SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), limesema hakuna kanuni inayozuia timu ya Ligi Kuu kuwapanga nyota watano wa kimataifa katika mechi moja, kama benchi la ufundi litaamua hivyo kulingana na mazingira ya timu na mechi husika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na hofu iliyopo kwa baadhi ya wapenzi na mashabiki wa soka nchini juu ya kitendo cha Yanga kuwachezesha wachezaji watano kwenye mechi ya Jumamosi.
Katika mechi hiyo namba 15 iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Yanga ilipata ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo Septemba 15, wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.
Nyota wa kigeni waliopangwa kwenye kikosi hicho cha ‘maangamizi,’ na nchi zao kwenye mabano ni Yaw Berko (Ghana), Mbuyu Twite (Rwanda), Hamis Kiiza (Uganda), Haruna Niyonzima (Rwanda) na Didier Kavumbagu (Burundi).
Wambura alisema jana kuwa sheria na kanuni za Ligi Kuu zinaruhusu klabu moja kusajili nyota watano wa kigeni na kanuni iko kimya juu ya wangapi watumiwe kwa mechi moja, hivyo kitendo cha Yanga kuwachezesha wote watano, hakuna kanuni iliyookiukwa.
Ufafanuzi huo wa TFF, ni habari njema kwa wapenzi na mashabiki wa timu ya Yanga, ambao kwa nyakati tofauti juzi na jana, walikuwa wakipiga simu kujua kama kuchezeshwa kwa nyota hao katika mechi moja, kusingeigharimu timu yao kwa kupokwa pointi.
“Yanga hawawezi kunyang’anywa pointi zao kwa kuwachezesha wachezaji watano wa kigeni katika mechi moja, hakuna utata wowote. Wachezaji wa kigeni wote wanasajiliwa ili kuisaidia timu, hivyo kanuni ziko kimya juu ya idadi ya kuchezeshwa,” alisema Wambura.
Wambura alirejea tena kuwa kuanzia msimu ujao klabu itaruhusiwa kusajili nyota watatu tu wa kigeni badala ya watano wa sasa kwa lengo la kulinda vipaji vya nyota wazalendo.
Chanzo:Tanzania
Post a Comment