Kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwezi Januari mpaka Februari 2013
pametokea matatizo ya kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kupungua kwa
uzalishaji wa maji katika vyanzo vya mto Ruvu na hivyo kusababisha
matatizo ya maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo
yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) katika Mkoa
wa Pwani.
DAWASA imeingia mkataba wa uendeshaji na Kampuni ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASCO) wa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo
kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na kufanya matengenezo
na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa. Aidha, DAWASCO
wanapaswa kuzingatia mikataba ya huduma kwa wateja ambayo inaitaka
kutoa taarifa kwa umma pale kunapotokea matatizo ya maji.
Kwa kuzingatia mikataba hiyo, DAWASA na DAWASCO wanapaswa kutoa
matangazo kwa umma kuhusu matatizo mapya yaliyojitokeza mwezi Januari na
Februari 2013 ili kuepusha matatizo hayo kuhusishwa na hatua ya
kuwasilishwa na kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi niliyoiwasilisha
tarehe 4 Februari 2013 juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji
wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es
salaam.
Kwa wakazi wa Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi, Saranga na Kimara ni
muhimu wakatambua kwamba nimefuatilia na kujulishwa kwamba palikuwa na
tatizo la kupungua kwa uzalishaji wa maji katika chanzo cha Ruvu Juu
ambalo limerekebishwa tarehe 12 Februari 2013 hivyo maji yataendelea
kupatikana kwa mujibu wa ratiba ya mgawo kama ilivyokuwa awali katika
maeneo ambayo yalikuwa yakipata maji tangu mwaka 2012.
Kwa wateja ambao bado watakuwa na matatizo katika maeneo yao
wawasiliane na DAWASCO kupitia namba ya huduma kwa wateja 022 55 00 240
au 0779090904 au info@dawasco.com ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kwa wananchi wa Jiji zima la Dar es Salaam ambao maeneo yao yana mabomba
yanayojulikana zaidi kama mabomba ya wachina ambayo hayatoi kabisa maji
kwa miaka mingi na wale ambao maeneo yao hayana kabisa miundombinu ya
mabomba ya maji; hatua za haraka kwa upande wao zinapaswa kutokana na
utekelezaji wa hoja binafsi niliyowasilisha bungeni.
Hali hii inayoendelea hivi sasa ya DAWASA na DAWASCO kushindwa kufanya
matengenezo ya mitambo kwa wakati na kushindwa kukabiliana na upungufu
wa uzalishaji wa maji kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam kunathibitisha
kwamba bunge lilipaswa kujadili hoja binafsi niliyoiwasilisha bungeni.
Katika maelezo ya hoja pamoja na mambo mengine nilitaka Bunge ambacho ni
chombo chenye wajibu wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi
kurekebisha kasoro zilizopo katika utendaji na uwajibikaji wa Wizara ya
Maji na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma ya maji.
Ifahamike kuwa majukumu ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam
na baadhi ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi
wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka na ina wajibu wa kupanga
na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na
kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.
Mwaka 2005 DAWASA iliingia mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na
Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya
mkataba huo majumu ya DAWASCO ni kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji
wa maji na uondoshaji wa maji taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa
ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji,
kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza
uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji.
Kisheria na kimkataba DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia
nayo mkataba; hata hivyo kwa kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma
ambayo bodi zake na watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile
na kuripoti kwa watu wale wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji
na uwajibikaji.
Wakati umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa
wazi kwa umma; kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya
utekelezaji; kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na
maandalizi kuanza ya mfumo bora unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya
kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.
Izingatiwe kuwa tarehe 10 Februari 2013 niliiwasilisha kwa wananchi na
kutoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji kujitokeza kwa umma na kutoa majibu
aliyokwepa kuyatoa bungeni na iwapo Waziri Prof. Jumanne Maghembe
hatatoa maelezo nitaongoza maandamano ya wananchi kwenda Wizarani
kuwezesha hatua kuchukuliwa.
Imetolewa tarehe 15 Februari 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Post a Comment