Na Zitto Kabwe Via Zitto na Demokrasia
Katika mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa
ya muundo wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya maamuzi ya
Spika yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Maamuzi haya yameleta
sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na
Uwajibikaji katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC
ulitokana na misingi gani na kwamba Uamuzi wa Spika unarudisha nyuma
maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Maamuzi ya Spika
ni kinyume cha kanuni za Bunge, sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi.
Maamuzi ya Spika yanavuruga Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na
kila mdau wa Uwajibikaji nchini.
Baada ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la Ubinafsishaji, mashirika
mengi ya Umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na
chombo kinaitwa SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations)
kwa madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya Umma. Bunge
lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa
mwaka 1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika
ya Umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati
hiyo. Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William
Shelukindo wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto
mkoani Tanga.
Mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya
mkutano wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi Mashirika ya Umma
bado yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni mabaya sana nafedha
za umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public
Authorities and Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa
maelekezo kuhusu mahesabu ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa
Mashirika ya Umma. Vile vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya
Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma.
Spika wa Bunge wa wakati huo,
kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa
dkt Willibrod Slaa, Beatrice Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod
Mkono) wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge za Mwaka 2007. Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008
mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati
hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati ya POAC bado zipo na kimsingi
sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla.
Majukumu ya POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane
ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13)(a-e).
Majukumu hayo ni pamoja na kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya
Mashirika ya Umma, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za
Umma, kutathmini ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia utekelezwaji
wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka 2008
Mdhibiti na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa
taarifa za mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na
sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama
moja ya kamati zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka
ya mahesabu ya Mashirika ya Umma.
Katika kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu
yake kwa umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko kamati nyingine zote
za Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika
mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa
kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha
mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni hatua
muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini
kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye
Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya
Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa
mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali
imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii
kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi
haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za wafanyakazi
kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.
Katika maelezo yake Spika amesema nchi nyingine duniani hazina kamati
kama ya POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye
akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia
Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda
inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India
ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public
undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya
Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma
(Ministry of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa
kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni binafsi badala ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas nk hauna uangalizi
wowote.
Uamuzi wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha
nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha
sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia
fedha za Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa Bunge anasema
kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla
ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka
mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia
Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia
Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo
Mashirika ya Umma 258? Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla
ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za
Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa Wizara za
Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye Mashirika na kutumia kifisadi
ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka zaidi ya
shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011). Ikumbukwe pia wizi
wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za Serikali
kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati
inayosimamia Mashirika ya Umma.
Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya
maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya
uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna
anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna
anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya
uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa
katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba
Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la
wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo
nchi yetu itaumia.
Post a Comment