Aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa ameitwisha zigo serikali na kusema kwamba
katika uongozi wake tume ya watalaam iliyoundwa kuchunguza maghorofa
yanayojengwa chini ya viwango hapa nchini mwaka 2006, ilimaliza kazi
yake na kuwasilisha ripoti katika ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ambao
walitaka kupata maoni yake kuhusu tume aliyounda kuchunguza maghorofa
mbalimbali yanayojengwa chini ya viwango hususani jijini Dar es Salaam,
Lowassa alisema yeye alimaliza kazi yake na kwamba ripoti hiyo
imekaliwa na ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Lowassa hakutaka kuingia kwa undani katika suala hilo
kwa madai kwamba ofisi ya Waziri Mkuu ina taarifa zote ambazo zimo
katika ripoti ya mwaka 2006.
“Nendeni mkaulize ofisi ya waziri mkuu mimi sipo huko na ripoti
hiyo ya watalaam ipo katika ofisi ya waziri mkuu mimi sina cha kusema,”
alisema Lowassa.
Ripoti ya tume hiyo iliyojulikana kama "tume ya Lowassa" ilibaini
maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalitakiwa kubomolewa kutokana na
kubainika kuwa na kasoro za kitalaam jambo ambalo hadi sasa
halijafanyika.
Msemaji wa ofisi ya ofisi ya waziri alipotafutwa jana ofisini kwake
kuzungumzia ripoti hiyo ya watalaam hakupatikana na NIPASHE iliambiwa
kuwa yupo nje ya ofisi kikazi.
Wiki iliyopita jengo la ghorofa 16 liliporomoka na kuua watu 30 na
wengine kujeruhiwa huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kutokana na
kujengwa chini ya viwango vinavyotakiwa.
Tayari serikali imeunda tume nyingine inayoongozwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi kuchunguza ajali hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment