Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WANAFUNZI LONGIDO WALALAMIKIA KUNGUNI MABWENINI

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Longido mkoani Arusha, wameulalamikia uongozi wa shule hiyo kwa kushindwa kumaliza kero ya wadudu aina ya kunguni inayowasumbua usiku kucha wakiwa wamelala.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wanafunzi wa shule ya bweni inayomilikiwa na serikali ikiwa na kidato cha kwanza hadi cha sita, walisema kero ya kunguni imekuwa sugu shuleni hapo.


“Tumejaribu kutoa malalamiko yetu katika uongozi wa shule, lakini kilichofanyika alitafutwa mtu akaja kupuliza dawa ya ‘kuua’ wadudu hao, badala ya kufa ndio wamezaliana wengi na kutusumbua,” alisema mmoja wa wanafunzi hao na kuomba kutotajwa jina gazetini.


Alisema tatizo la kunguni limekuwa likiwasumbua kwa muda mrefu na kuwasababishia kutopata usingizi wakati wa usiku, hali inayofanya baadhi yao kupangisha vyumba uraiani.


Aidha, wanafunzi hao kwa niaba ya wenzao walisema tatizo jingine shule hiyo imefurika wanafunzi wengi zaidi ya 1,400 tofauti na uwezo wake wa kawaida wa kuchukua watu 800 hadi 900, na kufanya kuwapo na msongamano mkubwa.


Hata hivyo, wanafunzi hao walimlalamikia mkuu wa shule hiyo, Daniel Temu kwa kuonyesha kutojali malalamiko ya wanafunzi hao ya kung’atwa na kunguni kila kuchapo.


Akizungumzia malalamiko hayo ya wanafunzi wa shule yake, mkuu wa shule hiyo, alisema wanafunzi wenyewe ndio wanaoleta kunguni shuleni pale warejeapo toka likizo.


“Shule ikifungwa, kuna watu wamepewa tenda na halmashauri ya kupuliza dawa, lakini wanafunzi wenyewe wakirejea tu shuleni, kunguni wanaibuka kwa wingi,” alisema mwalimu Temu.


Temu alisema pamoja na wanafunzi hao kuleta kunguni, lakini uongozi wa shule unayafanyia kazi kwa nguvu zote matatizo hayo, na sasa ni awamu ya pili kupuliza dawa ya kuua wadudu hao inaendelea.


Mkuu huyo wa shule alisema, awamu ya kwanza ilifanyika na kufanikiwa kwa kiasi kuua kunguni hao, lakini awamu ya pili wapuliza dawa hiyo wametoa siku 28 kuweza kuthibitisha kuuawa kwa kunguni wote waliopo shuleni na tathimini kutolewa baadaye. Hata hivyo, Temu alipinga wingi wa wanafunzi shuleni hapo kwa kusema shule hiyo inamilikiwa na serikali na utaratibu wote wa kiserikali ndio unaofuatwa.
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top