Ni ile ya shule za msingi, sekondari, Darasa la kwanza walizwa kila kona.
Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza kwenye mikutano yake ya kampeni wakati akipeperusha
bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya urais kabla ya
kuibuka mshindi, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake
itahakikisha kuwa inatoa elimu bure kwa kila Mtanzania kuanzia elimu ya
msingi hadi kidato cha nne, huku akisisitiza kuwa anaposema bure
anamaanisha ni bure kweli bila kuwapo na rundo la michango
inayowasababishia kero wananchi na kujikuta wakiichukia serikali yao.
Kadhalika, siku moja tu baada ya Magufuli kuingia madarakani
kufuatia ushindi wake wa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa,
Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu alitoa taarifa iliyoonyesha kuwa kuna
maelekezo maalum yametolewa kwa watendaji kuhakikisha kuwa ahadi ya Rais
kuhusiana na elimu bure inatekelezwa mara moja kuanzia Januari mwakani.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alikiri kupokea malalamiko ya wazazi
kuwa baadhi ya shule jijini Dar es Salaam zinawatoza michango wazazi na
kusema kuwa jambo hilo ni kosa na walimu watakaothibitika watachukuliwa
hatua.
Alitoa taarifa wiki iliyopita inayowataka wakuu wa shule kuacha
kuwatoza michango wazazi, kuanzia darasa la kwanza zikiwamo zilizoanza
uandikishaji, lengo likiwa ni kutimiza ahadi ya Rais ya kuhakikisha kuwa
elimu inatolewa bure.
“Hao walimu wanaopinga agizo hilo (la kufuta michango) ni kina nani na fedha hizo zinaingia katika akaunti gani?
Nitawachukulia hatua wote watakaohusika kwani michango hii ni kero
kwa wazazi,” Sagini alikaririwa pia akisema katika taarifa iliyosambazwa
mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, pamoja na nia hiyo nzuri ya serikali, uchunguzi
uliofanywa na Nipashe katika maeneo mbalimbali umebaini kuwa ipo kazi
kubwa kuhakikisha kuwa jambo hilo linatekelezwa kwa dhati.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa hadi sasa, tayari kuna
shule kadhaa zinazoendelea kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza
kwa kuwatoza michango mbalimbali licha ya ukweli kuwa watoto hao
wataanza shule Januari, 2016 -- kipindi ambacho Rais Magufuli ameamuru
kuwa elimu iwe bure hadi kidato cha nne na michango ni marufuku.
Baadhi ya shule hazijaanza uandikishaji, lakini Nipashe imebaini
kuwa wazazi wanaofika kwenye shule hizo ili kuulizia utaratibu wa
kuandikisha watoto wa darasa la kwanza, hutakiwa kujiandaa kwa michango
mbalimbali ikiwamo ya nembo, ulinzi, uji, T-shirt na pia masomo ya
ziada.
MANISPAA KINONDONI
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa michango inaendelea kuhimizwa
kwa wazazi wanaoulizia utaratibu wa kuandikisha watoto wao darasa la
kwanza katika baadhi ya shule za manispaa hiyo.
Katika Shule ya Msingi Mwenge, Nipashe ilikuta baadhi ya michango
inayotajwa kwa wanafunzi wa darasa la kwanza kuwa ni pamoja na nembo ya
shule Sh 2,000, T-shirt za shule Sh. 8,000, uji kwa siku Sh. 500, masomo
ya ziada kwa siku Sh. 400 na mchango kwa ajili ya ripoti ni Sh. 1,000
kwa muhula.
Katika Shule ya Msingi Ally Hassan Mwinyi iliyopo Magomeni,
michango inayotajwa ni pamoja na Sh. 23,000 kwa ajili ya T-shirt, nembo,
fomu ya kujiunga na fagio. Na kwa mwanafunzi mpya anayehamia katika
shule hiyo baada ya kufanyiwa mahojiano maalum, kiwango cha michango
huwa ni Sh. 67,000 na kati yake, Sh. 50,000 ni kwa ajili ya madawati na
kiasi kinachobaki ni kwa ajili ya michango mingine ikiwamo ya nembo,
fulana na fomu ya kujiunga.
Katika Shule ya Msingi Gilman Ruthinda, michango inayotajwa ni Sh.
30,000, ambayo huhusisha pia ulinzi na maji, achilia mbali uji Sh. 200
kwa siku na masomo ya ziada Sh 300 kwa siku.
Inaelezwa kuwa taarifa za kuwapo kwa michango zipo pia katika shule
za msingi Mburahati, Barafu, Kigogo, Msasani, Saranga, Temboni, Kwembe.
Jitihada kumpata Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuzungumzia
suala la michango katika manispaa yao zilishindikana kwani mwandishi
alipofika ofisini kwake alielezwa kuwa hayupo na simu yake ya mkononi
iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi bado hakujibu.
MANISPAA YA ILALA
Taarifa za kuwapo kwa michango zimepamba moto pia katika baadhi ya
shule za manispaa ya Ilala, ambazo baadhi waandishi wa Nipashe
walizitembelea na kujitambulisha kuwa ni wazazi wanaohitaji kupewa
utaratibu juu ya namna ya kuandikisha watoto wao wa darasa la kwanza.
Ilibainika kuwa katika Shule ya Msingi Tabata Mtambani, wazazi
hutakiwa kulipa Sh. 3,000 ya daftari la ripoti kwa mwaka, ulinzi Sh
3,000, uji Sh. 3,00 kwa siku na pia masomo ya ziada Sh. 300 kwa siku.
Shule nyingine jirani ya Tabata Jica pia wazazi hutakiwa kutoa michango
kadhaa ikiwamo Sh. 300 ya masomo ya ziada kwa siku.
Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alisema suala
hilo linaweza kuelezewa vizuri na Afisa Elimu ya Msingi wa manispaa yao,
ambaye hata hivyo hakuwapo kwani alikuwa kwenye semina elekezi ya
mitihani ya taifa ya darasa la nne.
MANISPAA YA TEMEKE
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa baadhi ya shule zinazotoza
michango kwa ajili ya uandikishaji darasa la kwanza ni pamoja na
Mabatini iliyopo Tandika. Mzazi hutakiwa achangie jumla ya Sh. 25,000,
mchanganuo wake ukionyesha kuwa ni pamoja na uzio, ulinzi, lebo, uji na
masomo ya ziada.
Aidha, katika Shule ya Msingi Veterinary iliyopo kwenye manispaa
hiyo ya Temeke, michango inayotajwa kuwa hutakiwa kwa wanafunzi
wanaoandikishwa darasa la kwanza ni pamoja na nembo ya shule Sh. 6,000,
madawati Sh. 3,000 kwa mwaka, ulinzi Sh. 3,000 pamoja na Sh. 300 ya uji
kwa siku.
Hata hivyo, uandikishaji shuleni hapo ulitarajiwa kuanza wiki hii baada ya kikao kati ya kamati ya shule yao na wazazi.
Afisa Elimu ya Msingi wa Manispaa ya Temeke, Salum Upunda, alisema
hadi sasa bado hajapokea waraka na kueleza kwamba michango inayotozwa ni
makubaliano kati ya wazazi na kamati za shule.
MTWARA
Katika mkoa wa Mtwara, shule nyingi za msingi uandikishaji rasmi
ulikuwa haujaanza kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo,
baadhi ya wazazi waliiambia Nipashe kuwa walipofuatilia kutaka kujua
utaratibu wa uandikishaji kwa darasa la kwanza utakuwaje, waliambiwa
wajiandae kwa michango kwani bado hakuna waraka wowote uliotumwa na
serikali kuelezea suala hilo.
Mmoja wa walimu waliozungumza na Nipashe alisema kuwa michango
hutofautina kati ya shule moja na nyingine, na kwamba baadhi hutoza hadi
Sh. 15,000.
Hata hivyo, Afisa Elimu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya
Mtwara Vijijini, Tamimu Kambona, alisema wamejiandaa kufuta michango
kama ilivyoagizwa na wazazi wasiwe na hofu kwani watatekeleza jambo hilo
kwa asilimia mia moja.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkubiru wilayani Mtwara Vijijini
alisema hadi sasa hawajapata waraka lakini wamejipanga kutochukua
michango kwa wazazi wanaofikisha watoto wao kuwaandikisha darasa la
kwanza.
Januari mwaka huu, shule hiyo ilichangisha Sh. 7,700 kutoka kwa
kila mzazi wa mwanafunzi aliyeandikishwa darasa la kwanza, baadhi ya
michango hiyo ikiwa ni ulinzi na T-Shirt.
MBEYA
Katika maeneo mengi mkoani Mbeya, uandikishaji bado haujaanza huku
baadhi ya walimu wakuu wakidai jukumu la kuandikisha wanafunzi wa darasa
la kwanza ni la maofisa watendaji wa mitaa na kata. Hata hivyo,
wanafunzi walioandikishwa mwanzoni mwa mwaka huu walikuwa wakichangishwa
fedha kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwamo ulinzi, madawati na maji.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Itigi, Tomath Mwilenga, alisema
kuwa michango yote ilikuwa ikipitishwa katika vikao vinavyoshirikisha
wazazi na kwamba, anaamini mwaka huu hakutakuwa na michango. Katika
Shule ya Msingi Maendeleo, mwaka huu wazazi walichangishwa Sh. 6,000
ikiwa ni michango ya ulinzi, maji na ukarabati wa vifaa vya shule.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isanga, Kanjoka Hashim, alisema
kuwa anachofahamu ni kwamba agizo la Serikali linataka uandikishwaji wa
wanafunzi ufanyike bure na kwamba hivi sasa wanasubiri maelekezo ya
rasmi kwa maandishi ili waanze utekelezaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, alisema
uandikishaji wanafunzi wa darasa la kwanza utaanza Desemba na
hawatarajii kuchangisha wazazi bali kutii maelekezo ya mkuu wa nchi.
DODOMA
Katika shule mbalimbali za Manispaa ya Dodoma, kuna taarifa pia za
kuwapo kwa michango kwa wazazi wanaopeleka watoto wao ili kuandikishwa
darasa la kwanza. Uchunguzi umebaini kuwa katika Shule ya Msingi
Kaloleni, wazazi hutakiwa kuchangia Sh. 5,000, Shule ya Msingi Mlimwa C
hutozwa Sh. 10,000, Shule ya Msingi Kizota Sh. 5,000, Shule ya Msingi
Nkuhungu Sh. 6,000 na Shule ya Msingi Chamwino A Sh. 5,000 kwa kila
mtoto. Michango hiyo huwa ni pamoja na ulinzi, maji na ukarabati wa
madawati.
MICHANGO SEKONDARI
Mbali na kuwapo kwa michango katika shule za msingi, imebainika
kuwa bado kuna utitiri wa michango katika shule za sekondari kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha sita ambayo hulalamikiwa na wazazi kuwa
inaondoa uhalisia wa dhana ya utoaji wa elimu bure kwa shule za msingi
na ada nafuu ya Sh. 20,000 inayotozwa kwa shule za sekondari za kutwa
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Nipashe imebainbi kuwa katika Shule ya Sekondari ya Kambangwa
iliyopo kwenye Manispaa ya Kinondoni, wanafunzi wa kidato cha kwanza
walipoingia mwaka huu walichangishwa michango iliyofikia Sh. 160,000,
huku kidato cha kwanza wakichangia Sh 110,000, kidato cha tatu Sh.
83,000 na kidato cha nne Sh. 145,000.
Kadhalika, ingawa sekondari kidato cha tano na cha sita siyo sehemu
ya ahadi ya elimu bure iliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa kampeni,
lakini Nipashe imebaini kuwa nako kuna rundo la michango inayoumiza
wananchi kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano, wanafunzi walio kidato cha tano hivi sasa katika shule
ya sekondari Tambaza iliyopo katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es
Salaam, walichangishwa michango zaidi ya 10 iliyokuwa na thamani ya Sh.
240,000 wakati wakisajiliwa shuleni hapo katikati ya mwaka huu.
Mchanganuo wa michango hiyo ni Vifaa vya usafi na karatasi Sh. 100,000,
madawati 15,000, maendeleo 15,000, taaluma 10,000,
masomo ya ziada 30,000, mitihani ya kila mwezi 30,000, tahadhari 5,000,
kitambulisho 5,000, ulinzi 5,000, nembo ya shule 2,000, usafi wa vyoo
3,000, matibabu 5,000, mahafali 10,000 na kijiji cha michezo Sh. 5,000.
“Serikali ya Rais Magufuli inapasw akufanya kazi ya ziada kukomesha
michango hii mara moja ili kusiwe na wajanja wachache wanaotumia
visingizio mbalimbali kuendelea kuikusanya … vinginevyo dhamira ya Rais
Magufuli kutoa elimu bure hadi kidato cha nne inaweza kukwama,” alisema
mmoja wa wazazi waliozungumza na Nipashe.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam aitwaye Mohamed Khalfan, ambaye
huendesha taasisi inayofadhili makumi ya watoto yatima wanaosoma katika
shule mbalimbali nchini, alisema serikali inapaswa kukomesha michango ya
uandikishaji wa watoto wa darasa la kwanza mara moja kwani kutofanya
hivyo kunawaathiri watoto wengi wanaopaswa kuwapo shuleni, wakiwamo
yatima anaowasaidia yeye.
“Jambo hili linatukwaza hata sisi tunaojitolea kusaidia yatima.
Kuna walimu wa shule mbili za msingi kule Temeke wametuambia watoto
hawawezi kaundikishwa hadi walipe michango yao ambayo ni Sh. 15,000 na
Sh. 30,000… hili jambo siyo zuri na serikali inapaswa kuingilia mara
moja ili kuokoa watoto wetu,” alisema Khlafan aliyezungumza na Nipashe
kwa njia ya simu jana.
UFAFANUZI ZAIDI WA TAMISEMI
Akifafanua zaidi kuhusu zuio la michango kuanzia shule za msingi
hadi sekondari, Sagini aliiambia Nipashe kuwa walimu wanaoendelea
kuchukua michango kwa wazazi wanakiuka maagizo ya Rais yanayotaka
kufutwa kwa michango hiyo ili elimu iwe bure kweli na hivyo ikithibitika
hatua kali zitachukuliwa.
“Nisaideni majina ya shule hata namba na majina ya walimu
wanaoendesha kazi hiyo, wazazi waliochangia na kiasi chao walichotoa
nami nitachukua hatua ili iwe fundisho kwa walimu na shule nyingine
zenye tabia hiyo,” alisema Sagini.
Sagini aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutumia
sehemu ya mapato wanayokusanya kwa ajili ya kuwekeza katika shule ili
kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kutoa elimu bure.
“Manispaa nyingi mapato ya kodi yanayotokana na kodi ya wananchi na
imeongezeka ikiwamo Manispaa ya Kinondoni ambayo awali ilikuwa
ikikusanya Sh. bilioni 16 lakini sasa imefikia bilioni 37… hivyo ni
vyema wakurugenzi wakatumia busara kutekeleza agizo la Dk. Magufuli kwa
kutoa kiasi cha fedha kulipa gharama katika shule hizo,” alisema Sagini.
Alisema ameshapokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kuna baadhi
ya shule jijini Dar es Salaam wazazi wanapoenda kuandikisha watoto wa
darasa la kwanza hutozwa fedha ili watoto waandikishwe, jambo ambalo
ni kinyume cha maelekezo.
“Sielewi ni kwa nini maafisa elimu wa wilaya hamuwachukulii hatua
walimu wakuu wenye viburi ambao wanakiuka agizo la Mhe. Rais linalosema
elimu ya msingi hadi sekondari ni bure.
“Hao walimu wanaopinga agizo hilo ni kina nani na fedha hizo
zinaingia katika akaunti gani? Nitawachukulia hatua wote watakaohusika
kwani michango hii ni kero kwa wazazi,” alisisitiza Sagini katika
sehemu ya taarifa iliyosambazwa mwishoni mwa wiki kuelezea suala hilo.
*Imeandikwa na Efracia Massawe, Hussein Ndubikile, Gwamaka Alipipi,
Augusta Njoji, Emmanuel Lengwa, Mary Geofrey, Juma Mohamed, Nebart
Msokwa.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment