>Wabunge washtukia figisufigisu ya mgombea kubebwa
>Ndugai apita bila kupingwa, Ukawa wamteua Medeye
NA WAANDISHI WETU, DODOMA
BAADA ya jana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpitisha aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 10, Job Ndugai, kuwania kiti cha uspika, vita kubwa inaonekana kuanza katika nafasi ya Naibu Spika.
Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa, zinasema kuwa katika nafasi hiyo, baadhi ya vigogo wa Serikali wanataka Dk. Tulia Akson, mbunge aliyeteuliwa jana na Rais Dk. John Magufuli, ashike wadhifa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wanaomuunga mkono Dk. Tulia, aliyejitoa dakika za mwisho kuwania uspika kupitia chama hicho jana, wanaamini akiwa Naibu Spika, atakuwa msaada mkubwa kwa Serikali pindi atakapokuwa akiliongoza Bunge kwa kuwa kitaaluma ni mwanasheria.
Dk. Tulia, kabla ya kuteliwa jana na Rais Magufuli kuwa mbunge, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wakati Dk. Tulia akiungwa mkono na vigogo hao, taarifa zinasema idadi kubwa ya wabunge wateule wa CCM wanamtaka Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, achukue nafasi hiyo kwa kuwa wanaamini ana uwezo wa kuongoza Bunge.
Kigezo kikubwa kinachowafanya wabunge hao wamuunge mkono Zungu, ni uzoefu wake bungeni pamoja na umahiri wake aliouonyesha wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Bunge la 10.
Kutokana na uwapo wa makundi hayo, taarifa hizo zinasema hivi sasa wabunge wa CCM wamegawanyika kwa kuwa wengine wanaonekana kuwa na msimamo tofauti na viongozi wa Serikali ya chama chao.
Pamoja na uwapo wa taarifa hizo, Katibu wa Wabunge wa CCM ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge katika Serikali ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Jenista Mhagama, alipozungumza jana na MTANZANIA kwa simu juu ya waliochukua fomu kuwania unaibu Spika kwa upande wa chama hicho, alimtaka mwandishi wetu avumilie hadi leo kwa kuwa ndiyo mwisho wa kuchukua fomu.
“Kwa sasa niko kwenye kikao, siwezi kusema chochote unachotaka kuniuliza. Nakuomba uvumilie hadi kesho (leo) kwa sababu ndiyo utakuwa mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu, tafadhali vuta subira,” alisema Mhagama.
Pamoja na kutotaka kuzungumzia suala hilo, taarifa zilizopatikana zinasema hadi jana jioni, jumla ya wanachama saba wa CCM walikuwa wameshachukua fomu kuwania unaibu Spika wakiwamo Dk. Tulia na Zungu.
Wakati huo huo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, aliwaambia waandishi wa habari, kwamba ofisi yake imepokea majina manane ya wagombea uspika kutoka katika vyama vinane.
Aliwataja wagombea hao na majina ya vyama vyao kwenye mabano kuwa ni Peter Salungi (AFP), Hassan Almas (NRA), Dk. Godfrey Malisa (CCK), Job Ndugai (CCM), Gudluck ole Medeye (Chadema), Richard Lyimo (TLP), Hashim Rungwe (Chauma) na Alexander Kasinini wa DP.
“Hayo ndiyo majina niliyoyapokea ya wanaowania uspika. Pamoja na hayo, kwa ujumla maandalizi ya kuanza kwa vikao vya Bunge la 11 linalotarajia kuanza kesho (leo), yako vizuri kwani hadi sasa waliokwishajisajili ni wabunge 348.
“Taratibu za ukumbi wa Bunge nazo zimekamilika na kazi ya kwanza kesho itakuwa ni kuchaguliwa kwa spika na baadaye ataapishwa kwa ajili ya kuanza kuliongoza Bunge ikiwa ni pamoja na kuwaapisha wabunge wengine,” alisema Dk. Kashililah.
Wakati hayo yakiendelea, Ofisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), pamoja na kumpitisha Medeye kuwania uspika, wamempitisha Mbunge wa Kaliua ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, kuwania unaibu Spika.
ZITTO AHOJI
Kutokana na kile kinachoonekana ni figisufigisu za uspika na unaibu wake, Mbunge mteule wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alishangazwa na hatua ya viongozi wa Serikali kuandaa Spika au naibu wake kwa kile alichokiita kutoka mfukoni.
Alisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hakuwahi kujaribu kuleta Spika wake au Naibu Spika wake mfukoni.
“Alipomteua Chifu Adam Sapi Mkwawa kuwa waziri, alifanyiwa ‘rebellion’ na wabunge (wakati wa chama kimoja) akamrudisha mpaka alipostaafu tena kwa kumtungia sheria ya ustaafu (wakati wa Mwinyi).
“Unapoona rais anajaribu ku-‘impose’ kiongozi wa Bunge anayemtaka, mjue huko mbele Bunge litafanywa kibogoyo. Kwa mfano, hakuna Naibu Spika yeyote katika nchi hii ambaye hakuwahi kuwa mbunge wa jimbo.
Nawakumbusha tu kwamba, Bunge huendeshwa kwa kutumia katiba, sheria, kanuni na desturi au maamuzi yaliyokwishafanywa,” alisema Zitto kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.
NDUGAI APITA BILA KUPINGWA
Wabunge wa CCM, jana wamempitisha kwa kauli moja aliyekuwa Ndugai, kuwa mgombea wa nafasi ya uspika.
Ndugai alipitishwa baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC), kukutana mjini Dodoma juzi na kupitisha majina matatu ya wana CCM waliokuwa na sifa za kuwania nafasi hiyo.
Mbali na Ndugai, wengine waliopitishwa na CC kati ya wanachama 22 waliochukua fomu ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia na Abdullah Ally Mwinyi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha uchaguzi jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema Ndugai alipitishwa kwa kauli moja baada ya Dk. Tulia na Mwinyi kujitoa.
“Dk. Tulia na Mwinyi waliamua kujitoa ili kumwachia Ndugai, hivyo wabunge wa CCM wamempitisha Ndugai kwa kauli moja kuwa mgombea wa uspika. Jina la Ndugai litapelekwa kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya uteuzi, tunamuamini ni mgombea sahihi atalimudu Bunge,” alisema Nape.
Pamoja na hayo, alisema CCM wana uhakika mgombea huyo atashinda kwa kuwa wabunge wa chama hicho ni asilimia 74.8 ya wabunge wote.
NDUGAI ANENA
Kwa upande wake, Ndugai, aliwataka Watanzania watarajie mabadiliko tofauti na mabunge yote yaliyopita.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya jina lake kupitishwa, ambapo alisema Bunge la 11 lina vijana wengi wasomi kuliko mabunge yote yaliyowahi kutokea na lina uwakilishi mkubwa.
“Sasa ni kazi tu! Bunge hili lina wabunge wengi vijana, lina wabunge wengi wasomi zaidi kuliko mabunge yote yaliyowahi kutokea na lina uwakilishi mkubwa. Hili pia ni Bunge ambalo litakuwa na changamoto nyingi, tutegemee migomo ya hapa na pale, hata hivyo ubora wa kazi utakuwa ni mkubwa.
“Nitatenda haki, hakutakuwa na ubaguzi, kila chama kitatendewa haki, kwahiyo, nawaomba wabunge wote wakiwamo wa upinzani, waniunge mkono ili niwe Spika wa Bunge la 11,” alisema Ndugai.
Pamoja na hali hiyo, Ndugai, aliahidi kusimamia Bunge inavyotakiwa kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha kupitia nafasi ya unaibu spika aliyokuwa akiishikilia kwa muda mrefu.
KINANA AWAFUNDA WABUNGE
Awali akifungua mkutano wa uchaguzi, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwaeleza wabunge wateule wa chama hicho, kwamba wana kazi moja ya kujipanga kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
“CCM itakuwa nanyi kuhakikisha mnafanikiwa katika kutekeleza majukumu yenu, kwa sasa kazi kubwa ya kisiasa inahamia bungeni, sisi tuna matumaini na nyie bungeni na majimboni.
“Baada ya Bunge hili kuahirishwa, ofisi yangu itaandaa utaratibu wa kuwaita wabunge wote wa chama chetu kwa ajili ya kupanga mikakati ya kazi na kupeana majukumu.
“Tutawaita tukae, tuzungumze, tupange, tupeane majukumu na malengo ya kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, aliwaambia waandishi wa habari, kwamba chama hicho kina imani na Ndugai kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha bungeni.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wabunge wote wamuunge mkono mgombea huyo wa CCM kwa kuwa ana uwezo wa kuliongoza Bunge kwa mafanikio.
“Ndugai ni kiongozi mzuri, tuna imani naye na ana uzoefu wa kutosha bungeni. Kitendo cha Ndugai kupitishwa na chama kugombea nafasi hiyo, ni kielelezo cha jinsi Mkoa wa Dodoma unavyoheshimika kwa kuwa na majimbo kumi ya uchaguzi ambayo CCM imeshinda kwa kishindo, na pia Dodoma ni makao makuu ya chama tawala,” alisema Kimbisa.
UKAWA WAFANYA UTEUZI
Wakati hekaheka za uchaguzi wa Spika na naibu wake ndani ya CCM zikipamba moto, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), navyo vimefanya uteuzi wa wagombea wao.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, ilieleza kwamba katika kikao chao, Ukawa wamemteua Goodluck Ole Medeye, kuwa mgombea wa uspika kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge mteule wa Kaliua, Magdalena Sakaya, akiteuliwa kuwa mgombea wa unaibu spika kupitia Chama cha Wananchi (CUF).
“Baada ya mchakato wa ndani ya vyama na hatimaye maridhiano baina ya vyama vinavyounda Ukawa, tayari uteuzi wa wagombea uspika na naibu Spika umefanyika.
“Katika nafasi ya Spika wa Bunge, Ukawa imemteua Goodluck Ole Medeye ambaye atagombea uspika kwa tiketi ya Chadema na kwa nafasi ya Naibu Spika, Ukawa watawakilishwa na Madgalena Sakaya ambaye atagombea kwa tiketi ya CUF,” ilieleza taarifa hiyo ya Makene.
SOURCE:MTANZANIA
Post a Comment