi za IMF na Benki ya Dunia.
Wakati Meles anaaga dunia ameacha
mradi mkubwa sana unatekelezwa nchini mwake. Mradi wa kuzalisha umeme
10,000 MW, Grand Millenium Project. Lengo lake ni kuzalisha umeme wa
kutosha kufanya mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi wa Ethiopia na
pia kuuza nchi jirani (Diplomasia ya Nishati). Benki ya Dunia ilikataa
kufadhili mradi huu, yeye akaamua kila muEthiopia kutoa fedha za
kufadhili mradi huu. Wananchi wa Ethiopia wote kila mmoja akajitolea
mshahara wake wote wa Mwezi mmoja na fedha hii kugeuzwa kuwa dhamana. Pia wananchi wa Ethiopia wanaoishi nje ya nchi nao waliruhusiwa kununua dhamana
hizi na kufadhili mradi huu kabambe. Mradi unatekelezwa kwa fedha za
WaEthiopia wenyewe. Nina imani kuwa mradi huu utaendelezwa na viongozi
wapya wa Ethiopia. Uzuri ni kwamba Meles alilea kizazi kipya cha
uongozi. Aliamua kuchukua vijana wa rika mbili chini yake na kuwapa
majukumu na kuwalea kiuongoni ili waweze kuwa tayari kurithi mikoba ya
viongozi wanaomaliza muda wao. Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia ana
umri wa miaka kumi chini ya Meles. Meles alijua umuhimu wa kuandaa
viongozi wa baadaye. Yeye hakuandaliwa. Mazingira ya ugandamizwaji,
unyanyasaji na umasikini yalimwita kuchukua majukumu ya kiuongozi akiwa
kijana mdogo sana wa miaka 19 alipoamua kujiunga na jeshi la ukombozi,
miaka 29 alipochaguliwa kuongoza jeshi la ukombozi na miaka 36
alipochaguliwa kuwa Rais na baadaye Waziri Mkuu wa Taifa lake.
Meles
ana makosa yake kama binaadamu. Amelaumiwa sana na mataifa ya magharibi
kuhusu rekodi yake ya masuala ya haki za binaadamu na kidemokrasia.
Lakini pia amelaumiwa na baadhi ya wanaharakati kwa kuuza ardhi ya
wananchi kwa makampuni ya kilimo ya mashariki ya kati na mashariki ya
mbali kama China. Hata hivyo sijawahi kusikia tuhuma zozote za Meles
kuhusu ufisadi na kujilimbikizia mali. Siku zote aliamini kuwa cheo ni
dhamana na hakutumia cheo chake kwa faida yake tofauti na viongozi
wengi sana wa kiafrika. Hapa nchini kwetu tunashuhudia watu wakitumia
nafasi zao za uongozi kulimbikiza mali.
Watu wana tamaa iliyokithiri ya mali. Ufisadi imekuwa ni hulka na sasa
ufisadi unahusisha nafasi yeyote ya uongozi. Hata tuhuma za ufisadi na
rushwa zimekuwa za kawaida mno mpaka unakuta wala rushwa wanatuhumu
viongozi wenye maadili ili mradi tu ionekane rushwa ni ya kila mtu wa
kila chama. Imekuwa kama Wezi kuungana kumkimbiza Polisi. Meles
hakutaka Ethiopia ifikie hali hii. Alipambana na rushwa yeye mwenyewe
kwa kujiwekea viwango vya kutokuwa na mawaa ya rushwa au matumizi mabaya
ya Ofisi ya Umma.
Meles
Zenawi ameacha mfumo wa Uchumi ambao haujapata fursa ya kujadiliwa vya
kutosha. Mfumo ambao umeiweka Ethiopia kuwa moja ya mataifa yatakayokuwa
na nguvu kubwa ya kiuchumi katika bara la Afrika ndani ya muongo mmoja
na nusu ujao. Meles alipambana na umasikini kwa dhati na kwa nguvu
inayostahili. Meles ametimiza wajibu wake.
Natamani kuwa Meles maana ameishi anachoamini kwa kupambana na ufisadi bila yeye kuwa fisadi ama kutumia vibaya Ofisi yake ya Umma.
Nitaishi kuwa Meles maana adui wetu nambari moja ni Umasikini,
umasikini wa vijijini. Meles alitangaza mwaka 1991 ‘our first enemy is
poverty and backwardness’ na akapambana na adui umasikini kadiri ya uwezo wake. Hakuna namna bora zaidi ya kumuenzi Meles zaidi ya kutenda yale mema aliyoyatenda na kurekebisha yale aliyoyakosea.
Nilipata
fursa ya kukutana na Meles mara moja. Nilikutana naye nchini Nigeria
katika mkutano kuhusu mashirikiano ya kiuchumi kati ya nchi za Ulaya na
nchi za Kiafrika mwaka 2009. Baada ya mkutano ule niliamua kumsoma Meles
na misingi anayosimamia. Ni kama nilimwona Mahathir Mohamad wa Malaysia
ndani ya Meles Zenawi kwa namna ya utendaji wao na uwezo wao wa kujenga hoja. Isipokuwa
tu Meles hakumaliza shahada yake ya udaktari na Mahathir alimaliza
yake. Ni dhahiri kwamba Meles Zenawi alikuwa ni kiongozi mwenye uwezo
mkubwa sana kiakili pengine kuliko viongozi wote wa kizazi cha pili
barani Afrika. Uwezo wake wa Akili uliwatisha viongozi wa mataifa ya Magharibi. Walimwogopa. Wenzake wa Afrika walimheshimu. Alikuwa sauti ya Afrika kutoka Addis Ababa, Makao makuu ya Afrika.Upumzike kwa amani Meles.
Chanzo:Zitto na Demokrasia.
Post a Comment