Na Sarah Mossi
Wazanzibari walisahau mambo mengine, walijikita kwenye Muungano.
VIONGOZI wa CCM na CUF Zanzibar, wanadaiwa kutibua kwa makusudi zoezi la ukusanyaji maoni ya Katiba mpya lililomalizika visiwani humo juzi na kusababisha wananchi kutoaminiana na kuheshimiana.
VIONGOZI wa CCM na CUF Zanzibar, wanadaiwa kutibua kwa makusudi zoezi la ukusanyaji maoni ya Katiba mpya lililomalizika visiwani humo juzi na kusababisha wananchi kutoaminiana na kuheshimiana.
Viongozi hao wanatuhumiwa kufanya kampeni ya kuwashawishi wafuasi wao
nini cha kuzungumza wakati Tume ilipokuwa ikichukua maoni ya wananchi
kwenye maeneo mbalimbali ya Zanzibar na kusababisha kutokea vurugu
zilizoacha watu kadhaa wakijeruhiwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba upande wa Zanzibar,
Profesa Mwesiga Baregu, aliiambia RAI kuwa viongozi wa kisiasa Zanzibar,
wamefanya kampeni kwa wafuasi wao na kuwahadaa, ili waione Tume kama
mkusanyaji wa kura ya maoni kuhusu Muungano.
Akizungumza na RAI katika mahojiano maalumu mara baada ya kumaliza
kazi ya kukusanya maoni Zanzibar, Profesa Baregu amesema licha ya watu
wengi kujitokeza kwenye mikutano iliyoandaliwa na Tume hiyo , lakini
wajumbe walishangazwa kuona maoni yalikuwa ya kuegemea katika Muungano
na kusahau vipengele vingine.
Profesa Baregu alisema wananchi wengi (wafuasi wa CUF) walikuwa
wamejikita kwenye hoja ya Muungano wa ‘Mkataba’ na tunadhani ndio
waliosababisha vurugu katika mikutano ya Tume na wale wa CCM
walijitokeza na kugusia Muungano wa Serikali mbili na kuondolewa kero za
Muungano.
Profesa Baregu alisema licha ya Makamishna kujaribu kuwaelekeza
wananchi wanatakiwa kutoa maoni ya mabadiliko ya Katiba na siyo ya
Muungano pekee, lakini kazi hiyo ilishindikana.
“Ama kwa kutojua ama vinginevyo lakini viongozi wa siasa Zanzibar
wamefanya kampeni kwa watu wao waseme nini, wamefanya kama kura ya maoni
kuhusu muungano, wanafikiria namba za watu kwamba tume itaamua nani
kapata wingi nani kapata wachache.
“Tuliwaeleza jambo kubwa hapa ni zoezi la kuchukua maoni ya watu, si
kuhesabu wangapi wamesema nini, bado ilishindikana, hawa wa mkataba
walisema tu mkataba…. mkataba, bila kutoa maoni mengine, angalau hawa
waliotaka serikali mbili waligusia kero ziondolewe na hapo ndipo watu
wakaanza kuzomea, kushangilia na hilo likasababisha ushabiki wa kisiasa”
alisema Profesa.
Profesa Baregu alisema uzoefu alioupata katika zoezi hilo, ni
kutokuwapo kwa maridhiano miongoni mwa jamii ya watu wa Zanzibar na
kuelekea kugawanyika kinyume na watu wanavyofikiria.
“Tumepata viashiria ambavyo hapo baadaye tutapata mgogoro ambao
utaathiri hata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…. iweje
katika Serikali ya maridhiano, lakini huyaoni hayo maridhiano yenyewe?
“Ni muhimu sasa viongozi watafute muafaka katika jamii na namna ya
kuondoa uhasama wa waziwazi ambao si mzuri kwa hali ya baadaye….Kuna
umuhimu wa kujenga kuaminiana kati ya watu na kuelewa wote wataishi
katika Zanzibar na lazima itafutwe namna ya kuishi pamoja bila ugomvi na
kuheshimiana” alisema Profesa Baregu.
Hivi karibuni wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikiwa katika hatua
za mwisho kupokea maoni ya wananchi wa Zanzibar juu ya mabadiliko ya
katiba mpya kulitokea vurugu kwenye maeneo mbali mbali ya Wilaya ya
Mjini Unguja na kusababisha baadhi ya watu kujeruhiwa kwa kuchomwa visu.
Vurugu hizo zilizotokea katika mikutano ya kukusanya maoni, zilidaiwa
kusababishwa na wanasiasa na kulazimisha Makamishna wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kusitisha mikutano.
Hali iliyojitokeza katika mikutano hiyo ya Katiba, imeashiria
kutokuwapo kwa kutovumiliana kisiasa miongoni mwa jamii ya Wazanzibari
kunakochangiwa na viongozi wa vyama vya siasa vikuu visiwani humo CCM na
CUF.
Julai 31, 2010, Zanzibar iliingia katika ukurasa mpya wa kisiasa
barani Afrika baada ya wananchi wake kupiga kura ya maoni kubadili
katiba ili kuruhusu uundwaji wa serikali za kuwagawana madaraka.
Kura hiyo iliungwa mkono na vyama vyote vikuu vya siasa visiwani humo
CCM na CUF wakiwa na lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu
tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi
vya siasa uliofanyika 1995.
Katika uchaguzi huo ambao upande wa CCM, alisimama kuwania kiti cha
Urais, Dk. Salmin Amour na kwa upande wa CUFnafasi hiyo iliwaniwa na
Maalim Seif Shariff Hamad. CCM ilishinda, ingawa kwa asilimia ndogo na
kuacha malalamiko kutoka CUF na kusababisha kuwapo ghasia za kisiasa
visiwaqni zilizodumu hadi 2010, vyama hivyo vilipoamua kuwapo kwa kura
hiyo ya maoni.
Matokeo ya kura ya maoni yalionyesha asilimia 66 ya wananchi wa
Zanzibar walikubali kuwapo kwa Serikali ya Maridhiano, ambayo ingeunda
Serikali ya Umoja wa Kitaifa, huku asilimia 34 waliokataa kuwapo kwa
serikali hiyo.
Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar, walionyesha
wasiwasi wao juu ya matokeo hayo na kubainisha kuwa asilimia ya
waliokataa kuwapo kwa Serikali ya Maridhiano ni ya wale ‘wahafidhina’ wa
siasa za Zanzibar wasiotaka mabadiliko yoyote.
Wachambuzi hao walikwenda mbali zaidi na kusema kundi hilo linaweza
kuleta taabu siku za usoni wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa
itakayoundwa na kuifanya isiweze kufanya kazi zake kutokana na kile
walichokitaka kutofanyika
Chanzo:Mzalendo.net
Post a Comment