Tume ya uchaguzi ilisema Magufuli alipata asilimia 58.46 ya kura zilizopigwa.
Mgombea urais kupitia chama cha CCM John Mafuguli amepewa cheti cha ushindi baada ya 
kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.
Bw Magufuli amekabidhiwa cheti hiyo kwenye hafla iliyoandaliwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Hafla
 hiyo imehudhuriwa na kiongozi anayeondoka mamlakani Rais Jakaya Kikwete
 pamoja na waangalizi wa uchaguzi kutoka makundi mbalimbali.
Kadhalika,
 mgombea wa pekee mwanamke katika kinyang'anyiro hicho Bi Anna Mghwira 
wa chama cha ACT Wazalendo alihudhuria hafla hiyo, na kumpongeza Bw 
Magufuli kwa ushindi wake.
Kiongozi huyo mpya hakutoa tamko lolote wakati wa hafla hiyo na alifululiza moja kwa moja hadi ikulu chini ya ulinzi mkali.
Mwenyekiti
 wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mstaafu Damian Lubuva 
alisema Alhamisi kuwa Magufuli, alijipatia kura 8,882,935 ikiwa ni 
asilimia 58.46.
Mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa chama 
cha Chadema alijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura 
zote halali.
Matokeo hayo yamepingwa na Bw Lowassa na chama chake.
Akiwahutubia wanahabari kabla ya kutangazwa kwa matokeo Bw Lowassa alidai tume imeshirikiana na chama tawala kumpokonya ushindi.
Aliitaka tume hiyo 
kumtangaza kuwa mshindi.
Lakini tume hiyo imejitetea na kusema mchakato wote ulikuwa huru na wa haki na kwamba uliendeshwa kwa kufuata katiba.
Bw Magufuli, ambaye alikuwa 
Waziri wa Ujenzi katika serikali ya Rais Kikwete, anatarajiwa kuapishwa kuwa rais katika muda wa siku saba zijazo.
BBC SWAHILI. 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
Post a Comment