Na: Mkina
NIMELIA. Nikalia na kulia tena na tena, kila napoona picha ama kusikia wengine wakimlilia mwandishi mwenzetu.
Nalia zaidi nikiona waandishi waliokuwa karibu zaidi na Daudi Mwangosi, yule mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel 10, aliyekuwa akiripoti kutoka Iringa.
Napata uchungu zaidi napolazimishwa kutazama damu, matumbo, moyo, maini na mapafu ya Mwangosi, binadamu aliyezaliwa, akalelewa, akasoma, akaanza kazi zake, akaoa, akapata watoto wane kupitia tumbo la mkewe, Itika.
Mimi sio daktari, sikuwa na lazima kuyaona maungo ya ndani ya Mwangosi, lakini nimelazimishwa na watu, binadamu kama yeye ambao, wamezaliwa na labda wamezaa ama kuzalisha. Hawa ni kama hayawani, wasiokuwa na chembe ya utu.
Hata daktari, mwenyewe hana ulazima wa kuona matumbo ya mtu, hadi kwa sababu maalum ya upasuaji, tena kwenye tumbo labda.
Wao, kwa tukio hili, wanaonekana wamesomea (sema wamejifunza) kuua. Tena siyo kuua mbwa, wala farasi ama kuku. Hata hivyo, katika kuua huko, hawaelezwi, kuua hovyo hovyo tu wanyama, au kuua yeyote; raia mwema.
Hawakufundishwa kuua waandishi, lakini sijui nini kimewakumba. Sasa wameamua kuanza kuua waandishi. Wameua mjumbe. Hawakuwa hata na huruma, wakakusanyika, wakampiga, tena kama gaidi. Walikuja kama tai, wakamvamia, wakagawana kumshambulia, wengi wakiwa na silaha za kuua.
Kumpiga ngwala, kumshambulia kwa vikalio vya bunduki, haikutosha. Mmoja wao akafyatua…paaaaa. Hiyo paaaa, ikawa chanzo cha kufumua tumbo la Mwangosi na uhai wake ukakoma papo hapo.
Hakika kifo cha mwangosi, kama ilivyo kwa binadamu awaye yote, kinaleta simanzi. Kinasikitisha na zaidi sana kinapotokea kwa kulazimishwa. Tena hiki chake, kimelazimishwa na walinzi wa amani, wenye jukumu la kulinda uhai wake, sasa wao wamekuwa chanzo cha kuuondoa kwa nguvu za ziada na haraka mno.
Nimewaona waandishi wakikusanyika, wakiliaani mauaji hayo. Kila mmoja, hata aliyekuwa adui yake amesimama kulaani mauaji ya Mwangosi. Nimefarijika zaidi kuona makundi mbalimbali ya umoja wa waandishi (hata kama bado, katika maeneo mengi haujaimarika) yakisimama na kulaani mauaji hayo ya kinyama.
Makundi na jumuia nyingi za nje ya Tanzania, zimeibuka na kumlilia Mwangosi. Habari zikasambaa kama moto wa nyika, dunia nzima ikajua na hakuna kilichofichama kwa sasa. Tumsubiri huyo atakayekuja na uongo wake. Tutamsuta, tutamjua siyo mwenzetu. Hakika dunia nzima itamcheka.
Matumaini yangu ni kwamba, pamoja na kumlilia Mwangosi, huenda kifo chake kikaanzisha chachu ya kuwepo kwa umoja zaidi kwa waandishi, kazi zao kuthaminiwa zaidi na kuheshimika.
Kifo hiki kinaweza kuwa njia ya kujitambua kwa waandishi huku kikijenga wigo utakaowapa nafasi ya kuthaminiana zaidi na kuvunja misambaratiko na minyukano isiyokuwa na tija kwao.
Waandishi tumeshuhudia wakinyanyaswa, tena na wenzao; baadhi ya wakubwa katika vyumba vya habari wakishindwa hata kupigania maslahi ya waandishi wanaowajazia habari kwenye vyombo vyao.
Tumeshuhudia waandishi wa mikoani (nje ya Dar es Salaam) wakifiwa na wazazi wao, watoto wao hata wake zao, na vyumba vyao vya habari vikishindwa kuwasaidia hata vipande vya sabuni kusaficha mikono ya wachimba ‘vyumba vya milele’.
Mbaya zaidi Tanzania imeshuhudia vyombo vya habari vikiwakana waandishi wao, hasa –correspondents, wale wa mikoani wanapopatwa na madhila, licha ya kuwafanyia kazi kwa muda mrefu, bila hata kuwaajiri rasmi.
Wanawakana, mara nyingi wanapopata matatizo, ingawa, nina uhakika ikiwa waandishi hao hao wanaowakana, kama wakishinda tuzo za kimataifa za tasnia ya habari, watasimama hata juu ya mapaa wakipaza sauti za kumpongeza na kujipiga kifua kwamba huyo ni mwandishi wao. Poor Bongo journalists.
Wakati wa kubadilika ni sasa. Wakati wa kujenga umoja wenye nguvu ni sasa na wakati wa kuthaminiana ni sasa. Hivi kama wananchi wasiokuwa waandishi wanaonekana kutulilia, iweje sisi tushindwe?
Tuvunje makundi ya ubaguzi ya wahariri kuthamini zaidi wahariri. Waandishi kuthamini zaidi waandishi wenzao, huku pia wakilazimishwa kuwathamini zaidi wahariri wao.
Ulale salama Mwangosi.
Chanzo: http://blog.simonmkina.com
Post a Comment