Na Dkt A. Massawe
Pamoja na habari njema za maelewano kupatikana baina ya Serikali na wenyeji wa Mtwara kuhusiana na swala la gesi asilia ya Mtwara kutumika Dar es Salaam badala ya huko huko Mtwara kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, ukweli ni kwamba bado hilo sio jibu kwa watanzania wengine wengi ambao bado wanaona kwamba gesi ya Mtwara ilibidi izalishe umeme huko huko Mtwara badala ya Dar es Salaam ili kuwezesha taifa kupata faida kubwa zaidi.
Ukweli ni kwamba upembuzi yakinifu ulikuwa ni muhimu sana ili kubaini faida na hasara za matumizi yote mbada ya gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ili kuwezesha ule mbada wenye faida kubwa zaidi kwa taifa kwa kipindi chote cha uhai wa mradi kuchaguliwa.
Hii ni kuzingatia kwamba, uzalishaji wa umeme tarajiwa kutokana na gesi asilia ya Mtwara ni mradi mkubwa unaogharimu fedha nyingi sana na wa muda mrefu na kwamba matumizi mbadala ya gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji umeme ni mingi na inayotofautiana sana kwa gharama na faida kwa vipindi vyote vya uhai wake. Miongoni mwa matumizi hayo mbadala ni yale ya gesi asilia ya Mtwara kuzalisha umeme huko huko Mtwara na gesi asilia ya Mtwara kuzalisha umeme Dar es Salaam ambayo hutofautiana sana kwa gharama na manufaa kwa taifa kwa vipindi vyote vya uhai wake.
Pia maamuzi ya Serikali kuhusu ni mbadala upi miongoni mwa matumizi ya gesi ya Mtwara mbadala kwa ajili ya uzalishaji wa umeme utumike hapa Tanzania yalibidi yahusishe wataalamu kutoka wizara zote, sekta binafsi na watanzania wote kupitia Bunge lao tukufu kwani matarajio na matakwa ya sekta mbalimbali za kiuchumi hapa nchini kutokana na matumizi mbada ya gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji umeme yanaweza kutofautiana na kupingana sana.
Hivyo, ilibidi upembuzi yakinifu ufanywe kwa kuzingatia mapendekezo ya wataalamu kutoka Wizara zote, sekta binafsi na watanzania wote kwa kupitia Bunge lao tukufu ili kuwezesha kubaini gharama na faida za matumizi yote mbadala ya gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kwa kuzingatia matarajio na matakwa ya wote kitaifa ili kuwezesha kuchaguliwa kwa ule mbadala wa matumizi ya gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa umeme unaozingatia matarajio na matakwa ya wote na ulio na manufaa makubwa zaidi kwa wote na kwa taifa lote kwa ujumla kwa kipindi chote cha uhai wake.
Ni vizuri serikali ikaweka bayana vipengele vilivyozingatiwa na taratibu zote zilizofuatwa kuwezesha kuamuliwa na Serikali gesi asilia ya Mtwara izalishe umeme Dar es Salaam badala ya Mtwara.
massaweantipas@hotmail.com