Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MADUDU YA KIDATO CHA NNE YAZIDI KUFICHULIWA

*NECTA yabanwa, yadaiwa kutoa matokeo ya uongo
*Mwanafunzi apewa alama za juu bila kufanya mtihani

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limezidi kuandamwa na kashfa, kutokana na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa juzi kuwa mabaya.

Kashfa hiyo inazidi kuchukua sura mpya kutokana na udanganyifu mkubwa, ambapo imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi waliopata alama za juu katika matokeo hayo hawakufanya mitihani.

Taarifa hizo ziliibuliwa jana na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Green Acres, Julian Bujugo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya matokeo hayo.

Bujugo, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Magomeni, jijini Dar es Salaam, alionyesha kukerwa na matokeo hayo, huku akihoji mazingira ya baadhi ya wanafunzi wa shule yake kupatiwa alama za juu.

Katika mazungumzo yake, Bujugo alisema wanafunzi wa shule yake wamefanyiwa mchezo mchafu na baadhi ya watendaji wa Baraza la Mitihani nchini, jambo ambalo limewaathiri kisaikolojia.

Bujugo alisema katika matokeo hayo, wanafunzi wake watatu wamekumbwa na tatizo hilo ambapo mmoja wa wanafunzi hao, Amphey Sanga, aliyefukuzwa shuleni hapo kabla ya kufanya mitihani, alionekana kufanya vizuri kwa kupata daraja la tatu na pointi 24 (Div 3.24)

“Baada ya kupata matokeo haya, tumefanya uchambuzi wa haraka ambapo mwanafunzi Amphey Sanga amepewa namba ya mtihani 01197/0148.

“Matokeo yake amepata masomo ya Civics- D, Historia-D, Geograph-C, Kiswahili-D, Kiingereza-C, Physics-D, Chemistry-C, Biology-C na Hesabu-D, ambapo amepata Division 3.24.

“Tunashangaa huyu mwanafunzi amepataje alama hizi hali ya kuwa hakufanya mtihani wa Taifa na alifukuzwa hapa shuleni?,” alihoji Bujugo.

Matokeo mengine yanayoleta utata na kushangaza ni kuhusu mwanafunzi aliyefanya mtihani huo wa taifa, Martin Rushwangwa, mwenye namba ya Mtihani 01197/0173, ambaye matokeo yake yanaonyesha amepata daraja sifuri.

Mkurugenzi huyo alisema mwanafunzi huyo alisaini kufanya masomo saba ya mchepuo wa sanaa, lakini katika matokeo yake anaonekana pia amefanya masomo ya biashara kinyume cha utaratibu na sheria za mitihani.

Alisema mwanafunzi Habib Ibrahim naye alifanya mtihani huo wa Taifa, lakini katika matokeo hayo inaonyesha kama hakufanya mtihani huo, jambo ambalo sio la kweli.

“Kutokana na utata huu, hatuwezi kukubaliana kabisa na matokeo yaliyotangazwa na kwamba kuna haja ya Wizara ya Elimu kuingilia kati jambo hili haraka, ili haki itendeke kwa kila mmoja.

“Kwa matokeo haya, ni hakika hawakutenda haki na mfumo wao mpya wa kusahihisha mitihani kwa kutumia namba pekee umehujumiwa.

“Tunataka usahihishaji wa matokeo ya wanafunzi wetu urudiwe upya. Kwani hali hii imewafanya wanafunzi wengi kuathirika kisaikolojia kwa matokeo haya ya uongo yaliyotolewa na NECTA,” alisema Bujugo.

Hali hiyo imezua taharuki kwa wanafunzi wa shule ya Green Acres, jambo lililowafanya baadhi ya wazazi kulazimika kufika shuleni hapo na kupanga kuitisha kikao cha dharura Jumapili ijayo ili kujadili hali hiyo.

“Jumapili wazazi watakutana hapa shuleni kwa ajili ya kujadili hali hii na hata kutokana na uchambuzi wa matokeo ambayo bado yanaendelea kuchambuliwa, ninatumai mambo mengi tutayabani kutokana na uchakachuaji huu wa matokeo ya wanafunzi wa shule yetu.

“Katika hili nipo pamoja na wazazi na kubwa tunabaki na msimamo wetu wa kutaka ni lazima usahihishaji urudiwe na kwa gharama za baraza lenyewe. Huu ni ukandamizaji na uchakachuaji wa wazi ambapo haulipeleki Taifa letu pazuri,” alisema.

Hata hivyo MTANZANIA ilipomtafuta Ofisa Habari na Mawasiliano wa NECTA, John Nchimbi, alitaka apewe muda wa dakika 30 ili kuweza kupata ufafanuzi wa jambo hilo kwa kina.

Baada ya muda huo, Nchimbi aliwasiliana na MTANZANIA na kusema kuwa hakuna kitu kama hicho, kwani NECTA imekuwa makini katika mfumo wa usahihishaji na madai ya shule hiyo hayana ukweli wowote.

“Swali moja katika mtihani husahihishwa na mwalimu mmoja, sasa inawezekana vipi kwa mtu ambaye hakufanya mtihani apewe maksi, hili halipo na hata ukiangalia mtandao wa NECTA umeweka wazi kila kitu,” alisema Nchimbi.

Katika matokeo hayo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli.

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top