Shilingi bilioni 86 zaibwa Wizara ya Nishati/TANESCO, Gridi ya Taifa hatarini
Gazeti la The East African la Novemba 24 – 30, 2012
limetoa taarifa kwamba jumla ya dola za kimarekani milioni 54
zimegundulika kuibwa na watumishi waandamizi wa Wizara ya Nishati na
Madini na Shirika la TANESCO kupitia manunuzi ya Mafuta ya kuendesha
mtambo wa Umeme wa IPTL. Gazeti hili limenukuu taarifa ya ukaguzi kutoka
kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Tanzania (Controller and Auditor
General). Taarifa hiyo inasema kuna kikundi (racket) ambacho kazi yake
kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango wa umeme wa dharura kupitia
manunuzi ya Mafuta mazito ya IPTL.
Itakumbukwa kwamba toka mwaka 2011 kumekuwa na shinikizo lililotolewa
na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba zabuni za
ununuzi wa mafuta ya kuendesha mpango wa umeme wa dharura na mchakato
mzima wa manunuzi ya mafuta haya ufanyiwe uchunguzi wa kina (forensic
audit).
Katika mkutano wa 3 wa Bunge la Kumi (April 2011) niliuliza swali
Bungeni kuhusu kashfa hii ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mtambo wa
IPTL na baadaye tarehe 16 Aprili 2011 nilimwomba Spika airuhusu Kamati
ya Nishati na Madini kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hii. Kamati ya
Nishati na Madini chini ya aliyekuwa Mwenyekiti ndugu January Makamba
ililitaka Bunge kuazimia kufanyika kwa uchunguzi kuhusu suala hili
kwenye Taarifa yake ya mwaka 2011 iliyowasilishwa Bungeni mwezi Aprili
mwaka 2012. Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ndugu John Mnyika katika
Hotuba yake ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2011 alipendekeza kufanyika
kwa uchunguzi kuhusu kashfa hii pia. Juhudi zote hizo hazikuzaa matunda.
Kipindi hicho kiwango kilichokuwa kinahojiwa kuibwa ni shilingi
bilioni 15 tu. Taarifa ya The East African kama walivyonukuu kutoka
kwenye taarifa ya CAG inaonyesha fedha zilizoibwa ni shilingi bilioni
86.
Zabuni za kununua mafuta ya kuendesha umeme wa dharura zimekuwa
zikitolewa bila kufuata utaratibu wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya
manunuzi. Hivi sasa kila mwezi Tanzania inatumia dola milioni 70 kununua
mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme. Fedha hizi zinatoka Hazina na
sehemu ndogo kutoka TANESCO. Wakati fedha hizi bilioni 112 zinachomwa
kila mwezi kununua mafuta mazito na dizeli ya kuendesha mitambo ya
umeme, Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kwamba Bwawa la Mtera hivi lina
kina cha maji chini ya kiwango kinachotakiwa na uzalishaji wa umeme ni
asilimia 20 tu ya uwezo (installed capacity).
Iwapo TANESCO wataendelea
kutumia zaidi maji yaliyopo Mtera, Mitambo itashindwa kazi na Gridi
nzima itasimama maana Mtera ndio nguzo kuu ya Gridi ya Taifa. Hali hii
ni hatari sana kwa uchumi na ulinzi na usalama wa Taifa. Kimsingi Gridi
ya Taifa ipo hatarini kutokana na kiwango cha Maji kilichopo Mtera hivi
sasa na kuendelea kupungua kwa kina hicho cha maji.
Wananchi wanapaswa kuelezwa kinaga ubaga nini kinaendelea katika sekta ndogo ya umeme hapa nchini;
1. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuhusu zabuni
za manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura iwekwe
wazi na ‘racket’ inayosemekana kuiba jumla ya shilingi bilioni 86
ionyeshwe na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja na bila kuchelewa.
2. Waziri wa Nishati na Maadini auleze umma hali yalisi ya sekta
ya umeme nchini, uzalishaji wa umeme upoje, hali ya maji katika bwawa
mkakati la Mtera na nini hatma ya mitambo ya IPTL, kesi zake na
utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge kuwa kesi za kampuni hii zimalizwe
nje ya mahakama. Pia Taifa lielezwe Mpango wa Dharura wa umeme unakwisha
lini maana muda uliotolewa na Bunge mwezi Agosti mwaka 2011 tayari
umekamilika. Waziri aeleze hatua agni amechukua baada ya kukabidhiwa
taarifa na CAG kuhusu maafisa waandamizi wa Wizara waliohusika na wizi
wa shilingi bilioni 86 za kununua mafuta ya IPTL.
3. Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma ni kiwango gani cha
fedha Hazina imetoa kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa
dharura kati ya Mwezi Novemba mwaka 2011 na Oktoba mwaka 2012 na kama
taratibu zote za zabuni zilifuatwa na pale ambapo hazikufuatwa ni hatua
gani PPRA wamechukua dhidi ya waliokiuka sheria ya manunuzi na kuleta
hasara ya mabilioni ya fedha kwa Serikali.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha
Dar es Salaam. Novemba 25, 2012
Post a Comment