Vyama sita vya siasa vimemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar 
(ZEC) Jecha Salum Jecha kujiuzulu kwa kukiuka katiba ya uchaguzi na 
kutaka kuiingiza nchi katika machafuko.

Wajumbe wa vyama sita vinavyomtaka 
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kujiuzulu; vyama hivyo ni 
Demokrasia Makini, SAU, CHAUMA, NRA, Jahazi Asilia, na DP wakizungumza 
na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace 
iliyopo Malindi Mji Mkongwe wa Zanzibar
Vyama hivyo ni pamoja na Demokrasia Makini, SAU, CHAUMA, NRA, Jahazi 
Asilia, na DP ambao wamezungumza na waandishi wa habari jana katika 
ukumbi wa hoteli ya Grand Palace iliyopo Malindi Mji Mkongwe wa 
Zanzibar.
Akizungumza na katika mkutano huo Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa 
tiketi ya CHAUMA, Abdallah Kombo Khamis alisema wao kama wana siasa na 
ni wazanzibari hawapo tayari kuona demokrasia inavizwa wakakaa bila ya 
kutoa tamko lolote.
“Kwa vyovyote vile iwavyo, hatutakubali uvizwaji wa demokrasia wa aina 
yoyote, kwamba kwa kuwa matokeo tulioyoyataja kutokwenda sambamba na 
matarajio ya CCM, mwenyekiti wa ZEC amekubali kutumika kukinusuru chama 
cha CCM ambacho yeye ni mwanachama aliyewahi kuwania ubunge kupitia 
chama hicho”  alisema Mgombea huyo.
Wamesema sababu alizozotoa Mwneyekiti wa tume ambazo zimepelekea kufutwa
 kwa uchaguzi huo zilikuwemo ndani ya uwezo wa tume yake kuzifanyia 
marekebisho hata kabla hazijaathiri zoezi la uchaguzi wote katika hatua 
ya mwisho.
Alisema Mwenyekiti huyo ameshindwa kuchukua hatua mwafaka muda uliofaa 
katika mambo yaliokuwa ndani ya mamlaka yake unatia mashaka juu ya 
ukweli wa hoja zake.
“Zaidi ya yote ametoa maelezo jumla jumla hakuainisha ni eneo lipi hasa 
lililohusika ili na wadau wengine wakajiridhisha na maelezo yake, hili 
linatia shaka” alisema.
Mgombea huyo ambaye aliambatana na wagombea wenzake wa vyama vilivyounda
 umoja huo kwa ajili ya kutoa yamko lao la kupingana na Mwenyekiti wa 
Tume  mbali ya kulaani tukio la Mwneyekiti lakini pia wanaona uamuzi 
wake huo utaathiri matokeo ya uchaguzi wa Muungano.
“Huku demokrasia ikipindwa katika kiwango hicho, mitaani wananchi 
wamekuwa wakipata mateso ya kupigwa na kuumizwa vibaya pasipo na sababu 
kunakofanywa na vikosi vya ulinzi, vitendo hivi ni uvunjifu mkubwa wa 
haki za binaadam na haki za watu hivyo tunaiomba serikali ichukua hatua 
kusitisha mara moja mateso kwa raia zake” aliongea kwa uchungu Khamis.
Walisema khofu yao uchaguzi utakaofutwa na kurejeshwa tena hali ya 
wananchi itakuwa tete zaidi nap engine kupelekea mauaji kama yaliowahi 
kutokea katika chaguzi zilizopita.
“Sisi tukiwa miongoni mwa wagombea urais wa Zanzibar hatujaridhika na 
maamuzi pweke ya Jecha na hivyo tunaitaka ZEC ikae katika kikao halali 
cha tume iyoe tamko ya kufuta kauli ya Mwenyekiti wao na kueleza 
umaliziaji wa hatua iliyobaki ya majumuisho na matangazo ya uchaguzi wa 
nafasi ya urais wa Zanzibar ili aliyeshinda apewe haki yake katika njia 
ya kidemokrasia ili nchi yetu idumu hali ya Amani na utulivu” aliongeza.
Mgombea huyo alisema suala la uchaguzi lina gharama kubwa ambapo 
Zanzibar imetumia shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya uchaguzi hivyo 
kuijeresha tena Zanzibar ndani ya uchaguzi ni kuingia tena kwenye 
gharama kuliangamiza taifa.
“Tunaziomba jumuiya za kimataifa na taasisi nyengine kusaidia kulimaliza
 tatizo la uchaguzi huu kwa kuhakikisha kuwa aliyeshinda anapewa haki 
yake ili Amani iendelee kudumu Zanzibar” alisema Khamis.
Aidha mgombea huo aliitaka tume ya uchaguzi Zanzibar kuendelea na 
mchakato na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa mujibu wa fomu 
zilizokusanywa katika vituo vya kupigia kura.
Pia mgombea huyo aliiomba tume ya kimataifa na mashirika ya maendeleo 
kuingilia kati suala hilo kwa kutumia waangalizi wa jumuiya mbali mbali 
zilizoshiriki katika uchaguzi huu ambapo wao wanaweza kupata taarifa 
kamili na za uhakika.
Katika kutoa wito wamewataka wazanzibari wote bila ya kujali itikadi za 
kisiasa kuwa tayari kupigania haki zao na kuhakikisha demokrasia 
inachukua nafasi yake kwa lengo la kuimarisha na kukuza ustawi wa 
Zanzibar na watu wake.
Chanzo: zanzibariyetu.wordpress.com
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Post a Comment