Nawaomba wananchi na wadau wa sekta binafsi mnaotumia Barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa muwasiliane na Diwani wa Kimara Pascal Manota 0784954657 awape utaratibu wa kuchangia kuwezesha kukodi grader kusawazisha na malori kuweka vifusi kwenye maeneo korofi kwa dharura wakati tukisubiri matengenezo ya haraka yanayopaswa kufanywa na Serikali kwa kodi zetu; mimi tayari nimeshampatia mchango wangu wa shilingi laki mbili kati ya milioni moja zinazohitajika, wewe je?
Izingatiwe kwamba tayari Wizara ya Ujenzi ilishakubali kuihudumia barabara hii na wiki chache zilizopita niliandika barua kwa meneja wa TANROADS Mkoa wa Dare es Salaam kutaka hatua zake kwa hali mbovu ya barabara hiyo pamoja na kuwa kero wa wananchi inamwaibisha Rais Kikwete mbele ya wakazi husika kwa kuwa alitembelea mwaka 2010 na kuahidi itajengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, mwaka 2011 ilifanyiwa matengenezo ya kawaida lakini kwa sasa imeharibika tena kufuatia mvua zilizonyesha, hali mbovu ya barabara hiyo inaathiri pia hatua za kupunguza msongamano kwenye barabara ya Morogoro wakati huu ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) unapoendelea kwa kuwa barabara hiyo hutumika kama njia mbadala kutoka Manispaa ya Kinondoni mpaka Manispaa ya Ilala.
Leo na kesho nitakuwa kwenye mfululizo wa mikutano ya baraza la madiwani wa jiji hivyo wakati nikiendelea kufuatilia majibu ya hatua za haraka za serikali kuwezesha matengenezo makubwa, naomba utaratibu kwa kushirikiana na diwani na watendaji kwa ajili ya kuunganisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine ili kufanya matengenezo madogo kupunguza kero uendelee.
John Mnyika (Mb)
10/09/2012
Post a Comment