Rais wa Malawi, Joyce Banda
Mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi umeanza kutumiwa vibaya na baadhi ya watu, kufuatia baadhi yao kuanza kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kupitia simu za mkononi na kuwajengea hofu wananchi hususani wa wilaya za mkoa wa Mbeya.
Ujumbe huo ulianza kusambazwa na watu wasiojulikana tangu wiki iliyopita, unawatahadharisha wananchi kuwa makini kwa madai kuwa kuna mabomu yamerushwa toka nchi jirani ya Malawi na kuwataka wachukue hatua kwa kuhakikisha hawaokoti kitu chochote watakachokiona kinachofanana na chupa.
“Habari zilizotufikia hivi punde, Mtanzania yeyote kaa makini usiokote kitu chochote ambacho una mashaka nacho kuna mabomu yamerushwa kutoka nchi jirani ya Malawi zaidi ya 30 yenye uzito usiopungua tani 100, hivyo basi uonapo kitu kipo kama chupa ya chai kina rangi ya fedha usikiguse, piga namba 0756000042, imetolewa na JWTZ/LSL5CAMRM,“ umeeleza ujumbe huo.
Ujumbe huo unawataka wananchi kuutuma kwa watu wengine zaidi.
Kufuatia ujumbe huo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekanusha taarifa hizo na kusema kuwa ni za uzushi na hazihusiani na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi Upanga, jijini Dar es Salaam jana na kusambazwa kwa vyombo vya habari, taarifa hizo ni za uzushi kwa sababu uzito wa mabomu ulioelezwa ni mkubwa sana kiasi ambacho ni vigumu kubebwa kwa ndege au kurushwa na mzinga wowote.
“Tunawaomba wananchi wote wazione taarifa hizi kuwa ni za uzushi na wala hazikutolewa na JWTZ. Hatari ya mabomu haiwezi kutolewa na Jeshi kwa njia ya simu, zitatolewa kupitia vyombo vya habari vya radio, runinga na magazeti,” imeeleza taarifa hiyo ya JWTZ.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa kama kuna tahadhari yeyote, serikali itatoa taarifa hiyo kwa wananchi kwa kutumia mfumo ulio rasmi zaidi na si kupitia SMS za simu za mikononi.
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano imeeleza kuwa: “Zebaki (Mercury) ndiyo madini mazito kuliko yoyote duniani na kuwa umbo la chupa ya chai ya madini hayawezi kufikia hata kilo 15 (lita ya zebaki moja ni sawa na kilo 13.6) hivyo hata kama chupa zote 30 zikipimwa hazitazidi kilo 450.”
Wakati hayo yakitokea, Serikali ya Malawi imekubali kurudi katika meza ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati yake na Tanzania baada ya hivi karibuni Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda, kutangaza kujiondoa katika mazungumzo hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, alisema viongozi wa Malawi watakuja nchini kuanzia Oktoba 27 mwaka huu kuhudhuria vikao vya mazungumzo kuhusu mgogoro huo wa mpaka.
Mwezi uliopita, Rais wa Malawi, Rais Banda muda mfupi baada ya kuwasili nchini humo akitokea Marekani kwenye mazungumzo na Katibu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin-moon, alitangaza kujitoa katika meza ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo wa mpaka katika Ziwa Nyasa na kutangaza kupeleka suala hilo katika vyombo vya sheria vya kimataifa ikiwamo Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ).
Kwa mujibu wa Banda, serikali yake iliamua kutoa tamko hilo kufuatia madai ya kwamba Tanzania imevuruga makubaliano yaliyofikiwa nchini humo ya kuendelea katika meza ya mazungumzo kwa upande wa Tanzania baada ya kuchora ramani mpya inayoonyesha mpaka umepita kati kati ya Ziwa Nyasa.
Kabla Malawi kujitoa katika mazungumzo hayo, mazungumzo ya awali yaliyowahusisha mawaziri na wataalamu yalifanyika jijini Dar es Salaam na kufuatiwa na mengine yaliyofanyika katika mji wa Mzuzu, nchini Malawi.
Muda mfupi baada ya mazungumzo ya Mzuzu, Malawi ilitaka ipewe muda zaidi na baadaye kujitoa.
Malawi inasema kuwa inamiliki asilimia 100 ya Ziwa Nyasa wakati Tanzania inasisiziza kuwa kila nchi inamiliki asilimia 50.
Hivi karibuni uhusiano kati ya nchi hizo ulizorota baada ya madai kuwa Tanzania ilikuwa tayari kutumia nguvu za kijeshi.
Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete alipokutana na Rais Banda mjini Mapito, Msumbiji katika mkutano wa wakuu wa nchi na serikali za wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) Agosti 17, mwaka huu, alimhakikishia Rais Banda kuwa Tanzania haina nia ya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Malawi.
CHANZO: NIPASHEa
Post a Comment