HOFU ya mtandao wa Freemason imeanza kuathiri shughuli
zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini
(NIMR) Kanda ya Ziwa.
Meneja wa NIMR wa kanda hiyo, Dk. John Changalucha alithibitisha hayo
juzi alipokutana na viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na waandishi
wa habari, kwa lengo la kutoa ufafanuzi juu ya uvumi ulioenea kwamba
ofisi yake inafanya kazi kwa kushirikiana na Freemason.
Katika kikao hicho, Dk. Changalucha alisema tangu katikati ya mwaka
jana, kumekuwepo na uvumi huo katika Wilaya ya Geita na Kahama mkoani
Shinyanga.
Alisema baadhi ya wananchi wanahofia kazi ya utafiti pamoja na
matibabu ya magonjwa ya binadamu vinafanywa kwa ‘kivuli’ cha Freemason.
“Uvumi huu ni mbaya na umeathiri baadhi ya shughuli za NIMR za
kitafiti na huduma za kiafya kiasi cha kusababisha baadhi ya wajawazito
na kinamama wenye watoto wachanga kukataa kuhudhuria kliniki wakihofia
usalama wa maisha yao,” alisema.
Alitoa mfano kuwa mwaka jana, wilayani Kahama wananchi walikataa
kutumia jengo la afya lililojengwa kwa fedha za serikali kwa madai kuwa
liliwekwa nembo ya Freemason.
Mbali na wananchi wa Wilaya ya Kahama, katika hospiitali ya Wilaya ya
Nyamagana jijini Mwanza nako hali kama hiyo ilijitokeza ambapo baadhi
ya wajawazito walikataa kufanyiwa utafiti juu ya dawa sahihi
inayohitajika kutibu malaria wanapojifungua.
Dk. Changalucha alisema utafiti huo ulihusisha kuangalia maambukizi
ya ugonjwa wa malaria katika kondo la nyuma la akina mama punde
wanapojifungua.
“Ukweli ni kwamba NIMR haina uhusiano wowote na Freemason. Tunasema
haya kwa sababu NIMR ni taasisi ya kiserikali ambayo imeanzishwa kwa
mujibu wa sheria ya Bunge, na inafanya kazi zake chini ya Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii,” alisema.
Aidha, alizitaja baadhi ya kazi zinazofanywa na NIMR kuwa ni
kutekeleza, kusimamia na kuendeleza matumizi ya matokeo ya utafiti wa
magonjwa ya binadamu nchini.
Kwa upande wao, wawakilishi wa viongozi wa madhehebu ya dini
waliushauri uongozi wa NIMR na serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba
kanuni, taratibu na sheria za utafiti zinasimamiwa vizuri ili kuepusha
hofu miongoni mwa wananchi.
Post a Comment