Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya, Joseph Warioba
Jaji Warioba aliyasema hayo,wakati akijumuisha maoni yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Karemjee mjini Dar es Salaam janaAlisema katika maeneo hayo, wananchi wameonyesha kukatishwa tamaa kutokana na kukiukwa kwa misingi ya kitaifa,ikiwemo utoaji haki katika sekta za elimu, afya na utawala bora.
Alisema wananchi wana wasiwasi kuhusu haki mahakamani,uchumi, huduma za kijamii na utekelezwaji wake.
Alisema uzalendo wa Tanzania, umeporomoka kwa kiwango cha kutisha na kwamba kuna mgawanyiko mkubwa kati ya vijana na wazee, ukabila na ukanda, ambapo mpasuko mkubwa wa kidini uliopo bado haujazungumzwa kwa uwazi.
Alisema uhusiano wa wananchi na wabunge wao, si mzuri kwani wananchi wanataka wawe na haki ya kumwondoa mbunge ambaye anashindwa kuwatumikia muda wowote bila kusubiri miaka mitano.
“Ndugu zangu, nyinyi mlioko hapa ni watu muhimu sana, tusaidiane kufanikisha mambo haya, kazi hii ni nzito, hata sisi tunakuna vichwa namna bora ya kuhakikisha Watanzania wanapata kile wanachokihitaji, katiba lazima izingatie mambo haya.
“Wengi huko tulikopita wamekatishwa wakulima wanasema wamewekwa pembeni ingawa kila mwaka bajeti ya Serikali inafikiliwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi, wanasema kuna matabaka katika uchumi, huduma za kijamii, wanataka shule zote za Academy zifungwe ili zilizopo ziimarishwe.
“Wakulima wanadai wamebaguliwa, kuna mpasuko wa wazi katika masuala ya kidini, uzalendo umeporomoka, kuna mgawanyiko wa wazi kati ya vijana na wazee, hoja zote hizo zimetolewa,”alisema
Alisema kutokana na maoni hayo, kazi iliyo mbele ya tume ni nzito, hivyo wanahitaji msaada wa asasi hizo ili kuweka muundo bora wa katiba nzuri kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Najua mliopo hapa ni watu muhimu sana, mje mtusaidie kutengeneza mambo haya,”alisema Jaji Warioba.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba akiwasilisha maoni ya jukwaa hilo, alisema kuna mambo matatu ambayo yanahitaji kupata muafaka kwa kupigiwa kura ya maoni kwanza kabla ya kuingizwa kwenye katiba mpya.
Hayo ni pamoja na muundo wa Muungano,alisema bado haujapata muafaka ni Katiba gani inatungwa, kwa sababu Zanzibar wana katiba yao.
Mengine ni, aina gani ya mlengo wa Katiba tunayoitunga, kuondolewa na kubakia kwa adhabu ya kifo pamoja na Rais kutokuruhusiwa kusamehe wafungwa na watuhumiwa.
Mbali na mapendekezo mbalimbali, jukwaa hilo limependekeza kuwepo kwa lugha na alama za taifa, Katiba mpya itamke kwamba Kiswahili na Kiingereza ziwe lugha rasmi za mawasiliano na kwamba taarifa zote za kitaifa zisambazwe kwa kutumia maandishi ya kawaida na nukta nundu ambapo matangazo ya luninga na yale ya mitaani, yawekewe huduma ya lugha ya alama.
Kuhusu elimu, jukwaa linapendekeza kiwango cha elimu ya msingi iwe ni kidato cha nne, na kusiwe na Mtanzania yeyote ambaye atashindwa kufika kiwango.
“Ndugu zangu, ni gharama kubwa kuwa na taifa la wajinga, kuongoza taifa la watu wasiojua kusoma na kuandika ni hatari kubwa sana, lazima tuseme kwamba kiwango cha elimu ya msingi iwe ni kidato cha nne.
“Tunapendekeza pia kufutwa kwa ofisi ya mkuu wa wilaya, watendaji na wawakilishi wa wananchi wanatosha kufanya majukumu ya kimaendeleo na kiutawala.
“Tumeshuhudia wakuu wa wilaya hawashughuliki na maendeleo, badala yake wanaingilia kazi za wengine na kufanya kazi za mino’gono ambayo ni sawa na majungu”
Naye mwanaharakati na masuala ya uraia, Renatus Mkinga, alisema Katiba mpya ni lazima iseme kuwa viongozi wa sekta nyeti kama Rais, waziri mkuu, mkuu wa majeshi, jaji mkuu, mkuu wa polisi, spika wa bunge lwawe na uraia wa kuzaliwa.
Alisema hali hiyo, itaondoa uwezekano wa watu wasiokuwa na asili ya Tanzania kuongoza sekta hizo nyeti ambazo zinahitaji uzalendo wa hali ya juu.
Mbali na JUKATA, asasi zingine zilitoa maoni yake ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), TAWLA na nyinginezo.
Wengine waliotoa maoni yao jana, ni kundi la sekta binafsi.
Mwenyekiti wa wenye Viwanda Tanzania, Felix Mosha alisema, wamependekeza katiba mpya izungumzie misingi imara ya kuendeleza uchumi chini ya muhimili wa sekta binafsi pamoja na kodi inayozingatia ushiriki wa kila mtu.
Mbali na hayo wamependekeza raslimali ziwe za watanzania wote na wawekezaji wanaotaka kuwekeza washirikiane na watanzania io kuachiwa peke yao kama inavyofanyika sasa.
“Tumezungumza mengi lakini tumegusia pia utawala bora, kwamba kuwe na kura za uwiano kwamba kila kura ya mtanzania iwe na uwakilishi bingeni na pia mawaziri wasiwe wabunge” alisema Mosha
Naye mwakilishi wa Mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP), Mary Nsemwa alitaka mpya itambue mchango wa wanawake katika kuhudumia jamii.
Alisema katiba iseme wazi raslimali za taifa zilenge kumpunguzia mzigo mwanamke na serikali iwajibike kutunza wagonjwa mahututi, wasiojiweza, yatima ili kumpunguzia mzigo huo mwanamke
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment