CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebeza mkakati wa kisiasa uliozinduliwa na Chama cha Wananchi (CUF). Chadema imekejeli mkakati huo kwa kusema kuwa CUF haina uwezo wa kuendesha Operesheni ya Dira ya Mabadiliko (V4C) nchi nzima.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya CUF kufanya matembezi ya hisani ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwezesha operesheni hiyo kuzunguka nchi mzima.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, alisema CHADEMA inasikitishwa na kauli za CUF za kuwahadaa Watanzania.
Mtemelwa alisema chama hicho hakina uwezo wa kuzunguka nchi nzima kunadi mkakati wao na kwamba kusema kinakwenda kubomoa ngome ya CHADEMA jijini Arusha ni siasa za kitoto.
“CHADEMA hatuendeshi kampeni zetu kwa kubomoana, tunapeleka sera zetu kwa wananchi pamoja na mipango ya kuwakomboa wananchi kutoka kwenye umasikini.
“Pia tunapeleka hoja zetu kwenye vyombo vya maamuzi, tunawaomba CUF kuwa makini wasiige, ili wasije wakaaibika mbele ya safari. Moto wa Chadema hawauwezi,” alisema.
Mtemelwa aliongeza: “CUF wanapaswa kujitathimini kwanza, wanakwenda Arusha kwa mtaji upi na wana hoja zipi za kuwaeleza wananchi.
“Ndani ya CUF hakuna mtu mbunifu wa kupanga na kufanikisha operesheni nchi nzima, hawana mikakati imara, hawana nyenzo wala mtaji.
“Tunawaomba wasiige kinachoanzishwa na CHADEMA na kujigamba kuwa wanaweza, tumeanzisha M4C nao wameanzisha V4C, itakufa kabla ya kufika mikoa 10,” alisema.
Mtemelwa alisema CHADEMA haitasita kushirikiana na taasisi na watu wenye nia nzuri ya kutafuta ukombozi wa kweli katika kujenga demokrasia.
Mbali na suala la kuzunguka nchi nzima, CUF pia kilisema hakipo tayari kupokea fedha zozote au msaada kutoka kwa matajiri, akiwamo mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Sabodo, kama ilivyo kwa CHADEMA.
Akizungumzia kauli hiyo, Mtemelwa alisema. “Sabodo ni raia wa Tanzania ingawa ana asili ya Kihindi, hivyo basi CHADEMA tutaendelea kupokea misaada kutoka kwa Mtanzania mwenzetu mwenye uzalendo, ila hatupo tayari kupokea fedha kutoka kwa mtu mchafu hata kama ni Mtanzania.
“Sabodo anatoa fedha kwa CHADEMA baada ya kuona mwenyewe kazi inayofanywa na chama ya kupambana na ufisadi, tunawatetea Watanzania katika masuala muhimu ya kijamii.
“Wanasema Sabodo anatoa fedha CCM na CHADEMA na kudai ana jambo la siri juu ya misaada hiyo, niwahakikishie CUF kwamba kama wanakerwa au hawajapata misaada hiyo wajue hawajafanya jambo la maana kwa jamii,” alisema.
Mtemelwa alisema CCM na CUF wamekuwa wakiiga mikakati inayoanzishwa na CHADEMA, lakini imekuwa ikiishia njiani na kushindwa kuleta mafanikio kama walivyokuwa wamekusudia.
Alisema baada ya vyama hivyo kushindwa kuhimili mikiki ya CHADEMA, wameamua kutumia vyombo vya dola, likiwamo Jeshi la Polisi kuzuia operesheni zao kwa lengo la kukidhoofisha.
Mtemelwa alisema Serikali ya CCM imekuwa na mikakati ya kukichafua CHADEMA na kueneza propaganda chafu kwamba ni chama cha fujo na vurugu.
Pamoja na mambo mengine, alitoa wito kwa CUF kuwa makini katika kueneza sera zao kwa wananchi na kuongeza kwamba hakuna siasa za kubomoana kwa vyama vya upinzani.
Alisema ikiwa CUF itaendesha operesheni zao za kukibomoa CHADEMA haitafanikiwa kufika mbali, badala yake chama hicho kitaaibika.
Juzi CUF ilifanya matembezi ya hisani ya kukichangia chama hicho na kufanikiwa kukusanya Sh milioni 129, huku Sh milioni 325 zikitajwa kama ahadi.
Matembezi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba, ambaye alichangia Sh 110,000.
Mtanzania
Post a Comment