Kituo
cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinatarajia kuwakutanisha viongozi wa
dini, serikali pamoja na watu mashuhuri kwa ajili ya kujadili
mstakabali wa amani nchini kuanzia Aprili 23 hadi 24, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia ambaye pia ni Mbunge alisema wameamua
kufanya hivyo kutokana na kuwapo kwa tishio la kutoweka kwa amani
linalosababishwa na tofauti za kidini.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tayari taasisi hiyo imeshazungumza na
viongozi wa dini na serikali na wamekubali kuhudhuria mkutano huo.
Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa, alisema kumekuwapo na
viashilia vya kutoweka kwa amani nchini kutokana na matukio kadhaa ya
vurugu hususani baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
“Watanzania tulijengwa kuishi katika misingi ya kuwa na sauti moja,
kwamba kila mtu unayemuona ni ndugu yako na hakuna aliyejitokeza
akasema mimi ni wa kabila wala dini fulani. Tulijivunia katika hili hata
tunapokwenda katika nchi nyingine tulionekana watu wa amani,” alisema
Mbatia na kuongeza:
“Lakini jambo la kushangaza na kutia wasiwasi hivi sasa ni kutokana
na kuzuka kwa kasi kubwa ya chokochoko na mifarakano ya hapa na pale
katika nchi yetu ambayo hatukuizoea hasa zinazosababishwa na imani za
kidini, mfano zile za kugombania kuchinja,” alisema.
Aliongeza: “Chokochoko hizi hazina tija yeyote kwa taifa na hakuna
atakayenufaika nazo isipokuwa tutaangamia sote kama hatutafanya jitihada
za kuzikomesha.”
Mbatia alisema licha ya baadhi ya watu mbalimbali wakiwamo viongozi
wa dini na siasa kulizungumzia suala hilo, lakini hatua za makusudi za
kuhakikisha vuguvugu hizo zinakomeshwa hazijafanyika.
“Tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwa wanazungumzia sana suala
hili la tofauti za kidini ambazo zinaendelea nchini, lakini hatujaona
hatua za makusudi za kukomesha vitendo hivyo kwa vitendo zaidi ya
kuzungumza tu.
“Chondechonde ninawaomba Watanzania wenzangu tusichezee amani yetu,
tusikubali wala kumruhusu mtu yeyote anayetaka kuivuruga na anayejaribu
kutuchonganisha tumzomee sote,” alisema.
“Kwa nini watu tupoteze muda mwingi katika mambo yasiyo na tija
badala ya kufikilia mambo ya msingi. Kwa mfano, Mbeya watu wanabishania
kuchinja kwa kuonyesha jinsi gani hatuko serious (makini) wakati dunia
ni kama kijiji. Wanatushangaa sana.
Tabia inayoendelea ya watu kukalia umbeya tu na kujadili tukio
moja baada ya jingine na kusahau hoja za msingi tunapotea,” alisisitiza
Mbatia.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment