Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Sheria na
Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akisoma
hotuba ya kambi hiyo kuhusiana na muswada wa marekebisho ya sheria
mbalimbali iliyowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
bungeni mjini Dodoma jana.(PICHA:SELEMANI MPOCHI)
......
Pia imesema ni aibu kwa serikali kuendeleza sheria hiyo, ambayo ilitumika kumtia hatiani Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere zaidi ya nusu karne iliyopita, huku ikijidai kumuenzi.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema hayo jana wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.
Muswada huo, pamoja na mambo mengine ulipendekeza kufanya marekebisho ya vifungu vya 36 (1) na 37(1) (b) vya sheria hiyo kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari, uvumi au taarifa za uongo zinazoweza kusababisha taharuki au hofu kwa wananchi, au zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani; au kuchapisha, kusambaza au kutoa taarifa ya uchochezi.
FAINI JUU
Muswada huo umependekeza kuongezwa adhabu ya makosa hayo kutozwa faini kutoka Sh. 150,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja hadi Sh. Sh. milioni tano.
Mbali na Sheria ya Magazeti, Jaji Werema alisema pia kuwa katika marekebisho ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Maigizo, adhabu kwa mtu atakayetenda kosa ikiwamo kutoa filamu au mchezo wa kuigiza wenye lugha ya uchochezi imeongezwa kutoka faini ya Sh. 5,000 hadi Sh. milioni tano.
Hata hivyo, Lissu alisema wanapinga marekebisho ya Sheria ya Magazeti kwa sababu kadri ya ufahamu wa kambi ya upinzani, tangu sheria hiyo ilipotungwa miaka zaidi ya 37 iliyopita, hakuna mwandishi wa habari au mchapishaji wa gazeti lolote aliyewahi kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ya makosa hayo.
Alisema badala ya kuwapeleka wakosaji wa aina hiyo mahakamani wakaadhibiwe kwa mujibu wa sheria hiyo, serikali imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi wa habari.
Lissu alisema hiyo peke yake inathibitisha hoja kwamba sheria hiyo ilitungwa kwa malengo ya kisiasa ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa serikali na watawala na siyo kuzuia makosa ya jinai.
“Katika hili, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kwa Bunge lako tukufu, taarifa ya kesi zote– kama zipo- zilizofunguliwa mahakamani kuhusu ukiukwaji wa masharti ya vifungu vya 36 (1) na 37 (1) (b) vya Sheria ya Magazeti tangu Sheria hiyo ilipotungwa mwaka 1976,” alisema Lissu.
Pia aliitaka serikali itoe bungeni taarifa ya adhabu zozote za faini, kama zipo, zilizotozwa kwa mujibu wa vifungu hivyo, ili Bunge lipime ukweli wa kauli yake kwamba adhabu hizo ni ndogo kulingana na ukubwa wa makosa yenyewe.
Alisema taarifa hizo zitaliwezesha Bunge kujadili na kufanya maamuzi ya busara kuhusu mapendekezo ya muswada huo, badala ya kufanya maamuzi kwa hisia na taarifa au kauli potofu kama za AG.
Lissu alisema miaka 22 iliyopita, Tume ya Jaji Francis Nyalali iliwahi kusema kuwa sheria hiyo na ile ya Magazeti ya Zanzibar 1988 kwamba, zinakwenda kinyume cha Ibara ya 18 (1) ya Katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.
Alisema Tume hiyo pia ilisema sheria hizo zinawapa mawaziri mamlaka mengi na makubwa mno na kutolea mfano, namna mawaziri walivyo na uwezo wa kuagiza gazeti lisichapishwe tena.
Lissu alisema Tume hiyo iliendelea kusema kuwa sheria hizo pia hazitilii maanani umuhimu wa magazeti katika jamii kwamba ni moja ya vyombo muhimu vinavyotoa msukumo wa shughuli za umma.
Alisema hatimaye Tume hiyo ilipendekeza kuwapo sheria, ambazo zitayapa magazeti uhuru kamili bila ya kubanwa na chombo chochote cha dola na kuendelea kunukuu taarifa hiyo kuwa:
“Tunapendekeza kuwa sheria inayohusu uhuru wa magazeti itengenezwe haraka iwezekanavyo, ikitilia maanani vilevile hali iliyopo sasa ya teknolojia ya magazeti.”
Hata hivyo, Lissu alisema kwa kipindi chote hicho, serikali imekataa kutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo, badala yake, Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
KULINDA UFISADI
“Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi, watendaji na watumishi wa Serikali hii ya CCM. Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua,” alisema Lissu.
Alisema maneno hayo waliwahi kuyasema katika maoni yao kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Vijana katika Mkutano wa Bunge la Bajeti, mwaka huu.
“Miezi mitatu haikupita tangu tuseme maneno haya kabla ya Serikali hii ya CCM kuthibitisha ukweli wake kwa kutumia Sheria ya Magazeti kuyafungia magazeti ya Mtanzania na Mwananchi,” alisema Lissu na kuongeza:
“Na sasa, kwa muswada huu, badala ya kupendekeza sheria hii ifutwe kama ilivyokuwa kwa Sheria ya Shihata (Shirika la Habari Tanzania) na kama ilivyopendekezwa na Tume ya Nyalali, Serikali hii ya CCM inaliomba Bunge kuiongezea makali zaidi.”
Hivyo, aliitaka serikali kuuondoa muswada huo kwa kufanya kile ilichokifanya kuhusiana na Sheria ya Shihata kwa kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa Sheria ya Magazeti na kutunga sheria mpya itakayohifadhi uhuru wa habari na uhuru wa mawazo.
“Kwa nchi na serikali inayojidai kumuenzi Baba wa Taifa, ni aibu kwa Serikali hii ya CCM kuendeleza sheria ya jinai ya kashfa na uchochezi iliyotumika kumtia hatiani Mwalimu Nyerere na waandishi habari wenzake wawili zaidi ya nusu karne iliyopita,” alisema Lissu.
Alisema Sheria ya Magazeti ilitungwa kwa mara ya kwanza na dola ya kikoloni mwaka 1928.
Hata hivyo, alisema haikuwa na vifungu vya jinai za kashfa na uchochezi na kwamba, viliingizwa katika sheria za nchi kwa mara ya kwanza mwaka 1953 wakati vifungu vya 51-58, 63 na 63A vya Kanuni ya Adhabu vilipotungwa.
Alisema lengo kuu la vifungu hivyo lilikuwa kuwadhibiti wakosoaji na wapinzani wa sera na dola ya kikoloni waliokuwa wameanza kujitokeza katika miaka hiyo.
“Ndiyo maana mhanga wa kwanza wa vifungu hivi alikuwa mtu aitwaye Julius Kambarage Nyerere, wakati huo akiwa Rais wa chama cha siasa cha upinzani kiitwacho Tanganyika African National Union (Tanu), na wenzake wawili,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Kwa maneno ya Ndugu Edgar Maokola Majogo, wakati huo Mbunge wa Nachingwea, katika mjadala Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria hiyo katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Pili wa Bunge hili tukufu uliofanyika tarehe 16 Machi, 1976, kulikuwa bado na “... harufu ya kuwa na kasumba kasumba za kikoloni katika sheria zetu ambazo tumezirithi.”
Alisema Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Uhuru wa Mawazo na Uhuru wa Habari, Pansy Tlakula, alisema sheria za jinai za kashfa zinatumika karibu mara zote kuadhibu ukosoaji halali wa wenye madaraka badala ya kulinda haki za watu kuwa na haiba/sifa wanazostahili.
Lissu alisema kwa sababu hizo, Katiba Mpya ya nchi ya Kenya imepiga marufuku matumizi ya sheria za jinai za kashfa kuhusiana na mawazo au maoni au matangazo, na uchapishaji au usambazaji wa habari kwa kutumia njia yoyote.
Alisema hata Zimbabwe, licha ya majanga ya kisiasa yaliyosababisha nchi hiyo kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, nayo imepiga marufuku matumizi ya sheria hizo kwa mujibu wa Katiba Mpya ya nchi hiyo ya mwaka huu.
“Cha kushangaza zaidi ni kwamba, licha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuonyesha mwelekeo wa kupanua uhuru wa maoni, fikra na uhuru wa habari na vyombo vya habari, Tanzania imebaki nchi pekee katika ukanda wa Afrika inayoendeleza kasumba za kikoloni katika sheria ambazo imezirithi,” alisema Lissu.
Alisema sababu zilizoelezwa na Jaji Werema za kuandaa mapendekezo ya muswada huo kwamba, zina uhusiano na shambulio la kigaidi katika Kanisa Katoliki Olasiti, mkoani Arusha siyo sahihi.
Lissu alisema hiyo ni kwa sababu, hadi leo ikiwa ni zaidi ya miezi minane tangu shambulio hilo, serikali haijatoa taarifa yoyote rasmi, iwe ndani au nje ya Bunge kuhusu sababu za shambulio hilo la kikatili ndani ya nyumba ya ibada, au wahusika wake.
Alisema hivyo hivyo, miezi mitano baadaye, serikali haijatoa taarifa yoyote rasmi ndani au nje ya Bunge kuhusu sababu za shambulio la Bomu la Soweto, Arusha, kwenye mkutano wa Chadema wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa madiwani lililosababisha vifo vya watu wanne.
Lissu alisema ukimya huo mkubwa wa serikali unaashiria kwamba hadi sasa, haifahamu sababu za mashambulio hayo ya kigaidi.
Alisema dhana ya AG kwamba mapendekezo hayo yanalenga kuzuia kauli za uchochezi inapotosha kwa makusudi ukweli halisi juu ya lengo na maudhui ya Sheria ya Magazeti na marekebisho yanayopendekezwa kwenye Muswada huo.
Kuhusu marekebisho ya sheria ya filamu na michezo ya kuigiza, Lissu alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani na mapendekezo hayo na sababu zilizotolewa na serikali.
Alisema kambi inaona kuwa lengo halisi la mapendekezo hayo ni kuendelea kuminya na kudhibiti uhuru wa mawazo, maoni na fikra ambao umehifadhiwa na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
MHAGAMA AMKOSOA CHANA
Akichangia muswada huo, Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, alitofautiana na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Pindi Chana, aliyehoji la kufanya kama kuna magazeti yanachapisha habari za uchochezi na zenye kuhatarisha amani ya nchi.
Mhagama japo hakutamka waziwazi, aliunga mkono maoni ya kambi hiyo akisema badala ya Sheria ya Magazeti kurekebishwa kila siku, ni vyema sasa serikali ikapeleka bungeni muswada kuhakikisha sheria ya kusimamia na kulinda tasnia ya habari inapatikana.
CHANZO:
NIPASHE