Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KESI YA MURO BADO MBICHI

Aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Jerry Muro
HATIMA ya rufaa iliyokatwa na Serikali dhidi ya kesi ya aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Jerry Muro na wenzake wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10, itajulikana Aprili 29, mwaka huu.

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, inatarajiwa kutoa uamuzi wa kusikilizwa upya kwa kesi hiyo baada ya Serikali kuwasilisha rufaa ya kupinga kuachiwa huru Jerry na wenzake, ambapo imetoa sababu nne za msingi.

Hatua hiyo ilifikiwa jana na Jaji Dk. Fauz Twaibu, baada ya kusikiliza hoja hizo za Serikali zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomye na Awamu Mbagwa, wakidai kwamba, mwenendo wa kesi ulirekodiwa vibaya, hali iliyosababisha mahakama kushindwa kutenda haki na kuwaachia huru washitakiwa.

“Hakimu wa Mahakama ya Kisutu alijipotosha akashindwa kurekodi mwenendo wa kesi vizuri, ndiyo sababu mahakama ikafikia uamuzi usio sahihi, baadhi ya ushahidi haukurekodiwa vizuri na mahakama haiwezi kuelewa shahidi alikuwa anasema nini.

“Shahidi namba tano wa upande wa mashitaka, alitoa kielelezo cha kitabu cha usajili na upande wa utetezi ulipinga, lakini hakuna kumbukumbu ya kuonyesha kwamba kulikuwa na uamuzi dhidi ya pingamizi hilo,” alidai Mbagwa.

Mbagwa alitaja maeneo mbalimbali ambayo Hakimu Mirumbe aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo awali, kwamba hakuweka rekodi vizuri na maeneo mengine kilichoandikwa hakieleweki, hivyo aliiomba mahakama iamuru kesi hiyo isikilizwe upya ili haki itendeke.

Jaji Fauz alipitia baadhi ya maeneo ambayo yanalalamikiwa na Serikali na kusoma aya ya 46 ambapo alifika mahali akashindwa kujua kitu gani kiliandikwa na kuomba msaada kwa Wakili Majura Magafu, ambaye pia alishindwa kuelewa kiliandikwa nini na kurudisha jalada kwa Jaji.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Muro, Richard Rweyongeza, alisema hoja zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri haziwezi kuathiri kesi na kwamba walitakiwa kuweka wazi ni kwa jinsi gani haki haikutendeka.

Wakili wa mshitakiwa wa pili, Edward Kapama na Deogratias Ogasa, Majura Magafu, akijibu hoja za Serikali, alisema hukumu iko sawa na ilitolewa kwa mujibu wa sheria.

“Mheshimiwa jaji, malalamiko ya rufaa hii yameelekezwa katika vitu vidogo vidogo ambavyo haviwezi kuifanya mahakama ikaamua kesi irudiwe kusikilizwa.

“Mheshimiwa, mahakama ikifikia uamuzi huo ni sawa na kufanya biashara ya kubahatisha kwa kubadilisha mahakimu, yaani ukiona umeshindwa huku, unajaribu huku, hii siyo sahihi,” alisema Magafu.

Muro na wenzake walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Februari 5, 2011, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, Michael Wage.

Kesi yao ilisikilizwa ambapo upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi saba pamoja na vielelezo.

Katika shauri hili, inadaiwa kuwa, Januari 28, mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la kuomba rushwa na Januari 29,2011, kwenye Hoteli ya Sea Cliff, Dar es Salaam washitakiwa hao waliomba rushwa hiyo.

Ilidaiwa kuwa, washitakiwa hao waliomba rushwa ili kuzuia habari inayoelezea tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma iliyokuwa ikimhusu Wage, isirushwe hewani kupitia TBC1.

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe na hukumu kusomwa na Hakimu Frank Moshi, washitakiwa wote waliachiwa huru kwa sababu upande wa mashitaka ulionekana umeshindwa kuthibitisha mashitaka bila kuacha shaka.

Jaji Fauz aliahirisha kesi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika sababu ya kwanza ya kukata rufaa dhidi ya washitakiwa hao kuachiwa huru na kuahidi kutoa uamuzi Aprili 29, mwaka huu.

Uamuzi ukitolewa endapo kesi haitaamuliwa kuanza upya, mahakama hiyo itaendelea kusikiliza sababu nyingine tatu za kuikatia rufaa hukumu iliyowaachia huru akina Muro.

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top