NI KUHUSU UTEUZI WA MAJAJI ALIYODAI HAWANA SIFA
MNADHIMU wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, ameendelea kumwandama Rais
Jakaya Kikwete, akisema baadhi ya majaji aliowateua hawana sifa, na
kwamba viongozi wa serikali waliojitokeza kumpinga wameshindwa kujibu
hoja.
Akizungumza
na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana katika ofisi ndogo ya Bunge,
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), alisema kuwa
alishatoa maelezo hayo hata katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya
Bunge inayoongozwa na Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi.
“Nilieleza
jinsi rais alivyofanya uteuzi wa baadhi ya majaji pasipo kupata ushauri
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wamekuwa wakijibu kiujumla, mimi
niliwataja kwa majina yao na hata hili nilieleza katika Kamati ya
Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani pasipo sababu za
kueleweka,” alisema.
Alisema
wanaotaka kujibu hoja zake wanapaswa kuweka hadharani orodha ya majina
ya majaji waliopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kuanzia mwaka
2005 wakati Rais Kikwete alipoingia madarakani.
Lissu
aliwataja baadhi ya watu waliowahi kujitokeza kumjibu kuwa ni Naibu wa
Katiba na Sheria, Angela Kairuki, ambaye alisema kuwa serikali ina
taarifa hizo na itazifanyia kazi.
Alisema kuwa
msimamo huo ulikubaliwa na waziri wake, Mathias Chikawe na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambao kwa nyakati tofauti walisema kuwa,
endapo serikali itachukua hatua ambazo alipendekeza watakuwa wanaingilia
uhuru wa mahakama.
Wengine
waliojitokeza kujibu hoja yake ni Jaji Mkuu, Othman Chande na Jaji
Kiongozi, Faki Jundu ambao walisema kuwa tuhuma zilizotolewa bungeni si
za kweli.
Pia Rais
Kikwete naye alikaririwa hivi karibuni akiwa jijini Arusha ambapo bila
kumtaja Lissu kwa jina, alisema kuwa majaji wanateuliwa kwa kufuata
utaratibu na wana sifa zinazostahili.
Ni kutokana
na kauli hizo, Lissu alifafanua kuwa, katika hoja zake alisema kuna
baadhi ya majaji waliteuliwa bila kuwa na sifa maalumu kama
zilivyobainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 109,
kipengele cha 6, 7 na 8.
“Ibara hiyo
ya 109 kipengele cha 6-8 kinasema; mtu anaweza kuwa Jaji iwapo tu ana
shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambuliwa kisheria, awe
ameshakuwa hakimu, awe ameshakuwa wakili na kusajiliwa na sifa zote hizo
ziambatane na utumishi wa miaka kumi mfululizo.
“Lakini sifa
zote hizo lazima mtu anayeteuliwa kuwa Jaji awe nazo kwa miaka kumi
mfululizo. Sasa badala ya kuzungumzia masuala hayo kwa ujumla jumla,
ningependa wanaonijibu watamke wazi wazi Jaji Mbaruku Salumu Mbaruku
alisoma chuo kipi na akapata shahada ya sheria iliyompa sifa ya kuwa
jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar kabla ya kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama
ya Rufaa hadi sasa,” alisema.
Alishangaa
viongozi wanaojitokeza kumjibu akisema hata Katiba ya Zanzibar 94 (3)
inasema; ili mtu achaguliwe kuwa jaji, ni lazima awe na shahada ya Chuo
Kikuu.
“Huyu jaji ambaye anasoma sasa alipataje kuwa jaji kabla ya kuwa na shahada ambayo ndiyo sifa ya msingi?” alihoji.
Lissu
aliwataja majaji wengine ambao wameteuliwa bila kuwa na sifa kuwa ni
Fatuma Masengi, ambaye kwa mujibu wa Lissu alikuwa Hakimu wa Mahakama ya
Mwanzo Singida na baadaye akawa Hakimu Mkazi kisha akaanza kujisomea
Chuo Kikuu Huria na kuhitimu mwaka 2003 na kuteuliwa kuwa jaji mwaka
2006.
Alihoji kuwa kama katiba inaelekeza mtu awe jaji ni mpaka awe amekuwa hakimu kwa miaka 10, huyu alipataje kuwa jaji?
Majaji
wengine waliotajwa ni Latifa Mansoor, ambaye pamoja na kuwa na shahada
ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyotunukiwa 1993, lakini
alifukuzwa kwa udanganyifu na ubadhirifu akiwa mfanyakazi katika
Manispaa ya Ilala.
Kwamba
baadaye alipoibuka mwaka 2008 aliteuliwa kuwa jaji wakati hajawahi kuwa
wakili, na kwa kuwa alifukuzwa katika utumishi wa umma.
Lissu pia
alimlalamikia Rais Kikwete kwa kutumia vibaya madaraka yake kwani
anateua majaji wa mikataba, ambao wameshastaafu na kulipwa mafao yao.
Aliongeza
kuwa, majaji wengine waliteuliwa na Rais wakiwa wagonjwa ili waweze
kupata fursa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi, ambapo alimtolea mfano Jaji
Mwendwa Malecela kuwa tangu ateuliwe mwaka 2006 hajawahi kusikiliza
kesi hata moja. Badala yake Lissu alidai kuwa jaji huyo huenda matibabu
India tu.
Kufuatia
utata huo, Lissu emeendelea kushikilia msimamo wake kuwa anakusudia
kupeleka hoja binafsi bungeni ili Bunge liweze kuchunguza utendaji wa
rais kuhusu uteuzi wa majaji.
Lissu
alisema Bunge litaangalia kama rais ameteua majaji kwa mujibu wa katiba
au ameikiuka, na kwamba yeye ana uhakika kuwa rais amekiuka katiba.
Tanzania Daima
Post a Comment