Serikali
imetangazwa kuwa imeajiri walimu wapya 26,537 kwa mwaka 2012/2013
watakaosambazwa katika shule mbalimbali kukabiliana na uhaba wa walimu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa,
alitangaza ajira hizo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam na kusema kuwa walimu hao watasambazwa katika shule
za sekondari, msingi na vyuo vya ualimu.
Dk. Kawambwa alisema waliopangiwa shule za msingi ni 13,527, walimu
12,973 wamepangiwa sekondari na vyuo vya ualimu na 41 wamepangiwa
shule za msingi za mazoezi zilizopo chini ya wizara.
Alisema katika ajira hizo, walimu wa cheti ni 13,568, shahada ni
8,887 na stashahada ni 4,086 na kuwa mwaka huu idadi imeongezeka kwa
asilimia 11 sawa na ongezeko la walimu 2,630 ukilinganisha na mwaka
2011/12 ambao walimu walioajiriwa ni 23,907.
Alisema ajira hizo zimejumuisha walimu 841 wa stashahada waliofeli
mwaka 2011 na kurudia mitihani yao na walimu 200 wa shule za msingi
waliokuwa katika soko na kuomba ajira serikalini.
Dk. Kawambwa alisema walimu hao wanatakiwa kuripoti ofisi za
wakurugenzi wa halmashauri walizopangiwa na kwa wakuu wa vyuo Machi Mosi
mwaka huu.
Alisema mwisho wa kuripoti ni Machi 9, mwaka huu watakaoshindwa kuripoti nafasi zao zitapangiwa walimu wengine.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, alisema walimu wote
walioajiriwa watalipwa posho zao kama kawaida kulingana na utaratibu
uliowekwa na serikali.
Mulugo aliwakumbusha walimu hao kuwa serikali itaendelea
kuwachukulia hatua watakaokiuka taratibu za ajira ikiwamo ubadhirifu
alitolea mfano kuwa mwaka jana aliwasweka rumande walimu 11 kwa makosa
mbalimbali.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment