Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WALEMAVU WA MACHO WAFAIDI FURSA ZA ELIMU CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA


Na Fredy Azzah
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ndio taasisi pekee ya elimu ya juu inayoongoza kudahili wanafunzi wengi wenye ulemavu nchini.Hii ni kwa sababu  mojawapo ya malengo makubwa ya Serikali kuanzisha chuo hicho, ni kusaidia  watu wa kundi hilo waweze kupata elimu ya juu.


Hata hivyo, idadi ya walemavu inatajwa kuwa ndogo katika chuo hicho ambacho hivi sasa kinadahili zaidi ya wanafunzi 30,000 kwa mwaka.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tolly Mbwete, anasema Serikali ndiyo yenye jukumu kubwa la kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa za elimu ya juu,  hasa kwa kuwatengenezea mazingira bora ya kujifunza tangu wakiwa katika madaraja ya chini ya elimu.

“Hakuna njia itakayotuwezesha kupata wanafunzi wa chuo kikuu kama siyo wale waliopikwa vizuri kuanzia shule za msingi. Kwa hiyo, licha ya nia nzuri ya Serikali kuja na mpango wa elimu jumuishi, inatakiwa wajitazame upya,” anasema na kuongeza:
“Wale watoto wana mahitaji mengi ambayo wanatakiwa wapate wenyewe kuanzia darasani na nje ya darasa.”

Anasema kuwa pindi watoto hao wenye ulemavu wakipata fursa nzuri ya elimu ya msingi na sekondari, itasaidia kuwapo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.



Hata hivyo,  Profesa Mbwete anasema kuwa hayo yote yanahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha ambao bado anasema haujapewa kipaumbele nchini,
“Serikali ilivyoanzisha  chuo hiki,  lengo lake kubwa ilikuwa ni kusaidia watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali wapate elimu, lakini hakuna bajeti maalumu ambayo inatoka wizarani kuja hapa kwa ajili ya elimu kwa walemavu,” anasema.

Anaongeza: “Elimu kwa walemavu inahitaji uwekezaji wa hali ya juu sana, hii ni kutokana na mahitaji yao. Kwa hiyo,  ingetakiwa kuwapo  na bajeti maalumu kwenye vyuo na taasisi nyingine kwa ajili ya walemavu.”
Kutokana na hali hiyo, Profesa Mbwete anasema kuwa utashi wa kisiasa unahitajika kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kundi hili la wanajamii haliachwi nyuma kielimu.

Walemavu wa macho
Chuo Kikuu Huria, ni chuo pekee Tanzania chenye idadi kubwa ya wanafunzi wasioona, hata hivyo baadhi ya wahadhiri chuoni hapo, wanasema wanakabiliana na changamoto kubwa ya kuandaa masomo kwa ajili ya wanafunzi hao, kwa kuwa hawajahi kupewa mafunzo yoyote kuhusu namna ya kuwasaidia kielimu.


“Kwa sasa tunaandaa tu kama vile kila anayekuja kusoma anaweza kusoma, halafu watu wa kitengo cha wanafunzi wasioona ndio wanaochukua na kuyatafsiri ili wale wanafunzi wasioona waweze kufuatilia masomo yao,” anasema Janeth Jonas ambaye ni mhadhiri msaidizi katika kitivo cha elimu.

Kwa upande wake,  Dk Sydney Mkuchu, anasema kuwa  katika mazingira ambayo mwalimu anaandaa somo, na kisha linapitia katika mikono ya zaidi ya watu watatu ili hatimaye limfikie mwanafunzi, ni dhahiri ujumbe wa mwanzo wa mwalimu unaweza kupotea.

Kwa mtazamo wake kuhusu wanafunzi wasioona, anasema ingekuwa bora kama wanaotafsiri masomo kutoka katika maandishi kwenda katika mfumo wa sauti, wangekuwa nao wamebobea katika masomo husika.
Pamoja na changamoto hizo, mtaalamu wa teknolojia wa chuo hicho, Emanuel Mhehwa, anasema tiba kubwa ya kuwasaidia wanafunzi hao ni kutumia zana za kiteknolojoa kama vile matumizi ya mtandao wa kompyuta.

Anasema kwamba maabara ya kompyuta ya wanafunzi wasioona iliyofunguliwa chuoni hapo,  itakuwa chachu kubwa ya  kuwapatia wanafunzi walemavu utaalamu wa kutumia zana hiyo muhimu katika kujifunza.
“Zamani mtu mwenye ulemavu kama  wa macho, alikuwa anasoma kozi ya miaka mitatu kwa miaka saba mpaka tisa, lakini sasa hivi ana uwezo wa kuisoma kwa miaka mitatu tu kama mtu mwingine. Hii ni kwa sababu upatikanaji wa masomo kwenye mtandao ni umerahisishwa,” anasema Mhehwa ambaye naye ni mlemavu wa macho.

Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa macho chuoni hapo, Cosmas Muyanyi, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa sasa kina wanafunzi 70 wasioona waliopo katika matawi mbalimbali ya chuo hicho nchi nzima.
“Jukumu langu kubwa ni kuhakikisha kuwa hawa wanafunzi wote wanapata kozi. Huwa tunawatumia kanda za sauti wanazisikiliza,” anasema.

Out chajipanga
Kuonyesha dhamira ya kuwaendeleza watu wenye ulemavu kielimu, wiki iliyopita chuo hicho kilizindua maabara maalumu ya kutoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu wa macho na masikio kwa njia rahisi.

Maabara hiyo yenye kompyuta 30, zilizowekewa mfumo maalumu kwa ajili ya watu wa kundi hilo,  ilizunduliwa katika makao makuu ya chuo hicho yaliyopo mkoani Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Watu Wenye Mahitaji  Maalum ya Teknolojia (Astu),  Cosmas Kitengo, anasema kompyuta hizo zimewekewa spika zenye sauti ya juu kwa ajili ya wanafunzi wasiosiki,  na kwa upande wa wasioona,  kitengo kipo katika mikakati ya  kuwawekea alama kwenye kompyuta, ili waweze  kutambua kwa urahisi herufi na namba.

Anasema kupitia mfumo huo, walemavu wataweza kupata mafunzo ya ngazi ya vyeti, stashahada na shahada zinazotambuliwa na Baraza la Usimamizi wa Mafunzo ya Ufundi (Nacte).
Chanzo:Mwananchi
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top