SEKRETARIETI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
imejichimbia mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutengeneza mpango mkakati
wa namna ya kuendesha shughuli zao kwa mwaka huu.
Itakumbuka kuwa moja ya maazimio ya kikao cha Kamati Kuu
kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana, iliazimiwa
kuwa mwaka 2013 ni wa kutumia nguvu ya umma kuishinikiza serikali ya
Rais Jakaya Kikwete, kuwajibika kwa wananachi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa, alisema mpango huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa miaka
mitano wa chama hicho ulioanza mwaka 2011 na kuendelea hadi 2016.
Alifafanua kuwa kulikuwa na minon’gono kwenye baadhi ya mitandao ya
kijamii kuwa baadhi ya wajumbe wakiwamo wabunge wa chama hicho,
hawakualikwa kwenye kikao hicho, jambo alilodai kuwa ni uzushi.
Dk. Slaa alisema kuwa wajumbe wasiotokana na sekretarieti walioalikwa ni wale wenye majukumu maalumu ndani ya chama.
“Sisi tuna wabunge 49 na katika kikao hiki wabunge waliohudhuria ni
sita, ukimuacha Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe na hawa wabunge wameingia
kwa kofia za nafasi zao katika chama,” alifafanua.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa mkakati wanaoupanga utafika katika
ngazi nyingine za chama hicho kwa uamuzi kabla ya kutekelezwa.
Kwa sasa CHADEMA imejizatiti kwa kile inachokieleza kuwa ni mikakati
maalumu ya kuchukua dola kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka
2015.
Katika kudhibiti hilo, chama kimewataka wanachama wake kuacha kupoteza
muda kwa kulumbana juu ya nani awe mgombea urais na badala yake
utatengenezwa utaratibu maalumu wa wanachama kutangaza nia.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, aliweka bayana kuwa
hana mpango wa kuwania wadhifa huo wa urais na badala yake atakuwa na
jukumu la kuwafunda wagombea makini watakaopeperusha bendera ya chama
hicho kwa nafasi zote za uongozi wa vijiji na mitaa, udiwani, ubunge na
urais
CHANZO:TANZANIA DAIMA
Post a Comment