Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo. |
NA DANIEL MKATE
Jeshi la Polisi jijini Mwanza, jana lilitumia nguvu ndani ya Hospitali
ya Rufaa Bugando baada ya kuvurumisha mabomu ya kutoa machozi 12 kwa
lengo la kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Tukio hilo lililotokea jana saa 11:30 jioni, liliibuka baada ya baadhi
ya viongozi wa Chadema kuzungumza na wafuasi wao waliokwenda
kuusindikiza mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita,
Mawazo Alphonce, kwa ajili ya hifadhi.
Hata hivyo, licha ya hospitali hiyo kumilikiwa na Baraza la Maaskofu
nchini (Tec), polisi hawakuonea huruma wagonjwa waliolazwa ndani yake
na kuamua kuvurumisha mabomu hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, mgombea ubunge wa
Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, aliwataka wafuasi wa chama hicho
kukutana ofisi za kanda za chama hicho jijini Mwanza ili kuzungumzia
tukio hilo.
“Hapa ni chumba cha kuhifadhi maiti, hivyo tukutane katika ofisi za
kanda ambako tumeweka msiba wa kamanda wetu …tukusanyike hapo wote kwani
viongozi wetu waliopo Dar es Salaam na Dodoma wanakutana kwa ajili ya
tukio hili…hapa hatupo kwa ajili ya kukuna nazi,” alisema Lema.
Alisema hawatakaa vikao vya kuwafundisha wafuasi wao ujinga, bali vikao watakavyokaa ni vya kutiana ujasiri.
Wafuasi hao walianza kupigwa mabomu baada ya kusemekana askari polisi
mmoja kuingia katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo kwa
madai alitaka kuuchukua mwili wa Mwenyekiti huyo na kuutorosha. Askari
huyo alianza kushambuliwa na wafuasi hao ambao walioonekana kuwa na
hasira za majonzi za kuuliwa mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo alishambuliwa na watu wasiojulikana juzi saa 6:00 mchana
kwa kukatwa mapanga na shoka kichwani na sehemu mbalimbali za mwili
wake na kumsababishia umauti.
Mawazo ambaye pia alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda mkoani Geita, atazikwa baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.
Alishambuliwa kijijini Katoro wakati akiwa katika bodaboda akielekea kata ya Ludete.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo,
alipotakiwa na Nipashe kuzungumzia tukio hilo, alitaka apigiwe baadaye,
lakini hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, hakupatikana.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment