Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MUUNGANO WAMTOKEA PUANI WAZIRI SERIKALINI


  *Aondolewa rasmi madarakani

  *Alikaidi, akakejeli sasa yamkuta
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed, Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed, Shein, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kumuondoa aliyekuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum, Mansoor Yussuf Himid.


Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Rais  Dk Shein, amemteua Shawana Bukheti Hassan, kuchukua nafasi ya Himid.

Taarifa hiyo haikueleza sababu za kuondolewa kwa Himid katika nafasi hiyo, ingawa wachambuzi wameitafsiri hatua hiyo na msimamo aliouonyesha karibuni wa kutoa maoni ya kuukosoa muundo na mfumo wa Muungano.

Akichangia maoni ya Katiba mpya hivi karibuni, Mansour alisema kuwa Muungano wa sasa unakabiliwa na kasoro nyingi na kupendekeza uanzishwe muungano wa mkataba unaopigiwa debe na Chama cha Wananchi (Cuf).

Mansour alisema pamoja na kwamba msimamo wake ni kuendelea kuwepo kwa muungano wa mfumo wa serikali mbili, lakini Muungano huo unapaswa uwe wa mkataba ili Zanzibar ipate maendeleo ya kiuchumi.

Mansour ambaye ni mtoto wa mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Marehemu Yusuf Himid, alisema wazi wazi kuwa halitakuwa jambo baya chini ya Muungano wa mkataba ikiwa kila upande yaani Tanzania Bara na Zanzibar kuwa na kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).

Alisema haogopi kutokana na maoni aliyoyatoa kwa kuwa ni haki yake na kwamba hata akiadhibiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na maoni hayo, atakuwa tayari kukabiliana na adhabu yoyote.

Baada ya kauli yake, wanasiasa mbalimbali wa Zanzibar walimtuhumu  (Mansour) na wanachama wengine wa CCM ambao walitoa maoni yanayokinzana na sera ya chama hicho ya Muungano wa serikali mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema kuwa mwanachama yeyote wa CCM anayepinga mfumo wa serikali mbili ajiondoe ndani ya chama hicho, vinginevyo atanyang’anywa kadi.

Wakati wa mkutano wa Tisa wa Bunge, Wabunge wa CCM Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mohamed Saif Khatibu, waliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kukitaka chama hicho kuwashughulikia wale wote watakaotoa maoni tofauti na msimamo wa CCM kuhusu Muungano. 

UTEUZI WA SHEIN

Pia, Rais  Shein amewateua Mtumwa Kheir Mbarak (CUF) kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili na Mohammed Said Mohamed (CCM) kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Dk. Shein amemteua Dk. Juma Malik Akili  kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano akichukua nafasi ya Dk. Vuai Idd Lila ambaye atapangiwa kazi nyingine na Ali Khalil Mirza ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi.

Kabla ya uteuzi huo, Mirza alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mwalimu Ali Mwalimu atapangiwa kazi nyingine. 

Katika mabadiliko hayo Dk. Shein pia amemteua Tahir Abdulla kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na kumtema aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Msanif Haji Mussa, ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Mustafa Aboud Jumbe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikuwa Tahir Abdulla ambaye amehamishiwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano.

Jumbe aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kabla ya kutokea ajali ya boti ya MV Spice Islander na kuwajibishwa ikiwemo kuondolewa katika nafasi hiyo.

Rais Shein amemteua Dk. Julius Nalim Maziku kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kapteni Juma Abdulla Juma ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar hivi karibuni.

Juma Ameir Hafidh ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo). Amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdi Khamis Faki aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar.

FEROUZ AKUMBUKWA

Vile vile, aliyepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ali Khalil Mirza aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati.

Kadhalika,  Rais Dk. Shein amemteua Mussa Haji Ali kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top