TUMESIKIA vitisho vya kila aina kutoka kwa wakubwa wenye mamlaka ya
ulinzi, wakisema kuwa watawachukulia hatua wale wote waliowatumia ujumbe
wa matusi Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.
Hatua ya viongozi hao kutumiwa ujumbe mfupi (sms) na kupigiwa simu
ilitokana na wananchi kupewa namba hizo kwenye mkutano wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wiki iliyopita.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Kabwe Zitto, aliwataka wananchi wawatumie
ujumbe na kuwapigia simu viongozi hao kadiri wawezavyo na wawaeleze
jinsi wasivyoridhishwa na namna wanavyoliongoza Bunge.
Tangu kutangazwa kwa namba hizo, tumesikia taarifa nyingi kuwahusu
viongozi hao ambazo zinadai kuwa wamekuwa wakitumiwa ujumbe wenye matusi
na vitisho, ambapo sasa wale waliotuma ujumbe huo wamehadharishwa kuwa
wakae chonjo kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Kwamba vyombo vya dola kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini
(TCRA) wanabaini namba hizo zilizotumika kutuma ujumbe wa matusi na
vitisho ili kuwachukulia hatua wahusika.
Hatukubaliani kwa namna yoyote na wale wote waliotuma ujumbe au kupiga
simu na kuwatukana viongozi hao wa Bunge. Isipokuwa tunawaunga mkono
wale waliofikisha ujumbe sahihi na kueleza hisia zao.
Tunasema hivyo kwa sababu nia ya Zitto na wenzake kuwataka wananchi
wawatumie ujumbe viongozi hao ilikuwa ni kutaka walengwa wajue kuwa
wananchi hawakubaliani na jinsi wanavyoliendesha Bunge.
Makinda na Ndugai ni sawa na Watanzania wengine. Hivyo wanapokosea ni
lazima waelezwe makosa yao, lakini kwa sitaha, si kwa kutukanwa matusi
ya nguoni kama wanavyolalamika kufanyiwa.
Laiti vyombo vyetu vya ulinzi hususan Jeshi la Polisi na TCRA wangekuwa
wanawathamini wananchi wote kama ilivyo kwa Makinda na Ndugai, bila
shaka wangekuwa wamewanasa matapeli wanaowaibia watu mamilioni ya fedha
kila siku.
Kama hili la Makinda na Ndugai kusumbuliwa kwenye simu linaweza
kushughulikiwa kwa nguvu huku wakubwa wakitamba kuwatambua waliofanya
hivyo, hao matapeli wanaotumia laini tofauti za simu kutapeli watu mbona
TCRA na polisi wamewafumbia macho?
Je, tuamini kuwa Makinda na Ndugai ni zaidi ya Watanzania wengine ama
hili la matapeli halishughulikiwi kwa sababu kuna masilahi binafsi ndani
yake?
Wananchi kila siku wanatoa taarifa polisi na TCRA kuhusu matapeli hawa
wanaotumia namba hizi za simu: 0764856797 (Anold Mhina), 0656285221
(Mwaikambo), 0656285226 na 0718498072 lakini hakuna msaada wanaopata.
Hoja yetu kwa vyombo husika ni kutaka kujua kama tumesajili simu zetu
kwa ajili ya usalama wetu au kuwatambua wanaowatumia ujumbe wa vitisho
na matusi viongozi?
Tuache hadaa kwa wananchi, lazima tukubali kuwa suala la usajili wa simu
TCRA bado ina upungufu, matapeli wamewazidi nguvu, hivyo yawezekana
lengo halikuwa hilo tuliloelezwa isipokuwa ni kulinda masilahi ya
wakubwa pekee.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment