Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mboye
...............
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimeendelea na mchakamchaka
wake ulioanzia bungeni wa kutaka hoja zake zisikilizwe baada ya
kutupiliwa mbali kimizengwe bungeni.Wabunge wa upinzani waliowasilisha hoja zao ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliyetaka mfumo wa elimu nchini ufumuliwe au kuboreshwa.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alitetea mfumo wa elimu uliopo kabla ya hoja hiyo kuondolewa kabisa.
Hoja nyingine ni kero ya maji jijini Dar es Salaam iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambayo nayo iliondolewa baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kueleza kuwa Serikali inaendelea kutatua tatizo la mbunge huyo.
Hali hiyo ilizua vurugu na matokeo yake hoja nyingine binafsi za wabunge, ikiwamo ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari aliyetaka kujadiliwa kwa mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa na jinsi linavyoathiri mfumo wa elimu nchini, ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.
Mbali na kuzitupilia mbali hoja hizo, Bunge hilo lilimalizika likiifuta Kamati ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Baada ya wabunge hao kuvutana bungeni, wameamua kufanya maandamano na mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam ili kuwaeleza wananchi kilichotokea Bungeni na kuweka mikakati zaidi.
Mkakati wa kumng’oa Spika
Katika mkutano wa hadhara, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe anasema Spika wa Bunge, Anna Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta (Poac), Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, anasema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia maslahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Zitto anataja mbinu ya kwanza ya kumng’oa spika kuwa ni kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye, ambayo imeshakamilika inasubiri wakati wake.
“Njia ya pili tuandamane hadi pale shule ya msingi Bunge… au tutumie namba zake (za simu) kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…” anasema Zitto.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto anataja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM, na ujenzi wa vyuo vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha Nelson Mandela.
“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” anasema Zitto.
Zitto aligusia pia sakata la Mtwara akisema kamati iliyofutwa ililitaka Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) kuonyesha mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta, wakaahidi kuupeleka ifikapo Aprili mwaka huu.
“Tulipowataka TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi wakasema uko wizarani. Katibu Mkuu ambaye anapaswa kwenda kujieleza kwenye Kamati ya Nishati na Madini hakwenda kwa kuwa kamati hiyo pia imefutwa. TPDC wakasema watauleta Aprili. Ndiyo hivyo kamati yetu nayo imefutwa.”
Anafafanua kuwa kitendo cha Makinda kuifuta Poac ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji na ni kinyume cha sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za umma na kinyume cha Katiba ya nchi.
Hoja ya maji
Mbunge Mnyika aliyeibua hoja ya kero ya maji jijini Dar es Salaam yeye ametoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuwa ameshughulikia matatizo ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam, vinginevyo atawahamasisha wananchi kuandamana hadi ofisini kwake kumtaka ajiuzulu.
“Natoa wiki mbili kuanzia leo waziri wa maji awe ameeleza hatua anazochukua kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji kwa Dar es Salaam. Asipofanya hivyo tutaandamana kwenda wizarani kwake kumshinikiza atekeleze yale ambayo alisema yanaendelea kufanyika,” alisema.
Mnyika pia anakumbusha ahadi ya Rais Jakaya Kikwete katika kampeni za mwaka 2010 kuhusu upatikanaji wa maji kwa Jiji la Dar es Salaam ifikapo mwaka 2013 itakuwa historia na kufafanua kuwa Rais Kikwete alidanganya.
Mnyika anabainisha kuwa takwimu za uzito wa kero ya maji kwa sasa, zinaonyesha kuwa kati ya watu wawili mmoja hapati maji safi na salama.
Anaibua tuhuma za ufisadi ndani ya wizara ya maji, akidai zaidi ya Sh96 bilioni zingetumika kupeleka maji vijini zimeliwa huku mradi wa utandazaji wa mabomba ‘ya Kichina’ ukiwa hauna tija tena
“Wakati nchi inapata uhuru miaka 52 iliyopita, asilimia 68 ya wananchi walikuwa wakipata maji safi na salama. Lakini hadi sasa ni asilimia 55 tu wanaopata huduma hiyo. Rais Kikwete aliwadanganya wananchi wa Dar es Salaam kuwa ifikapo mwaka 2013, kero ya maji itakuwa historia,” anasema Mnyika na kuongeza:
“Mwaka 1995, Rais Kikwete akiwa Waziri wa Maji aliahidi kukomesha kero ya maji Dar es Salaam. Ilani ya CCM ya mwaka 2005 ilisema kero hiyo itakuwa historia ifikapo mwaka 2010. Hayo maji yako wapi? Lazima tuungane tuing’oe CCM mwaka 2015.”
Hawatoki tena bungeni
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anasema kuwa ule mtindo wa wabunge wa chama hicho kususia vikao vya Bunge hautakuwepo tena badala yake wataendelea kupiga kelele ndani ya ukumbi wa Bunge ili haki itendeke.
“Tulikuwa tunatoka nje ya Bunge, watu wakawa wanasema kuwa hatukuwachagua ili mkatoke nje, kwanza ni sawa na kumwachia nguruwe shamba la mahindi…. Sasa hatutoki, tutakuwa tunakomaa na kupiga kelele hadi hoja zetu zisikilizwe… kama noma na iwe nomaa… kama noma na iwe nomaaa,” anasema Mbowe huku akishangiliwa na wananchi.
Bunge laogopa nguvu ya umma
Akizungumzia hukumu ya Bunge iliyotolewa na Kamati ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo hata hivyo haikuwachukulia hatua wabunge waliotajwa kuhusika na kukiuka nidhamu ya Bunge, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anasema Bunge limeogopa nguvu ya umma. “Ijumaa iliyopita mliona Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Bunge, Hassan Ngwilizi akitoa hukumu, ilikuwa mimi, Mnyika, Pauline Gekul na Joshua Nasari tufungiwe kuhudhuria Bunge kwa miezi sita,” anasema na kuongeza:
“Wakati hukumu inaendelea kusomwa walipigiwa simu wakasema kama wakiisoma hukumu hiyo mitaani hapatakalika… wanaogopa wananchi. Kama wataendelea bungeni hapatakalika… hakuna hoja itakayopitishwa… hadi kieleweke.”
Akizungumzia Mabaraza ya Katiba yaliyotangazwa na Tume ya Katiba hivi karibuni, Lissu anasema tume hiyo imekula njama ya kuiongezea CCM muda wa kutawala kwa kuyahusisha mabaraza hayo na wingi wa watendaji wa chama tawala.
“Haya mabaraza yatakuwa katika makao makuu ya wilaya, ina maana kuwa wananchi walioko kwenye kata, vijijini na mitaa hawatashirikishwa…Kila mtaa utatoa watu wanne watakaoingia kwenye kamati zitakazosimamiwa na madiwani,” anasema na kuongeza:
“Asilimia 95 ya madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa nchini ni wa CCM. Mabaraza ya Katiba yatakuwa na ma-CCM kwa asilimia 90, watajadili nini kama siyo CCM tu? Hii ni mbinu ya kuipa CCM ARV ya kurefusha utawala wake, siyo suala la wanasheria tu, ni suala la wananchi kuingia barabarani kupinga.”
NA MWANANCHI
Post a Comment