Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Na Beatrice Shayo
Kadhalika, imeelezwa kuwa maamuzi mbalimbali ya kisiasa ndiyo
yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa mgawo wa umeme na kusababisha
kero kwa watumiaji wake huku pia shughuli za kiuchumi zikiathiriwa kwa
kiasi kikubwa.
Nipashe inatambua kuwa kabla ya kuwapo kwa mitambo mipya ya
kuzalisha umeme itokanayo na utekelezaji wa miradi mbalimbali, Taifa
lilikuwa likitegemea vyanzo vikuu vitatu vya nishati hiyo, ambavyo kwa
ujumla wake vilikuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 1,226. Vyanzo hivyo
vitatu ni umeme utokanao na maji uliokuwa ukichangia asilimia 45.8 kwa
kutoa Megawati 561; Megawati 435, sawa na asilimia 35.9 kutoka umeme wa
gesi na chanzo kingine ni cha mafuta, chenye Megawati 230 (asilimia
18.8) ya umeme wote unaozalishwa nchini.
Katika taarifa yake kwa umma ambayo Nipashe inayo nakala yake,
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco inaeleza kwa kina juu ya hali halisi
ya upatikanaji wa umeme nchini, ikisema kuwa inafanya hivyo kwa nia ya
kuondoa minong’ono, uzushi na kuwapo kwa taarifa nyingi za kubuni, hasa
kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo inafichua ukweli kuwa kwa ujumla, uzalishaji wa
nishati hiyo katika mabwawa yote nchini ni wa kiwango cha chini ya
asilimia 20, huku hali ikiwa mbaya zaidi katika Bwawa la Mtera ambalo
hivi sasa halizalishi kabisa. Kadhalika, hali siyo nzuri katika vyanzo
vingine vya kuzalisha umeme vya gesi na mafuta.
UMEME WA MAJI
Inaelezwa kuwa hivi sasa, mabwawa karibu yote yanayotegemewa
kuzalisha umeme wa maji yamekuwa hayazalishi ipasavyo kwa sababu ya
kukosekana kwa maji na kwamba, baadhi ya mabwawa hayo hivi sasa
yanaelekea kukauka.
Kwa ujumla wake, taarifa hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha juu cha
uzalishaji wa umeme kinachotarajiwa kutokana na mabwawa sita ya Mtera,
Kidatu, Pangani, Nyumba ya Mungu, Hale na Kihansi ni Megawati 561.
Hata hivyo, hadi kufikia Oktoba 4, mwaka huu, uzalishaji wa umeme
katika mabwawa hayo yote ulikuwa ni Megawati 105 (asilimia 18.7) ya
kiwango kinachotarajiwa.
“Kwa lugha sahihi, uzalishaji umeme katika mabwawa ya maji umeshuka
kwa 81.3%,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa Tanesco.
Taarifa inafafanua kwa kina hali ya uzalishaji katika kila bwawa,
ikieleza kuwa Mtera lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 80, hivi sasa
halizalishi kabisa kutokana na maji yake kupungua hadi kiwango cha
mwisho kinachotakiwa kuzalisha nishati hiyo.
Bwawa la Kidatu linaloongoza kwa kuzalisha umeme mwingi
kulinganisha na mengine wa Megawati 204, hivi sasa limepungukiwa maji
kiasi cha kuzalisha Megawati 27 tu (asilimia 13.2) ya uwezo wake wa juu.
Katika Bwawa la Kihansi lenye uwezo wa juu wa kuzalisha Megawati
180, uzalishaji wake hivi sasa umeshuka hadi Megawati 51.5 (asilimia
28.6) tu ya uwezo wake.
Upungufu wa maji umelikumba pia Bwawa la Nyumba ya Mungu lenye
uwezo wa juu wa kuzalisha Megawati 8, lakini bado linazalisha Megawati
5.5 tu (asilimia 68.8) ya uwezo wake wa juu; Bwawa la Hale lenye uwezo
wa kuzalisha Megawati 21 hivi sasa linazalisha Megawati 4 (asilimia 19)
na maporomoko ya maji ya Pangani (New Pangani Falls) yenye uwezo wa
kuzalisha Megawati 68, yameathiriwa na kupungua kwa kiwango cha maji
hadi kuzalisha Megawati 17 tu (asilimia 25).
UMEME WA GESI
Baada ya kuporomoka kwa kiwaango cha uzalishaji wa umeme utokanao
na chanzo cha maji, ilitarajiwa kuwa vyanzo vingine kama uzalishaji wa
nishati hiyo unaotegemea gesi kuokoa jahazi.
Hata hivyo, taarifa inafichua kuwa hadi sasa, Tanesco inashindwa
kupata ahueni inayotarajiwa kutoka katika chanzo hiki kutokana na kile
kinachoelezwa kuwa ni hatua ya wazalishaji wa gesi ya Songosongo
inayotoa umeme huo, kampuni ya Pan Africa, kushindwa kutoa kiwango
kinachotakiwa cha Megawati 340 kilichokuwa kikizalishwa awali na sasa
kuzalisha Megawati 260 tu (asilimia 76.5).
Tanesco wanaeleza katika taarifa yao kuwa hivi sasa, wazalishaji
hao wa umeme wa gesi (Pan Africa), wamewaambia kuwa wanaboresha visima
vyao na kazi hiyo ikikamilika uzalishaji utaongezeka.
“Japo ukarabati huo utatuhakikishia gesi zaidi baadaye, lakini
wakati huu wa matengenezo panakuwa na uhaba wa gesi kutoka Songosongo,”
inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
UMEME WA MAFUTA
Taarifa ya Tanesco inafichua vilevile ukweli mchungu kuwa
uzalishaji wa umeme kwa mitambo ya mafuta umeshuka pia, kutoka kiasi cha
Megawati 230 kilichokuwa kikipatikana awali hadi kufikia Megawati 190
(asilimia 82.6). Hata hivyo, haielezwi ni kwa nini uzalishaji wa umeme
wa mafuta umeshuka kwa kiwango hicho.
UZALISHAJI BOMBA JIPYA LA GESI
Inaelezwa katika tarifa ya Tanesco kuwa zipo jitihada kadhaa
zinazofanywa kuhakikisha kuwa bomba jipya la gesi lililowashwa
linazalisha umeme kwa kiwango kinachotarajiwa. Inaelezwa kuwa hivi sasa
mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi ya bomba jipya iliyowashwa ni
Megawati 90 na mwingine wa Megawati 35.
Taarifa inafafanua zaidi kuwa mitambo mingine inayotarajiwa
kuongeza uzalishaji wa umeme ndani ya wiki moja hadi mbili ni Symbion
(Megawati 20), Ubungo II (Megawati 35), Songas (Megawati 20) na
Kinyerezi Megawati 70.
Inaelezwa mwisho wa siku, matarajio ni kuona kuwa uzalishaji wa
mitambo mipya ikiwamo miwili ya Kinyerezi inaihakikishia Tanesco
Megawati 305 zaidi ya umeme unaopatikana sasa na ndipo kutakapokuwa na
uhakika wa kueleza kuwa tatizo la umeme nchini limemalizika.
Kadhalika, taarifa ya Tanesco inaeleza sababu za kutoa taarifa zenye matumaini ambazo nyingine zimetofautiana na uhalisia.
“Ni muhimu pia Watanzania watuelewe kwamba kila kitu hakiko katika
uwezo wetu. Hii ni kwa sababu baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme na
pia mifumo ya gesi siyo ya kwetu na inamilikiwa na watu wengine.
Hivyo taarifa tulizokuwa tunazipokea kutoka kwa makampuni haya
ndizo tumekuwa tukiwapatia wateja wetu na bahati mbaya baadhi yake
hazikuwa kama tulivyokuwa tumeelezwa,” sehemu ya taarifa ya Tanesco
inaeleza.
Mbali na mitambo ya Tanesco, umeme unaopatikana kwa sasa unatoka
kwa kampuni za Songas, Symbion, Aggreko na IPTL huku mfumo wa gesi
unahusisha kampuni za Pan Africa Energy, TPDC na M&P.
WASOMI WAZUNGUMZIA TATIZO LA UMEME
Dk. Donath Olomi wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali, anasema
matatizo ya umeme yaliyopo sasa ni matokeo ya usimamizi mbovu, hasa
kwenye suala la mikataba kwani haiko wazi.
Alisema kuna athari kubwa katika mgawo huo na ushahidi ni Tanesco
kupata hasara ya Sh. milioni 500 kwa siku kutokana na kukosa mapato.
Pia, alisema athari nyingine ni kwa wenye viwanda ambao sasa hujiendesha
kwa gharama kubwa kwa kutumia majenereta huku viwanda vingine
vikilazimika kusimamisha uzalishaji.
Alisema njia mojawapo ya kuondokana na matatizo ya kupatikana kwa
umeme wa uhakika ni kuipunguzia Tanesco baadhi ya majukumu iliyo nayo
sasa.
Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa
Tolly Mbwete, alisema Tanesco inatakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana
na tatizo la kukatika kwa umeme.
“Walisema kuna mitambo ya gesi inatengenezwa na imemalizika... sasa
inakuwaje kuna mgawo na ni kwa nini wanakaa kimya hadi wanasiasa
wanaliingilia,” alisema Profesa Mbwete.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi, alisema
kukosekana kwa umeme wa uhakika nchini kutaleta madhara makubwa kiuchumi
ikiwa ni pamoja na kutovutia wawekezaji wa uhakika wa ndani na nje ya
nchi.
Alisema hata sasa wawekezaji wengi wamekuwa wakilalamikia
kukosekana kwa nishati yenye uhakika na hivyo, suala hilo linapaswa
kutafutiwa suluhisho la kudumu.
Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda
nchini (CTI), Hussein Kamota, alisema ni wazi kwamba kuna hasara kubwa
imepatikana kwa wanachama wao na kwamba, wanafanya tathmini na taarifa
yao wataitoa kwa umma kesho.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment