Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

SIRI ZA BUNGE ZAANZA KUFICHUKA-MKAKATI WA KUTUMIA TEKNOLOJIA WABAINIKA

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah
*Sababu za Kashilillah kusalimu amri zaanikwa
*Waja na njia nyingine ya kutumia teknolojia

WAKATI Bunge likikana kauli yake ya kupiga marufuku kurushwa moja kwa moja kwa vikao vyake, imebainika kuwa matamshi hayo yaliyotolewa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, haukuwa msimamo wa vikao rasmi vya Bunge, Mtanzania Jumapili linaripoti.
Habari kutoka ndani ya Bunge zinaeleza kuwa, Tume ya Utumishi wa Bunge ambayo ndiyo ina mamlaka ya kupiga marufuku kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao, haikuwa na msimamo huo na kwamba wajumbe wake wote wamemkana Kashilillah.

Mtoa habari wetu anaeleza kuwa hatua ya Kashilillah kubadili msimamo wake inatokana na sababu hiyo, lakini pili ni mtikisiko wa wananchi kwa jinsi walivyolipokea jambo hilo vibaya.

Katika tamko lake hilo la awali, Dk. Kashilillah alisema ofisi yake imebaini kuwa vurugu zinazofanywa na baadhi ya wabunge wakati wa vikao vya Bunge chanzo chake ni kutaka waonekane kwa wananchi jinsi wanavyoisulubu serikali na kwa wabunge wanawake wanatumia fursa hiyo kuonyesha urembo wao.

Dk. Kashilillah alisema ili kuzuia hali hiyo, ofisi yake inakusudia kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge yanayorushwa na baadhi ya televisheni na redio za hapa nchini na badala yake, vipindi hivyo vitakuwa vinahaririwa kwanza kabla ya kuonyeshwa kwa wananchi.

Habari zilizozifikia gazeti hili zinadai kuwa kauli ya Dk. Kashilillah juu ya kusudio la kuzuia vikao vya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na ile ya kukana, zote kwa pamoja zina sura mbili tofauti.

Sura iliyomo katika kauli ya kwanza ya Dk. Kashilillah inadaiwa kuwa ilikuwa ni mkakati wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulitumia Bunge kutekeleza maagizo yake yaliyopitishwa katika vikao vyake vya juu, ili kukinusuru chama hicho na tishio la kuanguka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kauli hii imekuja siku chache baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwaeleza waandishi wa habari za Bunge waliokuwa wakiripoti Mkutano wa Tisa wa Bunge la Kumi kuwa kuna mapendekezo mengi kutoka kwa watu mbalimbali yanayoitaka Ofisi ya Bunge kusitisha urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kwa sababu yamekuwa yakiwaehuwa baadhi ya wabunge.

Naibu Spika Ndugai, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina ya waandishi wa habari za Bunge iliyofanyikia kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, alisema baadhi ya wabunge wa upinzani wamekuwa wakifanya vituko bungeni wakipewa nafasi ya kuzungumza, ili waonwe na wapiga kura, hivyo ili kuwarejesha katika hali ya kawaida, yapo mapendekezo kuzuia urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, lengo likiwa kudhibiti nidhamu wakati wa vikao.

Hata hivyo, Ndugai alisema mapendekezo hayo hayajaridhiwa na Ofisi ya Bunge, kutokana na ukweli kwamba yanalenga kulirejesha zama za ujima na kwamba Bunge linatambua umuhimu wa vikao vyake kuonyeshwa moja kwa moja ili wananchi wapate ufahamu wa kinachoendelea bungeni.

Awali kabla ya kutolewa kwa kauli hizo, habari ambazo Mtanzania Jumapili lilizipata zilionyesha kuwepo kwa hali ya mashaka kwa baadhi ya viongozi wa CCM kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa shughuli za serikali bungeni, jambo ambalo limekuwa likipunguza hadhi yake na kwa upande mwingine likipandisha ile ya kambi ya upinzani.

Duru za habari kutoka ndani ya vikao vya juu vya CCM zilieleza kuwa baada ya kubainika kwa hali hiyo, aliyekuwa Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, January Makamba, katika moja ya maandishi yake yaliyokuwa yakiangalia mwenendo wa chama na namna ya kukihuisha kutoka kwenye hali ya kutokuwa na mvuto kwa wananchi, alipendekeza kupigwa marufuku kwa urushaji wa moja kwa moja wa matangazo ya vikao vya Bunge kwa sababu yalikuwa yakiwapatia umaarufu zaidi wapinzani.

Wapasha habari wetu kutoka ndani ya CCM walieleza kuwa ushauri wa January ulitolewa baada ya kufanyika kwa utafiti wa kina wa jinsi wabunge wa CCM na wale walio katika kambi ya upinzani wanavyowasilisha hoja zao bungeni na namna zinavyopokelewa na wananchi wanaofuatilia vikao vya Bunge kupitia kwenye vyombo vya habari.

Matokeo ya utafiti huo yalibainisha kuwa wabunge wengi wa CCM wanapwaya katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge na hata baadhi ya mawaziri wamekuwa wakishindwa kujibu hoja za wabunge wa kambi ya upinzani, jambo ambalo limekuwa likiisababishia serikali fedheha mbele ya wananchi, hivyo ili kudhibiti hali hiyo, January katika ripoti yake alipendekeza usitishwaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja.

Katika kile kinachoonyesha kuwa uamuzi wa awali wa Ofisi ya Bunge ulikuwa ni utekelezaji wa matakwa ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, juzi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiunga mkono kusudio hilo kwa hoja kwamba wakati vikao vya Bunge vikiendelea hakuna Watanzania wanaoviangalia kwa sababu ni muda wa kazi.

Mkakati wa kutumia teknolojia wabainika
Hata hivyo inadaiwa kuwa baada ya kuona mkakati huo umekwama, kutokana na kauli ya Kashilillah kupokelewa vibaya na wananchi, sura ya pili ambayo pia inahusisha tamko la pili la kukana lile ya kwanza ni mipango ya utekelezaji wa mkakati mwingine mpya.

Inadaiwa kuwa katika mkakati huo mpya, Ofisi ya Bunge inataka kuleta teknolojia ambapo matangazo yote ya vikao vyake yatakayokuwa yanarekodiwa kwa ajili ya kuonyeshwa moja kwa moja na vituo mbalimbali vya televisheni yatachunjwa kupitia teknolojia hiyo kabla ya kuonyeshwa.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa katika teknolojia hiyo, wakati wa hatua za kuchujwa matangazo hayo kwa kuondoa yale ambayo watakuwa hawayapendi kutakuwa na ucheleweshwaji kidogo wa urushaji wa matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni.

Taarifa hizi zinadhihirishwa na kauli mpya ya Dk. Kashilillah ya kukana kusudio la kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja akidai kuwa alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari.

Katika taarifa yake hiyo ya kukana, Kashilillah anasema mpango mkakati uliopo sasa utakuwa ni kuboresha mawasiliano ya kawaida kupitia teknolojia ya mawasiliano (bila kufafanua ni teknolojia gani).

Kwa mujibu wa taarifa yake hiyo, Bunge linatarajia kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo ya matangazo kwa utaratibu ulio rahisi ambapo sasa hapatakuwa na fursa kwa vyombo vya habari kuingiza kamera ndani ya kumbi za Bunge kama ilivyokuwa awali hivyo kuzitumia zile za bungeni.

Dk. Kashilillah alipotafutwa kuzungumzia juu ya taarifa hizo, simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa muda wote jana, na hata mwandishi walipojaribu kufika ofisini kwake nako alipewa taarifa kuwa hayupo.

Tangu kutolewa kwa tamko lenye kusudio la kuzuia matangazo ya vikao vya Bunge kurushwa ‘live’, watu wa makundi mbalimbali wakiwemo baadhi ya wanasiasa, wasomi, walilaani wakidai kuwa ni mpango wa kufunika mambo yanayotokea bungeni.

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top