Leo ni siku nyingine ya mwaka mwingine 2013 , ambao ni vyema kwanza nikawatakia Watu wote wa Jimbo langu la Arusha Heri ya Mwaka Mpya na Watanzania wote kwa ujumla na Chama chetu Chadema.
Pamoja na salamu lakini pia ni muhimu tukaendelea kupongezana hasa Arusha kwani tumeendelea kuwa mstari wa mbele kupinga uonevu na dhuluma katika jamii yetu na ndio maana ujumbe wangu mwaka huu wa 2013 ni kwamba Arusha Tutaendelea kuwa kielelezo cha mabadiliko ya kweli mwaka 2013. Tuna wajibu mkubwa wa kuchukua na kufanya mwaka huu wa 2013 na wajibu huo kimsingi kabisa ni kuendelea kusonga mbele kwa kasi ambayo haijawahi kuonekana na nguvu na ujasiri ambao kila mtu akitazama atapaswa kushangaa kwani uonevu , dhuluma na ufisadi ni vitu dhaifu vinavyohitaji mshikamano wetu na nguvu zetu bila woga kuweza kupambana navyo na kushinda.

Mwaka huu 2013 hautakuwa na tofauti na mwaka jana kwa sababu ya mabadiliko ya herufi ya mwaka bali utakuwa tofauti na miaka mingine yote kama maono yetu na fikra zetu zitakuwa tofauti katika kutazama Nchi yetu kwa upendo na nia njema . Hakuna kikwazo nje ya mipaka ya fikra yetu hata kidogo , vikwazo vyote vitatokana na fikra zenye woga na hofu ndani yetu na huu ni mwaka muhimu kuchukua hatua muhimu kuushinda woga na hofu ili tuweze kuwa na legacy muhimu ya kuleta mabadiliko muhimu katika Taifa letu .

Tulipoianza leo , safari ya mwaka 2015 ndio imekaribia sana na Majambazi na majangili tunaoshindana nao wataongeza ukatili na kutafuta mbinu nyingi za kutodhoofisha na wanafikiri wataweza na mkakati wao mkubwa ni kupiga , kuchafua majina ya viongozi wenu , kufungulia watu kesi mbali mbali na kuua kama walivyofanya Arumeru na Igunga na hata Arusha Mjini na sehemu mbali mbali Nchini. Haya mambo machafu hayafanyiki kwa bahati mbaya hata kidogo bali ni mkakati wa kuwarudisha nyuma na kuwafundisha woga na kuwapandikizia maisha ya hofu ili dhuluma na uonevu viweze kuendelea kutawala .

Arusha , kila mara nimekuwa nikisema kuwa dhambi kubwa kuliko zote Duniani ni Uoga na Hofu , hakuna gereza baya Duniani kama uoga na hofu na gereza hili limeweka watu vifungoni kwa muda mrefu bila wao kujua na huku wakitafakari na kuamini kuwa wako huru , woga na hofu ni dhambi kubwa kuliko dhambi zote Duniani , mateso ya Maisha ya mwanadamu katika Taifa letu yanasababishwa na hofu na uoga ndio maana tunawajua wezi lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao kwa sababu ya hofu na uoga ya majina yao na vyeo vyao , huu ni upumbavu mkubwa sana.

Tumeibiwa , tunaonewa , tumedhulumiwa , tumepuuzwa na kusababishiwa maisha mabaya lakini tumebaki kupiga kelele tu na huku Taifa likiendelea kuteketea , sasa na tuseme basi inatosha na tusipochukua hatua muhimu ya ujasiri ya kupinga kwa vitendo maovu haya basi sababu yetu ya kuishi itakuwa ni ubatili kwa Taifa letu na vizazi vinavyokuja , Wezi wote na mafisadi wote wanajulikana na ukiwatazama hawana hofu na wengine wana imani kubwa kuwa wanaweza hata kuongoza Nchi hii katika nafasi ya Urais na kwa Bahati mbaya Taasisi nyingine za Dini zimetumika kuwasifisha mafisadi hawa kwa kupokea michango na fedha mbali mbali kwa ajili ya eti miradi ya maendeleo ya taasisi zao huku kumbe wakitumika kuwasafisha wahuni ,wezi na majambazi waliopora Taifa letu , ole wenu ninyi mnaofanya hivyo kwani hata ninyi hukumu yenu kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa sana .

Mwaka huu tutaendelea kufundishwa hekima ya kipuuzi na kijinga na makala nyingi zitaandikwa kwa weledi mkubwa wa kinafiki na kutuelekeza njia tunayopaswa kupita kufikia ukombozi wa kweli na huku wakijua hekima zao ni hofu na ,mashaka dhidi ya dhambi zao utasikia wakisema sasa Lema anapaswa kupunguza misimamo yake na kutulia kidogo kwani Arusha wakati akiwa nje ya Ubunge ilitulia , haya maneno kwangu ni upuuzi uliojaa fikra za shetani . Arusha Ndugu zangu na Rafiki zangu Mapambano bado yanaendelea na hata kama sisi tukifikiri tumeona mwanga na huku watu wengine wanahitaji nguvu zetu itabidi twende huko tukafanye kazi ya kuleta ukombozi lakini hata hivyo niwapongeze kwamba hamkuwahi kuwa chanzo cha fujo wala shari katika Jimbo letu , isipokuwa mara zote mmekuwa mkionewa sana na kupigwa pale mlipotafuta haki na usawa na utu wenu na warafiki zenu na hatima ya Nchi yenu , Msichoke endeleeni kufanya wajibu huu mkubwa bila kumogopa Mtu yeyote na propaganda za aina yeyote.

Hata hivyo ukisoma na kutazama maoni ya wadau wachache mbali mbali wakati mwingine utaona mitazamo feki na sahihi hasa kwenye jambo linaitwa maendeleo na mimi leo katika salamu zangu za mwaka Mpya kwenu ningependa kuweka mtazamo wangu kuwa “ HAKUNA MAENDELEO DUNIANI YANAYOZIDI ,HAKI , UTU , USAWA NA KUHESHIMIANA “ hivyo basi kama vitu hivi bado sio kipaumbele katika Jimbo letu na Taifa letu basi hakuna chochote kinachoweza kuitwa maendeleo kwa namna ya vitu na sisi kama watu tukakubali . Kama kiwango cha kuheshimu utu wa Mwanadamu kitakuwa sahihi katika fikra za viongozi wanaotawala basi vitu kama Maji , Barabara , Afya , na Ajira visingekuwa vitu vya kufanya tafrija mara Serikali inapofanya bali ni mahitaji muhimu katika maisha ya Mwananchi na sio upendeleo wa Serikali kwa Mwananchi . Mimi najua kama ambavyo uwezi kuandika makala na kufanya sherehe ya kununua sukari nyumbani kwako ndio ni ajabu kuona Serikali inajivunia kufanya vitu ambavyo ni wajibu wake wa Msingi ambao nilazima waufanye .

Arusha, tumepotezewa muda kwa takribani mwaka mzima , lakini tuliutumia vizuri na makusudi mabaya yaliyopangwa yalishindikana na sasa kazi inaendelea Nje ya Bunge na Ndani ya Bunge , hakika yangu kwenu hamtajuta mimi kuwa Mbunge wenu , Nitasimamia haki kwa nguvu zangu zote , nimeamua , nimeamua kutoka moyoni mwangu na niko tiyari kwa jambo lolote lile , mtanisikia Jimboni na sehemu mbali mbali Nchini katika Taifa hili , ukweli ni kwamba mwaka huu ni Die or Live , na ahadi zangu zote nazikumbukuka na hizo pia tutafanya , nitakuwa very positive katika mambo muhimu , huu sio wakati wa kupumzika hata kidogo twendeni kazini wote , tujenge Chama wote kwa nguvu zetu na akili zetu na raslimali zetu ndogo na tukimaliza kazi hii ya kutafuta uhuru wa pili tutapumzika mwaka 2016 kidogo na kazi iendelee.

Tunamshukuru Mungu kwamba tumeshinda kesi iliyokuwa imeingiliwa na Mapokezi yenu makubwa mliyonipa wakati narudi Nyumbani kutoka Dar ni kielelezo tosha kwa Nchi nzima kwa imani kubwa mliyonayo kwangu na Chama chenu , sitawangusha , Tumuombe Mungu Usiku na Mchana , vikwazo ni vingi lakini vyote tutashinda kama Che alivyosema “ HASTA LA VICTORIA SIEMPRE “ akiwa na maana “ UNTIL THE VICTORY “
Godbless Lema ( Mp)