Naibu Waziri wa Wizara ya elimu, Philip Mulugo
Kutokana na kashfa hiyo, walimu 200 wa Mkoa wa Dar es Salaam na
wenzao zaidi ya 300 kutoka mikoa mingine kuandamana, kwenda katika ofisi
za wizara hiyo, Ijumaa ya wiki iliyopita na Jumatatu wiki hii.
Walimu hao walichukua hatua hiyo baada ya kukosa ajira katika ajira
mpya za walimu zilizotangazwa na wizara hivi karibuni licha ya kuwa na
sifa zinazostahili baada ya kuhitimu masomo katika vyuo mbalimbali
nchini. Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa walimu hao
walikosa ajira mwaka huu kutokana na uzembe uliofanywa na maofisa wa
kitengo hicho.
Baadhi ya maofisa wa wizara hiyo waliozungumza na NIPASHE wizarani
hapo, walisema maofisa wa kitengo hicho waliingiza majina ya walimu
waliokwishaajiriwa tangu mwaka jana, ambao baadhi wapo masomoni
wakijiendeleza.
Walisema kasoro hiyo imetokea kutokana na kutokuwa na takwimu za walimu waliopo kazini.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philip Mulugo, alipoulizwa alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo.
Alisema wizara yake imeanza kufanya uchunguzi kubaini kama kuna maofisa waliohusika na uzembe huo ili wachukuliwe hatua.
“Walimu kutoka Dar es Salaam na mikoani wameandamana kwa nyakati
tofauti hapa wizarani kulalamika kukosa ajira. Tunafanya uchunguzi wa
suala hili. Tukibaini wapo maofisa waliohusika na uzembe huu wa kuingiza
majina ya walimu waliokwishaajiriwa na kuwaajiri upya, nitamshauri
waziri wangu tuwawajibishe,” alisema Mulugo.
Alisema inashangaza kujitokeza kwa tatizo hilo, ambalo ni la
kizembe kwa sababu maofisa wa wizarani kama walikuwa hawana takwimu za
walimu walioajiriwa mwaka jana, ambao wamekwenda kusoma, wangepata
takwimu hizo kutoka kwa maofisa elimu wa mikoa. Mulugo alisema tatizo
lingine lililojitokeza ni kwa baadhi ya vyuo vikuu kutoleta orodha ya
walimu waliohitimu katika vyuo vyao ili wapewe ajira. “Vipo vyuo,
ambavyo havikuleta majina ya watihimu wa ualimu katika vyuo vyao ili
waweze kuajiriwa.
Lakini nao huu ni uzembe wa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu
kwa kushindwa kufanya ‘follow-up’ (kufuatilia) vyuoni wakati wameajiriwa
hapa wizarani kwa kazi hiyo,” alisema Mulugo.
Februari 13, mwaka huu, wizara hiyo ilitangaza ajira za walimu
wapya 26,537 kwa mwaka 2012/2013 watakaosambazwa katika shule
mbalimbali.
Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema kati ya ajira
hizo, 13,527 ni kwa shule za msingi, 12,973 sekondari na vyuo vya ualimu
na 41 shule za msingi za mazoezi zilizopo chini ya wizara.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment