Ndugu zangu,
Wahenga walinena; Kuishi kwingi ni kuona mengi, na kusikia pia. Jana nilipokea meseji ya simu iliyokuwa ikisambazwa kwa watu mbali mbali, inasema hivi :
" Hatari, angalia watoto wa vigogo waliopita kwenye UVCCM ngazi ya Taifa. Kisha yakaorodheshwa majina 14 ya wenye kuitwa ' Watoto wa Vigogo'. Ikafuata rai:
" Nchi hii imekwisha, inatia hasira, wacha watoto wa masikini tupambane kupitia mlango mwingine' CHADEMA'ili kutetea masikini wenzetu, wazazi na wadogo zetu! Vita hii inaanza Sasa!" Unasema ujumbe huo.
Hakika, hatari hasa ya ujumbe huo iko kwenye ujumbe wenyewe na wala si hao watoto wa vigogo 14 miongoni mwa Watanzania milioni 40. Kwamba ni ujumbe wenye kuchochea chuki na ubaguzi. Ni dhambi inayoendelea kututafuna. Tukiziacha mbegu hizi za chuki ziendelee kupandwa na kusambaa, basi, sote tumo kwenye hatari ya kuangamia.
Kuna wakati Mwalimu Nyerere alipata kutamka, kuwa katika wakati ambao alifurahi sana ni pale aliposikia kuwa mwanawe, Makongoro Nyerere, amechaguliwa na wananchi wa Arusha Mjini kuwa Mbunge wao kupitia tiketi ya chama cha upinzani cha NCCR- Mageuzi. Makongoro Nyerere ni mtoto wa kuzaliwa wa Mwalimu, lakini, ilifika mahali aliamua kuchagua njia nyingine. Na wananchi wa Arusha hawakumchagua Makongoro kwa vile ni mtoto wa Julius Nyerere, bali walilidhishwa na uwezo wake.
Ndio, Mwalimu hakumkataza mwanawe Makongoro kujiunga na NCCR- Mageuzi, na wala hakumpigia debe kwa Wana- Arusha wamchague. Bila shaka, Mwalimu alitambua, kuwa Makongoro alikuwa mtu mzima na aliamua kuchagua njia anayoitaka. Hakuna dhambi ya mtoto wa kigogo anapokuwa mtu mzima kujihusisha na siasa. Hilo ni jambo la utashi wa mtu. Dhambi inakuja kama kiongozi atafanya uteuzi wa upendeleo kwa mtoto wake au mwanaukoo wake.
Lakini, kwenye suala la siasa za vyama vyenye kuendeshwa kwa Katiba na Kanuni, mwanachama na hata Mwenyekiti wa chama anajitafakari na kujipima kwanza kabla hajachukua fomu kuomba nafasi ya uongozi ya kuchaguliwa. Anayepitishwa kugombea nafasi ya uongozi kwenye chama cha siasa huwa ana sifa za kugombea, vinginevyo, hicho ni chama cha walevi wa chibuku.
Hivyo basi, kwa mwanachama mwenye sifa, kugombea uongozi ndani ya chama ni haki yake, anaweza kufanya hivyo hata kama mama au baba yake hataki, mume au mke hataki, maana, jukumu la kumpitisha na hata kumchagua litabaki kwa wajumbe wa chama chake. Hivyo basi, kama mwanachama ana sifa ya kugombea, basi, hana dhambi anayofanya akifanya uamuzi wa kujaza fomu na kusimama mbele ya wajumbe kuomba kura.
Na hakuna ajabu kwenye familia ya baba au mama mwanasiasa kukawepo na wanafamilia wenye kupenda kushiriki siasa. Na hutokea, na mifano ipo, kwa wanafamilia au wanaukoo kuwa wanachama wa vyama tofauti vya siasa, na wakabaki kuwa wanaukoo. Ni siasa tu. Hoja ni pale unapopatikana ushahidi wa wapiga kura kushinikizwa kwa rushwa au maneno kumchagua mwanachama mgombea kwa vile tu mama au baba ana wadhifa mkubwa kwenye chama.
Na katika nchi hii tuna mifano mingi ya watoto au wanaukoo wa viongozi walioshiriki siasa. Na kuna walioanguka kwenye chaguzi pamoja na kuwa na majina makubwa ya baba au mama zao. Joseph Nyerere alikuwa mdogo wake na Mwalimu. Alipata kushiriki siasa za TANU tangu enzi za TANU Youth League. Na kuna chaguzi za TANU na CCM kura za Joseph Nyerere hazikutosha, hata kama kaka yake alikuwa ni Rais wa nchi.
Nimesimuliwa pia, kuwa kuna wakati, ndugu yake na Mwalimu Nyerere, Chifu Wanzagi, naye aliangushwa katika uchaguzi wa TANU kule Musoma. Ilibidi Mwalimu aende kwao akamnusuru Chifu Wanzagi, arudi tena kwenye uongozi wa TANU, ni kwa vile tu, Mwalimu alitambua, kuwa Wana-TANU wale wa Musoma hawakumwangusha tu Chifu Wanzagi kwenye TANU, bali, kulikuwa na tatizo kubwa kwa ' Chifu Kuangushwa!'
Ukiacha siasa, kwa Wazanaki, Chifu Wanzagi Nyerere alikuwa Chifu Wanzagi haswa, alikuwa ni Chifu wa Julius Nyerere pia! Na kama Rais wa nchi, unafanyaje unaposikia Chifu wako wa kikabila ameangushwa kwenye uchaguzi wa Chama, tena na wanachama ambao wewe ni Mwenyekiti wao?
Naam, hamasa ya kisiasa imeongezeka kwenye nchi yetu. Huko twendako tuzazidi kusikia majina zaidi ya wanafamilia na wanaukoo wakishiriki siasa, ama katika chama kimoja , au vyama tofauti. Badala ya kuishia kulalamika, kupambana kuliko bora ni kwa wenye uwezo na utashi, kushiriki kwenye siasa bila kuogopa majina ya watu.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa, Iringa,
0788 111 765
Chanzo:Mjengwa Blog
Post a Comment