
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete
akimkabidhi bajaji mpya mlemavu wa miguu ambaye ni mfanyakazi wa
TANROADS Bi.Sarah Nalingigwa Nkumbo huko ikulu mjini Dodoma leo asubuhi.
Kulia ni Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli.Wapili kushoto ni mke wa
Rais Mama Salma Kikwete na kushoto ni mkurugenzi Mkuu wa TANROADS
Injinia Patrick Mfugale. Bi. Sarah ambaye ni Mfanyakazi wa TANROADS
mkoani Singida alikabidhiwa Bajaji hiyo ikiwa ni ahadi ya Rais alipokuwa
akifungua Barabara ya Manyoni- Itigi.
Picha na Freddy Maro-IKULU
----
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Februari 10,
2013 amekabidhi pikipiki aina ya bajaj kwa mama mmoja mlemavu, Mama
Sarah Mkumbo Nalingigwa katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu Ndogo
mjini Dodoma.
Mama Nalingigwa ni
mtumishi wa Wakala wa Barabara nchini – TANROADS- katika Mkoa wa Singida
na shughuli ya leo imehudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John
Pombe Magufuli, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mufugale na
Mama Salma Kikwete.
Shughuli ya makabidhiano ya leo,
inatimiza ahadi ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa kwa Mama Nalingigwa
wakati alipokutana naye miongoni mwa wananchi waliohudhuria sherehe ya
utiaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya
mjini Itigi, Mkoa wa Singida Novemba mwaka jana.
Akizungumza mara baada ya
kukabidhi pikipiki hiyo, Rais Kikwete amemwambia mama huyo: “Nimefurahi
kwamba nimeweza kutimiza ahadi yangu. Hii ndiyo faraja yangu kwamba sasa
utaweza kufanya kazi zako kwa urahisi zaidi, utaweza kutembea kwa
urahisi zaidi na kufika kazini na kurejea nyumbani kwa namna ya haraka
zaidi.”
Naye Mama Nalingigwa amemwambia
Rais Kikwete: “Wewe ni kiongozi shupavu, kiongozi hodari na mpiganaji
anayemjali kila mtu. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalia ili uendelee
kuwaona wengine wenye mahitaji kama ya kwangu.”
Ameongeza mama huyo ambaye
amefanya kazi Wizara ya Ujenzi kwa miaka 30 iliyopita: “Kwa kuniwezesha
kiasi hiki, umenipa uwezo wa kufanya kazi kwa namna bora zaidi., Ni
vyema kuwa viongozi wengine wakaiga mfano wako wa kujali watu walioko
chini yako.”
Amesisitiza: “ Sisi walemavu tuna
mahitaji mengi na hivyo naomba unedelea kutuangalia kwa jicho la huruma
na kutupunguzia vikwazo vya maisha kila nafasi inapojitokeza.”
Post a Comment