Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MANGULA AWAFUNGA GAVANA WANAOSAKA URAIS CCM

 MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula.
,,,,,,,,,,,,,
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula jana aliwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza mbio za kuusaka urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao, kwamba hawatavumiliwa.
Mangula, ambaye ni Makamu kwa upande wa Tanzania Bara, aliwaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kwenye semina mjini Dodoma kuwa chama hicho hakiko tayari kuona kinagawanyika tena vipande kutokana na makundi ya kuusaka urais wa 2015, na kwamba watakaofanya hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Habari kutoka ndani ya semina hiyo iliyoendeshwa chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete zilimnukuu Mangula akisema ili kuepuka viongozi kupita kwa rushwa au hila, ni lazima maadili ya chama hicho yazingatiwe na vikao vyote vinavyochuja au kuteua wagombea wa uongozi katika nafasi mbalimbali ikiwamo nafasi ya Rais.
“Ili tuweze kupata ufanisi katika chaguzi zetu, sharti tuepuke kasoro zote zinazogusa maadili ya chama na zile za utendaji ambazo zinawezesha watu wasiostahili kuchaguliwa kupenya kwenye uongozi kwa rushwa au kwa hila,”  alinukuliwa Mangula, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama hicho.
Kauli ya Mangula imekuja wakati ambao baadhi ya wanaCCM wanatajwa kuwa tayari wameanza maandalizi ya kuwania kwenda Ikulu na kwamba uchaguzi mkuu wa ndani ya chama hicho uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana ulitumika kupanga safu ya kutimiza azma hiyo.
Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Spika wa zamani, Sitta mbali na kutajwa kuwa katika kinyang’anyiro hicho, pia alinukuliwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kwamba anafaa kuwa Rais.
Jana Mangula akiwasilisha mada kuhusu maadili ndani ya CCM, alinukuliwa akisema kwamba atatumia Kamati ya Maadili ya chama hicho itakayoundwa kuhakikisha kwamba chama hicho hakipasuki kutokana na mnyukano wa siasa za urais.
“Tumeshasema ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chinichini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa,” alisema Mangula kwenye mada yake hiyo.
Habari zaidi zilisema kuwa  makamu mwenyekiti huyo alisema vikundi ambavyo vimekuwa vikianzishwa na wanaowania uongozi ukiwemo urais, ndiyo chimbuko la kukigawa chama hicho vipandevipande.
Kanuni za uchaguzi
Mangula aliapa kwamba Kamati ya Maadili ambayo yeye anahusika nayo, itavalia njuga kusambaratisha makundi na kuhakikisha tabia hiyo inakoma.
“Moja ya mambo yanayoleta mpasuko katika chama ni makundi ambayo huundwa kinyume cha utaratibu uliowekwa na NEC. Iko miiko ya kuzingatiwa wakati wa shughuli za uteuzi na uchaguzi. Miiko hiyo imepuuzwa na baadhi ya wanachama kwa makusudi au kutokuelewa,” alisema Mangula.


NA MWANANCHI
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top