Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akikagua gwaride rasmi katika Viwanja vya Jumba la Rideau Hall jijini Ottawa, Canada.
Rais Kikwete akitambulisha ujumbe wa Tanzania, uliomjumuisha Mhe. Bernard K. Membe (MB) (pichani akisalimiana na Gavana Jenerali Johnson), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Viwanja vya Jumba la Rideau Hall jijini Ottawa. Jumba hilo pia ni makazi na ofisi rasmi ya Gavana Jenerali wa Canada tangu mwaka 1867, ambalo hutumika kuwatunukia wananchi wa Canada waliofanya vyema. Aidha, Jumba hilo ni sehemu ya mapokezi ya wageni mashuhuri wa nchi za nje na pia ndipo mahala Gavana Jeneralia anapofanya shughuli zote kitaifa akiwa kama Mwakilishi wa Malkia wa Uingereza.
Rais Kikwete akisalimiana na Watanzania waliojitokeza kumpokea.
Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika mazungumzo na Mhe. David Johnson, Gavana Jenerali wa Canada. Mhe. Rais Kikwete alikuwa nchini Canada kwenye ziara rasmi ya siku mbili, mjini Ottawa.
Rais Kikwete na ujumbe wake akiwemo Mhe. Bernard K. Membe (MB) (kulia kwa Rais), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akiwa katika mazungumzo na Gavana Jenearli Johnson wa Canada.
Rais Kikwete awasili Canada kwa ziara rasmi ya Kiserikali
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Ottawa, Canada, Jumatano mchana, Oktoba 3, 2012, kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo kwa mwaliko wa Gavana Jenerali Mheshimiwa David Johnston.
Rais Kikwete na ujumbe wake wamewasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Macdonald-Cartier wa mji mkuu wa Canada wa Ottawa kiasi cha saa nane na dakika 55 mchana baada ya safari ya ndege ya saa moja kutoka mjini New York, Marekani, ambako amefanya ziara ya siku mbili pia.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Ottawa, Rais Kikwete amelakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mheshimiwa John Baird, Balozi wa Tanzania katika Canada, Mheshimiwa Alex Masinda, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mheshimiwa Deepak Obhrai, Balozi wa Canada katika Tanzania, Mheshimiwa Robert Orr na Mbunge Mheshimiwa Joe Daniel.
Miongoni mwa viongozi wengine walimpokea Rais kwenye Uwanja wa Ndege huo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe na Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Sospter Muhongo ambao wametangulia kuja Canada lakini ni sehemu ya ujumbe wa Rais Kikwete kwenye ziara hiyo.
Kwenye Uwanja wa Ndege huo, Rais Kikwete pia ameweka saini kwenye kitabu cha kumkaribisha rasmi Canada.
Kutoka uwanja wa ndege, msafara wa Rais Kikwete umekwenda moja kwa moja hadi kwenye Nyumba ya Serikali, ambako Mheshimiwa Kikwete ametoka kwenye gari na kuingia kwenye gari maalum linalovutwa kwa farasi na kuelekea kwenye Viwanja vya Jumba la Rideau ambako amepokelewa rasmi, kwa mbwembwe zote za Ziara Rasmi ya Kiserikali.
Mara baada ya kuwasili kwenye Viwanja vya Jumba la Rideau, Rais amepokelewa na Gavana Jenerali Johnston na mkewe, Mama Sharon Johnston, amepewa heshima ya kupigiwa mizinga 21 na pia amekagua Gwaride la Heshima la Majeshi ya Ulinzi ya Canada.
Katika hotuba fupi kwenye sherehe hiyo ya mapokezi ambayo pia imehudhuriwa na Watanzania wanaoishi Canada, Rais Kikwete ameishukuru Canada kwa misaada mingi ya maendeleo ambayo imechangia sana katika jitihada za Tanzania kujiletea maendeleo tokea uhuru mwaka 1961.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mheshimiwa Kikwete, Gavana Jenerali amemshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kufanya ziara hiyo ambayo iliahirishwa mapema mwaka huu kutokana na ajali ya meli M.V. Skargit iliyozama kwenye pwani ya Zanzibar na kupoteza maisha ya watu.
Amesema Gavana Jenerali Johnston: “Nafurahi sana umeweza kupata muda wa kuja kututembelea Mheshimiwa Rais na ninayo heshima sana kukukaribisha kwenye Jumba la Rideau, nyumbani kwa wananchi wa Canada.”
Ameongeza: “Tumekuwa na uhusiano mzuri kwa miaka mingi na kwa hakika hizi ni nyakati za kusisimua na zenye changamoto nyingi kwa nchi zetu mbili ambazo zinaendelea kujenga jamii zenye uvumilivu na za kidemokrasia.”
Mara baada ya sherehe za mapokezi, Mheshimiwa Kikwete na mwenyeji wake wamefanya mazungumzo ya kiasi cha dakika 40 kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuhusu masuala ya kimataifa.
Jumatano usiku, Oktoba 3, 2012 Gavana Jenerali Johnston ameandaa dhifa ya kitaifa kwa heshima ya Rais Kikwete kwenye Jumba la Rideau.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Oktoba, 2012
Post a Comment