Wagombea
wapigana vikumbo. Wakamata masafa ya redio na televisheni kusaka kura,
Ukawa, CCM wachuana kwa bendera, NEC yaingia kiwewe na amri ya kulinda
kura, Watanzania wenye asili ya Kiasia waanza kukimbia nchi
Wagombea urais wa Tanzania wakiwamo Edward
Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Dk. John
Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kila upande unatumia mbinu zake zote kuhakikisha kuwa unavuna kura
nyingi zaidi katika kipindi hiki ambacho ni siku sita tu zimebaki, sawa
na saa 144 kabla ya kupiga kura Jumapili ijayo ya Oktoba 25.
Nipashe imebaini kupitia uchunguzi wake kuwa hivi sasa, kambi za
Magufuli na Lowassa zimekuwa zikibadili mbinu kukamilisha kazi
walizoanza katika wiki ya mwisho ya Agosti. Kambi zote zimekuwa
zikipigana vikumbo huku na huko, sura mpya zikiongezwa katika kampeni
zao na pia vita nyingine imehamia katika kupigania masafa ya vituo vya
redio na televisheni katika kujitangaza.
Kadhalika, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwapo kwa vita kali ya
usimikaji wa bendera katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu
katikati ya maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Aidha, imebainika vilevile kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa
wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiondoka nchini na kwenda nje ya nchi
kusubiri uchaguzi upite, huku Tume ya Taifa ya Uchgauzi (NEC) ikikumbwa
na kiwewe juu ya namna ya kuelimisha umma kuhusiana na rai ya kuwataka
watu wote kurejea kwenye nyumba zao baada ya kupiga kura na siyo
kujiweka kwenye maeneo ya umbali wa mita 200 kutoka kwenye vituo vya
kupigia kura kama wanavyoelekezwa na baadhi ya wanasiasa, hasa wa
upinzani.
Hata hivyo, kadri siku zinavyokaribia, Magufuli na Lowassa
anayeungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NLD na NCCR-Mageuzi, ndiyo
wanaoonekana kuchuana kwa karibu kutokana na wingi wa watu wanaojitokeza
kwenye mikutano yao tangu kuanza kwa kampeni Agosti 21, 2015.
Mbali na Magufuli na Lowassa, wengine walio katika safari ya
kuwania kuingia Ikulu ili kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi
mkuu Jumapili ijayo ni Maximilian Lyimo wa TLP, Fahmy Dovutwa wa UPDP,
Anna Mghwira (ACT-Wazalengo), Chifu Lutasola Yemba (ADC), Hashimu Rungwe
(Chaumma) na Janken Kasambala wa NRA.
WAPIGANA VIKUMBO
Licha ya kuwapo kwa ratiba rasmi inayoratibiwa na NEC, bado Lowassa
na Magufuli wameonekana mara kadhaa wakipigana vikumbo katika baadhi ya
maeneo.
Kwa mfano, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa katika kampeni zao za
mikoa ya kaskazini mwa Tanzania, wote walikuwa wakifuatana kwa karibu
zaidi. Mmoja akipita siku ya kwanza na kutikisa kwa mkutano mzito,
mwingine alionekana kufika eneo hilo au la jirani katika siku inayofuata
na kufanya mkutano mkubwa zaidi katika namna inayoonekana ni kama
kufuta nyayo za mtangulizi wake. Hili lilionekana zaidi katika ziara za
Lowassa na Magufuli kwenye maeneo ya Babati, Monduli, Longido, Hanang,
Arusha Mjini, Moshi, Siha, Same na hata Vunjo.
MASAFA YA REDIO, TELEVISHENI
Katika saa hizo 144 zilizobaki, CCM na Ukawa wamekuwa wakichuana
kwa karibu katika kupata masafa ya kurusha matangazo yao kupitia vituo
vya televisheni na redio. Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa hivi sasa,
vituo vya redio na televisheni vimekuwa vikivuna fedha za kutosha
kutokana na vita hii ya aina yake baina ya timu ya Magufuli inayojinadi
kwa kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ na Lowassa inayojinasibu kwa kauli mbiu
ya ‘mabadiliko’.
Kwa mfano, Magufuli ana tangazo lake la televisheni lililoshiba kwa
ujumbe na ahadi kuhusu kuboresha huduma za jamii kabla ya kuomba kura,
sawa na Lowassa ambaye pia ana tangazo lake la kujipigia debe kali
kuwataka Watanzania wampigie kura nyingi za ndiyo ili alete mabadiliko
nchini. Na wote wawili wana matangazo kadhaa pia kwenye redio.
WACHUANA KUSIMIKA BENDERA
Vita ni vita, wahenga walinena. Hivi sasa, timu za kampeni za
Magufuli na Lowassa zinachuana pia katika kuweka mabango kwenye kuta za
majengo ya umma na kusimika bendera za vyama vyao katika maeneo yenye
mikusanyiko mikubwa ya watu na pia kwenye makutano ya barabara kuu.
Kwa mfano, katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, kunako mataa
yenye makutano ya barabara za Mandela na Morogoro, mashindano haya ya
bendera huonekana wazi. Hali hiyo ipo pia kwenye maeneo ya biashara kama
Mtaa wa Kongo, Manzese, Ubungo, Sinza Palestina na Kijiweni, Tandika na
Buguruni jijini Dar es Salaam; Makoroboi Mwanza na Soko la Matola
jijini Mbeya.
KIWEWE CHAIKUMBA NEC
Wakati vyama, hasa CCM na vile vinavyounda Ukawa vikihaha kutumia
kila mbinu kuhakikisha kuwa wagombea wao wanazoa kura nyingi baada ya
saa 144 kupita kuanzia leo, NEC iko katika kibarua cha aina yake
kuhakikisha kuwa watu hawakai karibu na vituo vya kupigia kura siku ya
uchaguzi na badala yake, wote wanarejea nyumbani ili kusubiri matokeo.
Kibarua hiki kwa NEC kimekuwa kizito kutokana na kile
kinachohubiriwa na viongozi wa Ukawa kwa wafuasi wao, kwamba kwa
vyovyote vile, wahakikishe hawarudi nyumbani na badala yake wanakaa
kuanzia mita 200 kutoka vituo vya kura ili kuhakikisha kile wanachodai
kuwa ni kulinda kura na mwishowe kuzuia mbinu za chama tawala kufanya
hila kupitia kauli maarufu ya ‘ushindi hata kwa bao la mkono’ aliyowahi
kukaririwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Vigogo wa
NEC, wakiwamo Mwenyekiti, Jaji mstaafu Damian Lubuva na pia Mkurugenzi
wa NEC, Kailima Ramadhani, wamekuwa wakisisitiza kuwa wananchi waondoke
na kurejea kwao baada ya kupiga kura kwani kazi ya kulinda kura zao
itafanywa na vyombo vya usalama, wakisisitiza kuwa jambo hilo ni muhimu
kuzingatiwa na atakayekaidi atachukuliwa hatua kwa vile kinyume chake,
kunaweza kuibua vurugu kwani uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuhusisha
wapiga kura wengi zaidi kulinganisha na chaguzi zilizopita.
WATANZANIA WENYE ASILI YA KIASIA
Katika kipindi hiki kifupi kilichobaki, Nipashe imebaini kuwa kuna
Watanzania kadhaa wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiondoka wao na hata
familia zao na kwenda nje ya nchi ili kupisha uchaguzi ufanyike.
Uchunguzi umebaini kuwa kati ya wale wanaoondoka, wengi wamekuwa
wakiingiwa hofu kutokana na ushindani mkali unaoonekana hivi sasa baina
ya wagombea wa CCM na Ukawa, tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi
zilizopita.
“Ushindani uliopo sasa ni mkali sana... hili kila mmoja
analitambua. Ndiyo maana baadhi ya Watanzania hawa (wenye asili ya
Kiasia), wamekuwa wakiondoka wao wenyewe na familia zao pia ili kupisha
uchaguzi,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kwa sharti la kutotajwa
jina.
AHADI, ILANI
Baada ya kutoa ahadi kemkem kila waendako huku pia wakijielekeza
katika ilani za vyama vyao, Lowassa na Magufuli wameongeza nguvu pia
katika kufafanua ni kwa namna gani watatimiza yote wanayoahidi.
Akiwa katika mkutano wake mmojawapo wa kampeni mkoani Mtwara,
Lowassa anayejivunia ahadi yake ya kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania
kuanzia chekechea hadi chuo chuo kikuu, aliwaeleza wapiga kura ni kwa
namna gani ahadi yake hiyo inaweza kutekelezeka kirahisi pindi dhamira
ikiwapo.
Maeneo mawili makuu ya mfano aliyoyataja kuwa ni chanzo cha mapato
ni matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo nchini kama za madini na gesi
ambazo aliahidi atazifuatilia kwa kuhakikisha kuwa serikali inapitia
upya mikataba yote iliyosainiwa ili kuhakikisha kuwa mwisho wa siku
inakuwa na manufaa kwa Watanzania na siyo kwa viongozi wachache
waliosaini mikataba hiyo.
Kadhalika, alisema kuwa serikali yake itazingatia nidhamu ya
matumizi ya kila kinachopatikana, ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya
magari ya kifahari kama Toyota Landcruiser (mashangingi) ili fedha
zitakazookolewa zielekezwe katika kutoa elimu bure kwa kila Mtanzania.
Kadhalika, Magufuli anayeahidi mabadiliko ya kweli kwa nia ya
kuneemesha Watanzania ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure hadi kidato
cha nne, kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila
kata, kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini na kugawa milioni 50
kwa kila kijiji na kila mtaa; anasema namna mojawapo ya kupata fedha za
kutekeleza ahadi zake hizo ni kuongeza mapato yatokanayo na kodi walau
mara mbili ya kiwango cha sasa na pia kubana mianya yote ya ufisadi na
rushwa serikalini, hasa kutokana na kile anachosema kuwa kwa muda mrefu,
‘mafisadi wamelelewa sana’ na kuwaumiza Watanzania kwa kiasi kikubwa.
SURA MPYA ZA KAMPENI
Kadri siku ya uchaguzi inavyokaribia, timu za kampeni za Magufuli
na Lowassa zimezidi kuimarishwa kwa kuongeza sura mpya kwenye mikutano
yao. Kwa mfano, mbali ya kuwa na kikosi chao cha watu 32, Magufuli
ameongeza nguvu katika timu yake ya kampeni kwa kuwahi kuwatumia
mawaziri wakuu wastaafu, Joseph Warioba na John Malecela. Kadhalika,
katika maeneo tofauti, marais wastraafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin
Mkapa wamekuwa wakitumiwa kuongeza nguvu.
Timu ya Lowassa imeendelea pia kutumia mbinu hii ya kuongeza sura
mpya. Hivi sasa, timu hii imeongezewa nguvu kubwa na aliyekuwa kada
mkongwe wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru na pia hivi karibuni
wamempata aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi
Juma Mwapachu. Hata hivyo, Mwapachu bado hajapanda jukwaani, ingawa
ameshawaambia waandishi wa habari kuwa mgombea pekee mwenye sifa ya kuwa
rais ajaye ni Lowassa.
CCM, UKAWA
Alipoulizwa kuhusu mikakati yao katika saa 144 zilizobaki kuanzia
leo, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hivi sasa mashambulizi
yao yataongezwa nguvu na timu mbalimbali ziatazokwenda kwenye kanda kumi
za Magharibi, Kati, Pemba, Unguja, Pwani, Kaskazini, Victoria,
Serengeti, Nyasa na Kusini.
“Tunakwenda kusambaza majeshi kila kona ya nchi. Tutashambulia kila
kanda, kwetu kila kanda ni kitovu cha mapambano... kila kanda kuna
vifaa vyote muhimu kama rasilimali watu na magari, tutafika maeneo yote
kwa wakati mmoja,” alisema.
Makene alisema kwa saa hizi ni sawa na kula ng’ombe na wanakwenda kumalizia mkia au kupondaponda kichwa cha adui.
“Kawaida watawala wanapokwenda kushindwa wanakunjua makucha yao, na
tunaona nchini kwa sasa wameanza kueneza hofu kwa Watanzania, watu
wanapigwa na kunyanyaswa, sisi tunaondoa hofu na kutoa elimu ya mpiga
kura kwa wananchi, wakati wao wanafanya hayo sisi tunawatia moyo
wananchi kuwa uchaguzi ni wao. Watumie haki yao ya msingi kuchagua
viongozi bora wa kuleta mabadiliko, ujumbe utapelekwa na timu hizo,”
alibainisha.
Alisema Lowassa amemalizia kampeni zake katika mikoa yote, baada ya
mkutano wa jana jijini Mbeya na sasa anakwenda kupiga kampeni kwenye
maeneo wanayoamini kuwa yana nafasi kubwa ya kuamua mshindi na pia hali
ya kisiasa kwa kila eneo nchini, kwa maana ya kuongeza nguvu kila
sehemu.
Kwa mujibu wa NEC, mikoa yenye wapiga kura wengi ambayo ni ngome
muhimu kwa ushindi wa chama chochote ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza,
Morogoro, Kagera, Tabora, Tanga, Dodoma na Arusha.
“Timu zote zitasambaa nchi nzima , tunatambua umuhimu wa kila eneo na ndiyo maana tumesambaza watu,” alisema.
Alipoulizwa jana kuhusiana na kampeni zao katika wiki hii iliyobaki
kabla ya uchaguzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CCM, Godfrey Chongolo,
alisema atafutwe Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba au
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Makamba alipotafutwa, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa
na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms), pia hakujibu hadi
tunakwenda mitamboni.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment