HATUA ya serikali kushindwa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu
kamati mbalimbali zilizoundwa kuichunguza Wizara ya Nishati na Madili,
imeibua hisia za watuhumiwa wa ufisadi kukumbatiwa, Tanzania Daima
limebaini.
Bunge kama moja ya mhimili huru, hadhi yake inakuwa imeshushwa kwa
kiasi fulani endapo maazimio yake yanachukua muda mrefu bila kutekelezwa
na serikali au kutofanyiwa kazi kabisa, tena kwa visingizio visivyo na
tija.
Kwa nyakati tofauti katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bunge limeunda
kamati teule ama kamati ndogo chini ya kamati za kudumu za Bunge,
kuchunguza masuala kadhaa, huku nyingi zikiigusa Wizara ya Nishati na
Madini na idara zilizo chini yake.
Hata hivyo, licha ya kamati hizo kutumia fedha nyingi za walipa kodi
kwa kusafiri na kukusanya vielelezo na kuhoji watuhumiwa, bado
mapendekezo yake yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa asilimia kubwa na
serikali.
Hali hii imewasononesha wabunge wengi makini, na kuwafanya kila mara
kusimama bungeni na kuhoji serikali ieleze ilivyotekeleza maazimio hayo,
lakini wakati wote majibu yamekuwa ya kujirudia, yasiyo na utekelezaji
wa kueleweka.
Mathalani, mwaka 2008, Bunge liliunda kamati teule kuchunguza zabuni
tata ya Kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC (sasa Dowans) chini ya
uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe.
Kamati hiyo ilileta ripoti iliyoonesha ‘madudu’ yaliyofanywa na baadhi
ya watendaji na viongozi serikalini, na hivyo kusababisha mabilioni ya
walipa kodi kufujwa kiaina.
Licha ya mapendekezo mengi yaliyotolewa na kamati husika, utekelezaji
wake umeishia kwa viongozi wa kisiasa kujiwajibisha kwa kuachia ngazi,
lakini hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa.
Kigugumizi hicho cha serikali katika utekelezaji wa maazimio ya
Richmond pamoja na Spika wa wakati huo, Samuel Sitta, kufunga mjadala
huo bila suluhu kupatikana, kimeendelea kuligharimu taifa hadi leo katia
sekta ya nishati.
Mwaka jana, Spika wa Bunge aliunda kamati ndogo mbili chini ya Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Moja ilichunguza uendeshaji na
uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi hususani ushiriki, ufanisi na
uadilifu wa Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) katika
mchakato wa uendelezaji wa sekta ya gesi nchini kwa maslahi ya taifa.
Kamati nyingine iliangalia utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, katika kuchangisha
mamilioni ya fedha kwenye idara zilizo chini ya wizara hiyo kinyume,
akidai ni za kusaidia bajeti yao kupitishwa.
Licha ya kamati zote kutoa taarifa yake na mapendekezo Novemba mwaka
jana, ambayo yaliazimiwa na Bunge zima kuwa serikali iyafanyie kazi,
bado hakuna hatua mahususi za kisheria zimechukuliwa kwa watendaji
waliozembea na kusababisha hasara hizo, badala yake viongozi kadhaa
walijiuzulu tu.
Mathalani, kamati iliyochunguza sakata la Kampuni ya Pan African
Energy Tanzania Ltd (PAT), iliyokuwa chini ya Mbunge wa Bukene, Seleman
Zedi (CCM), ilibaini kuwapo udanganyifu unaofikia jumla ya kiasi cha
dola za Kimarekani milioni 64 (sawa na sh bilioni 110) ambazo kampuni
hiyo ilijirudishia isivyo halali kama gharama walizotumia kuzalisha gesi
tangu mwaka 2004 hadi 2009.
Kwamba kati ya fedha hizo, PAT walikiri kwamba walijirudishia isivyo
halali kiasi cha dola za Kimarekani milioni 28.1; na dola milioni 36
zilizobaki wanaandaa vielelezo vya kuthibitisha uhalali wa kujirudishia
gharama hizo.
Taarifa ilisema kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini
(TPDC) na Wizara, kufikia Septemba 30 mwaka jana, PAT walitakiwa wawe
wamewasilisha vilelezo hivyo, vinginevyo wakamilishe ulipaji wa fedha
zote.
“Baadhi ya vitendo vya udanganyifu wa kimahesabu uliofanywa na PAT ni
pale ambapo mwekezaji huyu alipokuwa akitumia fedha za Watanzania
kulipia gharama za kutafuta mafuta na gesi katika nchi za Gabon, Uganda
na Nigeria,” alisema Zedi.
Kwamba alikuwa akilipwa gharama za kusafirisha gesi kutoka kwa
makampuni mawili tofauti ya Songas na TPDC kwa kusafirisha kiasi hicho
hicho cha gesi.
Zedi alisema hadi kamati inakamilisha taarifa hiyo, ilielezwa kwa
barua yenye kumb. Na CDA.90/159/01 ya Oktoba 20, 2011 kutoka TPDC kuwa
PAT walikuwa wamewasilisha vielelezo vya kiasi cha dola za Kimarekani
1,042,516.
“Katika kiasi hicho wamethibitisha kuwa dola za Kimarekani 746,153 ni
gharama sahihi za mradi na kiasi kingine dola za Kimarekani 296,363
zimegundulika na wamekubali kuwa ziliingizwa kwenye gharama za mradi
kimakosa na kinyume cha mkataba,” alisema.
Kwamba maofisa wakuu wa PAT waliajiriwa kama wataalamu elekezi kwa
nyakati tofauti na kulipwa ujira wa shughuli wanazofanya wakati pia
wanalipwa mishahara mikubwa kwa kufanya kazi zao za kawaida.
Katika kuiimarisha sekta hiyo wakati huu ambapo nchi inaingia kwenye
mchakato wa uchimbaji gesi, kamati ilitoa mapendekezo kadhaa, lakini
makubwa yakiwa ni mkataba huo kuvunjwa.
Pia Bunge liliazimia kuwa kamati ilijiridhisha bila shaka kwamba kwa
kipindi cha mwaka 2004 hadi 2009, PAT imejirudishia isivyo halali
gharama zinazofikia jumla ya dola za Kimarekani milioni 28.1 sawa sh
bilioni 46.3 na kufanya serikali kukosa gawio linalofikia dola za
Kimarekani milioni 20.1 zirejeshwe mara moja.
Kwamba kwa kuwa mapunjo hayo ni ya muda mrefu, marejesho yake
yaambatanishwe na riba kwa viwango vya benki, pia wafanyakazi wote wa
PAT waliohusika katika udanganyifu huu washtakiwe kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini hakuna utekelezaji wa
maana umefanyika katika maazimio hayo ya Bunge. Hii ni kwa mujibu wa
taarifa ya serikali iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka huu na
kukataliwa na waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini
iliyovunjwa.
Na kuhusu fedha zilizochukuliwa na PAT kinyemela, serikali imekuwa na
kigugumizi cha kuilazimisha kampuni hiyo izirejeshe, na badala yake
imeunda timu inayojulikana kama Government Negotiations Team kufanya
mazungumzo.
Tanzania Daima lilimtafuta Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, kuzungumzia utekelezaji huo wa maazimio ya Bunge,
lakini alisema suala hilo halifahamu na waulizwe TPDC wenyewe.
“Mimi napenda kuzungumzia mambo ya maendeleo na waandishi naomba
mnisaidie kwa hilo, hizi habari za kulipuana ebu tuziache, tuangalie
mbele,” alisema.
Alipobanwa aeleze kama mamilioni ya fedha za walipa kodi zilizofujwa
si habari za maendeleo, Waziri Muhongo alisema kama kuna wizi
ulifanyika, vyombo vya dola vipo na TPDC waliofanya makubaliano
watajibu.
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alisema Waziri
Muhongo anakwepa kujibu maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo na yale ya
Jairo na Richmond.
“Aliwahi kunijibu bungeni nilipohoji sakata la Jairo, akasema yeye
hafanyii kazi magazeti. Huyu anataka kulidhalilisha Bunge na kutufanya
wabunge kuwa tunafanya mambo ya hovyo, hatuwezi kukubali watumie udhaifu
huo kama uchochoro wa kulinda ufisadi,” alisema Mnyika.
Post a Comment