Mwandishi Wetu
WAKATI uongozi wa Yanga ukijinasibu kuwasafirisha wachezaji wake kwa ndege ya kukodi, imebainika kuwa huo ni uongo kwani wachezaji hao na viongozi wawili wa timu hiyo walipanda ndege ya abiria wa kawaida.
Yanga waliondoka juzi Jumamosi na ndege ya Shirika la Precision kwenda Mwanza kabla ya kuunganisha na charter kwenda Kagera na kufikia kwenye Hoteli ya Smart.
Wachezaji wa Yanga wakiwa na kocha msaidizi wa timu hiyo waliangua kicheko pale walipoulizwa kulikoni kujazana
kwenye ndege ya abiria wa kawaida badala ya ndege yao ya kukodi.
Wachezaji walisema viongozi wao wamekuwa watu wa maneno mengi huku wakifanya mambo tofauti.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga alisema, "Ndiyo wamewadanganyeni wanatukodia ndege? Achaneni nao hao wana maneno mengi utekelezaji sifuri."
Mwingine alisema,"Yaani hawa viongozi wangekuwa wanatekeleza yote wanayosema tungekuwa mbali sana, lakini ahadi nyingi utekelezaji hakuna tumeshawazoea uongo wao.”
Mwingine alisema, "Haaa sisi tunawaita wazee wa 'sound', wakakodi ndege wao? Hembu usinichekeshe huyo kiongozi aliyesema anakodi ndege ni nani jamani, dah viongozi wetu kwa maneno! Duh hiyo kali, kwa hiyo wakasemaje wanatukodia
ndege?" Alisema huku akiangua kicheko.
Kocha msaidizi wa timu hiyo Felix Minziro aliposikia kauli hiyo ya kukodi ndege aliangua kicheko huku akishikilia mbavu
zake akiwa amesimama na Kocha mkuu wa Yanga, Enerst Brandts ambaye hakuelewa kilichokuwa kikiendelea zaidi ya kutabasamu muda wote.
Yanga iliwasili Jumamosi saa tatu asubuhi kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza na kuunganisha kwa ndege ndogo kuelekea Kagera ikiwa na kikosi cha wachezaji 18 huku wachezaji waliosalia wakitarajiwa kuwasili leo na basi walilopewa na mdhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.
Kikosi cha Yanga kilichowasili juzi kwa ndege ni Kipa Yaw Berko, Ally Mustapha, Haruna Niyonzima, Omega Seme, Athuman Idd 'Chuji', Shamte Ally, Stephano Mwasika, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Nadir Haroub 'Canavaro'' na Jerry Tegete.
Pia wapo wachezaji wao wapya ambao ni Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu, Ladslaus Mbogo, Said Bahanuzi, Juma Abdul, Frank Dumayo, David Luhende na Nizar Khalfan.
Huku viongozi waliosafiri na timu ukiachia benchi la ufundi ni wajumbe wa kamati ya utendaji, Tito Osoro na Musa Katabalo.
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment